Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa nami nichangie hoja iliyoko mezani. Kimsingi hoja hii ni ajenda ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie Waheshimiwa Wabunge, tunapojadili hoja hii, tunapaswa kuwa Watanzania ili tuunge mkono jitihada anazofanya Mheshimiwa Rais, kiu ambayo Watanzania wamekuwa nayo kwa siku nyingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mjadala huu tunaojadili, ukiangalia haraka haraka, unaweza tu ukaingalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, lakini ukaacha kuangalia uamuzi wa makusudi ambao Serikali imeufanya kwa nia njema ya kutekeleza Sera yake ya Tanzania ya Viwanda. Ni bahati mbaya sana Watanzania tulio wengi huwa tunapenda matokeo ya haraka haraka kama ya kamari vile, kwamba unacheza halafu unapata matokeo; kama umepatia, umepatia; kama umekosea, umekosea.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo tunalolizungumzia leo, siyo jambo linaloota kama uyoga, ni jambo ambalo linahitaji utengenezaji wa vitu vingi sana ndiyo matokeo yake uweze kuyaona. Kwa mfano, leo hii tunavyoongea, tangu muda mwingi sana Serikali iliondoka kwenye sera ya kujenga viwanda, lakini leo tunapoongea kwenye Awamu ya Tano, Serikali imeweka mkono wake kwenye kujenga viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni hatua kubwa na ni utekelezaji wa vitendo wa dira ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa wakati wa Kampeni, wakati wa kuzindua Bunge, lakini pia na kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wengine mnasema Waziri anahamasisha, anahamasisha, lakini Serikali ilisema itajenga viwanda; mimi niwakumbushe, Serikali imetafuta dirisha ambalo itaweka mkono wake wa kujengea viwanda. Hivi leo tunavyoongea, Taasisi ama Mashirika ambayo yako chini ya Serikali kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, kwa Dira ya Mheshimiwa Rais, yamebadili mwelekeo ambao yalikuwa yakifanya kwa muda mrefu ambao haijafanyiwa tathmini na ikaingia kwenye utekelezaji wa ujenzi wa viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyoongea, PPF walishaingia mkataba na Magereza wa kufufua kiwanda cha viatu kule Karanga na mwelekeo na maelekezo tuliyoyapata na ambayo tumekubaliana kama Wizara, wateja wa kwanza tutakuwa watumishi wenyewe wanaopatikana kwenye vyombo vyetu vilivyoko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani na tutakwenda na kwenye Taasisi nyingine ambazo wanahitaji viatu hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, kwa tathmini ya haraka ni kwamba soko la bidhaa hizo zitakuwepo na hivyo itawezesha kiwanda kuwa endelevu. Maana yake lilikuwepo swali lingine kwamba ni namna gani mtahakikisha kwamba viwanda mnavyovijenga havitakufa? Kwa hiyo, moja ya sifa, utakuwepo upatikanaji wa soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tumeongelea hiki alichotoka kukielezea Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu mambo ya sukari. Ni kweli sukari bei yake imepanda ukilinganisha na miaka kadhaa iliyopita. Hata hivyo, Tanzania siyo kisiwa; panapokuwepo na bei za juu sana kwenye nchi zinazotuzunguka, ni kanuni za kiuchumi kwamba lazima na sisi tutaathirika na bei zitapanda. Ukiangalia kwa mfano, Uganda kwa bei ya Kitanzania sukari inakaribia Sh.5,000/=, ukienda Kenya inacheza kwenye Sh.4,300/= hadi Sh.5,000/=.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, kama tuna sukari kwetu huku na wao bei yao iko juu namna hiyo, ni lazima itaathiri bei kwa sababu watu watatorosha. Hatua za muda mfupi na za muda mrefu tunazochukua, kwanza tunakataza utoroshaji wa sukari na nimeelekeza taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani kuchukua hatua kwa wale wote watakaofanya zoezi la kutorosha sukari na kusababisha upungufu na kusababisha madhara ya bei katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijaishia kuchukua hatua za mpito hizo za kuzuia za kuweka doria, Mheshimiwa Rais ameelekeza na dira hiyo inafuatwa na Wizara zinazohusika ikiwepo kinara Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kazi, Wizara ya Mambo ya Ndani; hivi tunavyoongea, ndani ya wiki chache utekelezaji kwa maana ya kupata mtengenezaji wa kiwanda katika Gereza la Mbigili utakuwa umekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua za awali sasa hivi za utengenezaji wa mradi huo zilishatekelezwa na kiwanda hicho kitaweza kuzalisha sukari kati ya tani 30,000 mpaka 50,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maelekezo ya Mheshimiwa Rais, haijaishia hapo; kutakuwepo na mradi mkubwa wa Mkulazi ambao tuliuweka kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Rais na kwenye Hotuba ya Waziri wa Fedha na kwenye Hotuba ya Waziri mwenye dhamana ya Viwanda, katika vipindi vyote ambavyo amekuwa akisemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili unaona kwamba litaenda kutuondolea kabisa upungufu uliokuwa unajitokeza katika eneo hilo na liko katika hatua za mwisho za kwenda kwenye utekelezaji. Maandalizi ya eneo katika utekelezaji huo uko katika hatua za juu kama ambavyo atabainisha Mheshimiwa Waziri mwenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazingira ambayo ni tathmini ya jumla ya ajenda ya viwanda, wengine walikuwa wanasema kwamba mwekezaji atawekezaje wakati vivutio tumeviondoa?

