Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Rose Kamili Sukum

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Naomba pia iwe nafasi pekee ya kuwapa pole ndugu zangu wapendwa wa Arusha, Walimu na wazazi waliopotelewa na watoto wao. Mwenyezi Mungu awape faraja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata hii fursa ya kuchangia bajeti ya Wizara hii ya maji ambayo naita kwamba iko ICU. Sababu ya kusema iko ICU, ukweli ni kwamba kama mwaka jana ilitolewa au iliidhinishwa bajeti ya bilioni 915.2 na haikutolewa yote na leo tena tunaidhinisha bajeti ya bilioni 632.6 ambayo hatuna uhakika wa kutolewa; na tena iko pungufu ya bilioni mia mbili themanini na moja ya bajeti iliyopita mwaka jana, maana yake Serikali yetu haifanyi kazi ya kukusanya mapato nchi hii.

Mhesimiwa Naibu Spika, sisi Watanzania hapa tuna vitongoji 64,677, hivi vitongoji vyote vinahitaji maji, lakini ukiangalia wanasema wametoa miradi 1,333 ndani ya vitongoji 64,677, ndiyo maana nimesema wako ICU.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji tukubaliane ni uhai na kwa kuwa maji ni uhai, ni uchumi, ni msingi wa amani na ni haki za binadamu, nadhani sasa ifike mahali tuangalie ni jinsi gani tukomboe nchi hii kwa ajili ya maji. Mbinu pekee ya kuikomboa ni kuhakikisha kwamba, hii bajeti inarudiwa upya, hii bajeti ikarekebishwe upya tuijadili ili Watanzania waweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maana kwamba, Mheshimiwa Rais mwenyewe alitoa Kauli Mbiu kwa wanawake kwamba, nitawatua ndoo za maji vichwani. Sasa hapo ni kutua ndoo za maji au ni kuwawekea ndoo za maji? Labda hatujui Kiswahili! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hilo napenda tulijue vizuri kwamba, kama ni kutua hizo ndoo basi nendeni kwenye sera ya maji ya mwaka 2002, kuhusu suala la miradi ya maji vijijini, kila mwananchi aweze kupata maji isizidi mita
400. Je, mpaka sasa hivi mna mita mia ngapi ambazo zimewafikia hao akinamama, kama mnataka kuendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namna pekee ya kuokoa hii Wizara, nawaombeni sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa pamoja hasa sisi wanawake, ili tuwakomboe wanawake wenzetu vijijini; mimi nina uhakika asilimia 99 tumetoka vijijini ndipo tukaenda mjini. Sasa mjue kabisa kwamba, akinamama wanachota maji kwa umbali mrefu sana, sio chini ya kilometa 20 wengine, wengine kilometa tano na kadhalika wanaamka saa 9.00 kwenda kuchota maji. Namna pekee ya kuwasaidia ili waweze kuleta maendeleo ni sisi kuhakikisha kwamba, tunaliomba Bunge hili kwamba hizi fedha ziongezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namna pekee ya kuongeza kwenye huo mfuko, tunaomba kuuliza ile tozo ya sh. 100/= tuliyoiomba kwa nini mliikataa? Kama mnaweza kufanya maendeleo au mnaweza kutoa zile fedha za maendeleo, ni kwa nini mlikataa ile tozo ya Sh. 00/= tusiitoze kwenye mafuta, badala yake mkakaa kimya? Mngetueleza tena kwamba haiwezekani kwa sababu bei ya mafuta inapanda. Bora tupande bodaboda kuliko kukosa maji. Kama tungekosa maji humu ndani nyie wanaume mngekuwa na vikwapa na sisi wanawake ni uvundo mtupu; sasa kwa nini tusiangalie suala la maji kwa wenzetu na tuwaokoe? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namna pekee ya kuboresha huo Mfuko wa Maji, basi tutafute namna nyingine ya Mfuko wa Barabara ichangie Mfuko wetu wa Maji sh. 100 ile ipatikane ili maji yapatikane vijijini. Mfuko wa Umeme upatikane, kwa sababu barabara huwezi kujenga bila maji. Kwa hiyo nao wachangie kwenye ule Mfuko wetu wa Maji ili tuweze kuboresha hiyo miradi ya maendeleo kwenye vijiji vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kujua…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.