Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote niungane na wenzangu kuwapa pole wazazi wote waliopoteza watoto wao katika ajali mbaya. Mungu aendelee kuwafariji na kuwatunza.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kila mtu na hakuna hata Mbunge mmoja anayekataa kwamba, kuna tatizo la maji nchini, kila mtu anakiri hilo na tatizo hapa inaonekana ni fedha. Kama kweli Bunge hili lina wajibu wa kuisimamia Serikali na kupitisha bajeti ya Serikali ni lazima tuungane kwa pamoja kuhakikisha Serikali inaongeza fedha katika bajeti ya maji ili kuwasaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni mama na bahati nzuri kuna Wabunge wengi wa Viti Maalum wanaotokana na akinamama. Mimi kwa umri wangu huu sijawahi kuchota maji hata bombani kwangu pale ndani, nje ya nyumbani kwangu. Ni utamaduni na desturi ya Watanzania na ya
Waafrika wengi kwamba, akinamama ndio sehemu kubwa wanashughulikia matatizo ya watu majumbani. Kama kweli tunataka tuwasaidie kama sio kuwatwisha ndoo kichwani ni kuwatua ndoo kichwani, tuongeze bajeti kwa ajili ya kuwanusuru akinamama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata nyakati nyingine hata kazi za kufanya za kuwasaidia watoto wao hawafanyi, kwa hiyo jambo hili ni serious sana. Kama kweli, tuna nia njema ya kulisaidia Taifa hili, tuisaidie Serikali ikaongeze bajeti, heri hata ikasimamisha shughuli nyingine ili wananchi wakapate maji. Wakati wa kiangazi mwaka huu mnajua jinsi nchi yetu ilivyopita katika janga la ukame; kama hali ikiendelea hivyo nani atakuwa salama katika nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi naamini kama tukiamua kama Bunge, tuirudishe bajeti Serikali ikaongeze fedha katika Wizara hii ya Maji ili wananchi wetu wapate maji. Kama tunakubaliana kuwasaidia akinamama hawa na si kwa unafiki, turudishe bajeti hii ili Serikali ione ni namna gani itafanya ili kuwasaidia akinamama kuondokana na tatizo la maji. Kama ni punda anayeswaga ni mama, kama ni ndoo ni mama anayebeba kichwani, kwa sababu hiyo na sisi wote tunatokana na mama, naomba tuungane kuwasaidia akinamama kuondokana na tatizo hili la maji. Hatujui mateso ya mtu anayebeba ndoo ya lita 20 kichwani kwa kilometa mbili au tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni uchungu wanajua hawa akinamama, tuwasaidie kuondokana na tatizo hili la maji nchini. Sikusudii kuzungumza matatizo ya maji kwenye jimbo langu kwa sababu hata fedha mlizotenga hazifai hata kuzungumza, lakini kama tuna nia njema turudishe bajeti hii, Serikali ikapitie upya, ili jambo hili lipate kufikia muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kama Serikali ina nia ya dhati ya kuwasaidia Watanzania; kama Serikali ina nia ya dhati ya kusimamia suala la maji nchini itasikiliza kilio cha Waheshimiwa Wabunge wengi hapa ndani ambao kila mmoja kwenye jimbo lake anajua adha ya kwanza tunayokutana nayo kama Wabunge wa vijijini ni suala la maji vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wetu hata kwenye mikutano hawaendi kwa sababu ya maji; na naamini hata Waheshimiwa Wabunge hawa wanaosimamia Wizara hiyo wanatoka vijijini, wanajua matatizo na adha ya maji. Naibu Waziri alikuja Monduli, aliona mazingira ya Jimbo lile; miaka 50 ya uhuru wananchi wetu bado hawajui watachota maji wapi, miaka 50 ya uhuru tunahangaika na akinamama wanaendelea kununua ndoo sh. 500/=, hii haikubaliki mahali popote, lazima kama Bunge tuisaidie Serikali kutafuta Suluhu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Monduli maeneo ya Mfereji, maeneo ya Sepeko, maeneo ya Moita, maeneo ya Esilalei na maeneo mengine ya Lepurka ambayo ni kame, miaka 50 ya uhuru wananchi wale hawajawahi kuona maji ya bomba. Naomba Serikali isikie kilio cha Waheshimiwa Wabunge ikarekebishe bajeti hii ili iwafae wananchi wa leo na vizazi vijavyo kwa ajili ya maisha yao ya sasa na maisha yao ya baadaye.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waheshimiwa Wabunge tuache itikadi katika hili, tuisimamie Serikali ikarekebishe bajeti yake. Haiwezekani bajeti ya bilioni mia tisa unapunguza kwa asilimia 30 halafu hata ya mwaka jana umepeleka kwa asilimia 19 halafu upunguze, leo utapeleka kwa asilimia ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali itwambie ni kwa nini bajeti ya maji ambayo imetekelezwa kwa asilimia 20 imeshushwa kutoka ile bilioni mia tisa kuja bilioni mia sita, ni kwa nini? Ni vigezo gani vinatumika? Au ni mpango gani Serikali inao katika kuondokana na tatizo la maji nchini? Kama haiwezekani tu-admit kwamba hili ni Janga la Kitaifa na hili tatizo la maji sasa Serikali imeshindwa, ili tutafute namna nyingine hata wahisani kutusaidia. Hatuwezi kwenda

kwa namna hii kama hatukubaliani kusimamia suala la maji ambalo ni tatizo kubwa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru.