Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Gimbi Dotto Masaba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema kwa siku ya leo ili niweze kutekeleza majukumu yangu kwa ajili ya wananchi wa Mkoa wa Simiyu. Vilevile nishukuru Mwenyenzi Mungu; amsaidie mwenyekiti wangu wa Kanda ya Ziwa Serengeti Mheshimiwa Heche aweze kupata nafuu ili aweze kuja kutekeleza majukumu yake. Nimeona jinsi ambavyo ameanza kunyemelewa na kashfa na kwa jinsi ambavyo namfahamu mimi siyo muumini wa kupinga maendeleo. Nafahamu hilo yeye ni Mwenyekiti na mimi ni Makamu wake kwa hiyo tunafanya kazi ofisi moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba tu nizungumze kwamba tunapozungumza Tanzania ya viwanda naamini kabisa hakuna Mtanzania anayepinga Tanzania ya viwanda. Hata hivyo ninachokiona ni kwamba hatuendani na kauli ya Tanzania ya viwanda. Ninasema haya kwa sababu katika taarifa ya Waziri amezungumza mambo mengi sana na mimi kama Mbunge ninayetoka katika Mkoa wa Simiyu tunapozungumza viwanda maana yake tunagusa malighafi za maeneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Simiyu tunalima kila kitu, lakini cha kushangaza sijaona mahali popote ambapo Mkoa wa Simiyu unazungumziwa kuhusu kupata kiwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi niliuliza swali ambalo linahusiana na viwanda ambavyo vilikuwepo kwa muda mrefu, viwanda ginnery na nilivitaja kama viwanda vitano, Nasa Ginnery, Ngasamo Ginnery, Maswa na Malampaka, viwanda vyote hivi vimekufa na nikahoji Serikali inampango gani kuvifufua viwanda ambavyo vimekufa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri alisema mkakati wa Serikali na jukumu alilopewa ni kuhakikisha viwanda vyote vilivyokufa vinafanya kazi. Sasa ninataka kujua kauli ya Serikali, hivyo viwanda ni lini vitaanza kufanyakazi ili wananchi wa Mkoa wa Simiyu waanze kunufanikana na viwanda hivyo vya kuchambua pamba?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia viwanda lazima tulipe kipaumbele zao la pamba. Mkoa wa Simiyu zao la pamba limekufa, wakulima hawalimi tena zao la pamba kutokana na kwamba soko hili la pamba halipo. Wananchi wanatumia gharama kubwa kuandaa mashamba ya pamba kama vile palizi pamoja na vitu vingine lakini cha ajabu wanakwenda kuuza kilo ya pamba shilingi 1,000; jambo ambalo siyo zuri hata kidogo kwa Watanzania wa Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninachotaka kuomba kama kweli Serikali inadhamira ya dhati na kwa kutambua Mkoa wa Simiyu kwamba ni wa wakulima wakubwa sana, ninaomba ipewe kipaumbele kikubwa sana ili kuhakikisha kwamba tunapata viwanda vya kila aina.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumza wakulima na wafugaji, Mkoa wa Simiyu tuna wakulima na wafugaji. Lakini pamoja na malighafi zote hizi hakuna kinachofanyika kule Mkoa wa Simiyu. Sisi ni wafugaji lakini cha kushangaza hakuna hata kiwanda cha kusindika nyama, hakuna. Wafugaji anapakia ng’ombe kwenye malori kupeleka Dar es Salaam. Mmewahi kuona wapi sisi binadamu tunakwenda Jiji la Dar es Salaam kutalii ng’ombe nao wanakwenda kuangalia jiji la Dar es Salaam? Ni aibu kwa Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini Serikali isitengeneze viwanda ili wananchi hawa waweze kunufaika? Mimi niombe sana, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda niko kwenye kamati yako. Kilio changu kikubwa sijawahi kuchangia nikizungumza suala la kimataifa. Mara nyingi nazungumzia Mkoa wa Simiyu na Wabunge wenzangu wanaotoka Mkoa wa Simiyu kila siku tunapiga kelele kuhusiana na suala ya Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunalima choroko, tunalima zao la alzeti, tunafuga, bado ndani ya mifugo tunazalisha mbolea, kwa nini sasa tusiwe hata na kiwanda cha kutengeneza biogas inatokana na vinyesi vya ng’ombe? Kwa nini kila kitu hakuna? Halafu tunakuja tunasema Tanzania ya viwanda! Sipingani na kauli ya Tanzania viwanda lakini matendo yetu hayaendani na Tanzania ya viwanda. Mimi niombe sana kwamba tuangalie ni namna gani tunaweza kuusaidia mkoa huu wa Simiyu ili tuweze kuendena na kasi ya Tanzania ya viwanda ambayo mnaizungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda wewe unatoka Mkoa wa Kagera. Mkoa wa Kagera unazalisha ndizi, lakini cha kushangaza sisi unatudanganya unatuambia una viwanda una nini, kwako hakuna hata kiwanda cha kuchakata ndizi, hakipo. Naomba uoneshe mfano sasa wewe vinginevyo utaingia kwenye mkumbo wa Mawaziri hewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika tumekuwa na changamoto katika historia ya Tanzania. Historia ya Tanzania tumeshuhudia kwamba Serikali imekuwa ikiyakopesha mabenki kutoka Benki Kuu kwenda kwenye benki ndogo ndogo wamekuwa wakiwakopesha. Wakikopesha fedha zile benki wananchi wetu wananufaika kukopa hususan akina mama ntilie.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni kwa mara ya kwanza Serikali ya Awamu ya Tano kunyang’anya fedha kwenye mabenki na kuzirudisha Benki Kuu; jambo ambalo limesababisha sana kuyumba kwa uchumi. Lakini hizi fedha zingekuwa kwenye mabenki ya kawaida mama zetu wangeweza kukopa, lakini sasa hivi wamefungia kule benki tumebaki tunalia; mama analia, baba analia kila mtu analia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wabunge form one tuliambiwa kwamba ukiwa Mbunge unakuwa na fedha nyingi sana. Lakini sasa hivi tunalia hata kuliko mwananchi wa kawaida. Jambo ambalo ni aibu kwa Taifa hili. Hata hivyo naamini kabisa kwamba Wabunge tuna hali mbaya lakini tunashindwa kulia kwa sababu ya utu uzima wetu, kwamba unawezaje kulia wakati na mtoto kule analia; kwa hiyo inabidi mama unyamaze kimpya uendelee kuumia polepole. Lakini mimi ninachokiamini kabisa ni kwamba baada ya miaka kadhaa tutajikuta tumepata maradhi ambayo yametokana na stress zilizosababishwa na ugumu wa maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoomba kusema sasa ni kwamba Mheshimiwa Waziri wa Viwanda atakapokuja kuhitimisha hapa nitahitaji kufahamu suala la viwanda vya ginnery vilivyokufa, ni lini vile viwanda vitafufuliwa, la pilli, nini tamko la Serikali itakapofika msimu wa kuuza pamba wananchi wauze kwa shilingi ngapi ili tuweze kuendana na kasi ya Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ninakushukuru sana Mungu akubariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante Kiwanda ambacho Mheshimiwa Waziri wa Viwanda anajifunia nacho ni kwamba kilianzishwa na kikundi cha
vijana kwa ajili ya kutengeneza chaki na Halmashauri ikaingia ikachukua hicho kiwanda. Kwa hiyo, ndicho tunachojivunia nacho. Lakini sisi tunadai viwanda vinavyotokana na pembe za ng’ombe tunaka tutengeneze hata vifungo.