Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Hamadi Salim Maalim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kojani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze mchango wangu kwa kumshukuru Allah kwa kunijaalia afya njema na kuweza kutoa mchango wangu katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Nchi yetu ni nchi ya kilimo ambapo wakulima huzalisha matunda kama maembe, machungwa, mananasi na mengineyo. Kwa vile tumekusudia kujenga Tanzania ya Viwanda kwa nini basi mazao kama hayo ambayo nimeyataja hapo juu ambayo huzalishwa kwa msimu tunashindwa kuyatengenezea viwanda na kuyasindika kwa matumizi ya baadaye?

Mheshimiwa Naibu Spika, matunda hayo kama yangesarifiwa nina imani kwamba nchi yetu ingeweza kuuza nje ya nchi na kupata fedha za kigeni na hivyo kupelekea kuongeza uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli tunataka Tanzania ya Viwanda ni vema tukaangalia kwa kina nini kilisababisha viwanda vyetu vingi vimekufa, tena vile ambavyo malighafi zake zinapatikana ndani ya nchi yetu. Kama tatizo ni wataalam basi kabla ya kuanzisha ufufuaji wa viwanda hivyo, basi vijana wapewe taaluma inayolingana na viwanda hivyo; lakini lakini tatizo ni uongozi mbovu basi ni vema kukawa na usimamizi wa hali ya juu au wa mara kwa mara ili kugundua hizo kasoro zinazopelekea viwanda kufa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania yetu ya leo tunazalisha mpira kwa wingi lakini General Tyre imekufa na tunaagiza mipira kutoka nje ya nchi. Pia tunazalisha ngozi kwa wingi lakini tunashindwa kuzalisha viatu, mabegi na hata mikanda, vitu vyote hivi tunaagiza kutoka nje ya nchi. Hivi kweli kwa msingi huo tuna lengo thabiti la kuwa na Tanzania ya Viwanda?

Mheshimiwa Naibu Spika, masikitiko yangu makubwa ni kushindwa hata kuanzisha viwanda vidogo vidogo ambavyo vingeweza kusaidia kutoa ajira ndogo ndogo kwa vijana wetu. Leo Tanzania ni nchi ya tatu katika Afrika kwa ufugaji lakini tunaagiza maziwa kutoka nje. Pia maembe yanazalishwa kwa wingi Zanzibar lakini yanasafirishwa katika nchi za kiarabu tena huuziwa hapa nchini kwa fedha zetu za Tanzania. Hili linalikosesha mapato mengi Taifa letu.