Waheshimiwa Wabunge, siyo siku nyingi sana kwenye mijadala yetu, ukichukua Hansard za Bunge lililopita, mijadala yetu ilikuwa inajikita kwamba vivutio tunavyovitoa siyo vyenyewe. Kwa kuwa tulikuwa tunasema vivutio tunavyovitoa siyo vyenyewe, sababu tulizokuwa tunatoa ni kwamba baadhi ya nchi bado zinatuzidi kwenye wawekezaji ilikuwa ni aina ya vivutio. Sasa Mheshimiwa Rais amelenga kwenye vivutio vyenyewe ambavyo vinatumika Kimataifa, vinavyoondoa vikwazo kwenye uwekezaji na kuleta sifa halisi ya mwekezaji kuweza kuvutiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya vitu ambavyo vinavutia kwa kiwango kikubwa na Serikali imechukua hatua kubwa, Mawaziri wenye Sekta watasema kwa kirefu, mojawapo ni kasi kubwa inayofanyika kwenye umeme. Mojawapo ni kasi kubwa inayofanyika kwenye barabara; mojawapo ni kasi kubwa ya ujenzi inayofanyika kwenye reli na nyingine ni vita kubwa inayopiganwa ambayo Mheshimiwa Rais ameiishi kwenye maneno na kwenye vitendo ya mambo ya rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye nchi nyingine utasifia kwamba wamefanikisha mradi kwa haraka, lakini utakuta wametumia vibaya fedha za walipa kodi wa nchi zao. Sisi tunaenda katika utaratibu ambao tunapata mradi ukiwa umejumlishwa na matumizi bora ya fedha za walipa kodi. Kwa mwekezaji yeyote asiye mbabaishaji, atapenda sifa hizo kwamba pana umeme, pana amani, pana muunganiko wa kusafirisha bidhaa, lakini pia pana matumizi bora ya fedha za walipa kodi katika nchi husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vyote lazima vitaongeza ufanisi, vivutio vingine ambavyo tulikuwa tunavisema vya rejareja vinatumiwa zaidi na wawekezaji wababaishaji, lakini katika nchi zao ambako na nchi ambako tunatumia kama mifano walikowekeza vivutio vikubwa ambavyo ni standard katika uwekezaji, huwa ni vya aina hiyo na ndivyo ambavyo mwekezaji asiye mbabaishaji angependa avikute katika Taifa husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa dira yake hii na kwenye historia za nchi yetu Marais hukumbukwa watakapokuwa wameshaweka alama. Kwa hiyo, hizi kelele nyingi, miezi mitatu tu baada ya kumaliza awamu zake mbili, watakuwa wakiona mwekezaji mbabaishaji amepewa fursa, wanasema enzi za Mheshimiwa Magufuli hili lisingetokea. Watakuwa wakiona rushwa imetokea mahali wanasema enzi ya Magufuli hili lisingetokea hili, watakuwa wakiona viwanda vinaanza kufa, ama ndege zilizokuwa tano zinaanza kurudi kuwa nne, watasema enzi ya Magufuli hili lisingetokea. Sasa kwa sababu Tanzania itaendelea kuwa chini ya CCM, tuna hakika haya anayoyafanya Mheshimiwa Magufuli yanatengeneza viwanja kwa ajili ya nchi yetu kuweza ku- take off.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Watanzania wote wafunge mikanda, tuiandae nchi yetu, kwa dira ya Mheshimiwa Rais ili tuweze kuiona Tanzania ya viwanda na hiyo ndiyo itakayotengeneza ajira nyingi na sisi tutakuwa wauzaji wa bidhaa na sio waagizaji wa bidhaa kama ambavyo kwa kipindi kirefu tumeishi katika mazingira hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya pacha wangu na huku nikimshukuru kwa kuwekeza kwenye Gereza la Karanga ambako ukiondoa viatu vyako na vya Mheshimiwa Waziri Mkuu, basi humu Bungeni mimi ndio nimependeza zaidi viatu vilivyotoka Gereza la Karanga, vimetengenezwa hapa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.