Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Dr. Pudenciana Wilfred Kikwembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ili nami niweze kuchangia Hotuba ya Rais ambayo inalenga moja kwa moja kutatua matatizo ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda nitoe shukrani zangu za dhati kwa wananchi wangu wa Jimbo la Kavuu kwa imani kubwa waliyonipatia mpaka nikaweza kufika hapa nilipo, ni kutokana na uchapaji wangu wa kazi hawakuona kwa nini watoe kiongozi kutoka upinzani, wakaona wanipe mimi mwanamama, jimbo jipya, Mbunge mpya mwanamke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nianze moja kwa moja kujielekeza kwenye suala la elimu. Huu mpango wa elimu bure naomba niishauri Serikali yangu kwamba mpaka sasa bado una mkanganyiko, haueleweki kwa wazazi, walimu, wakurugenzi na wale wote wanaopaswa kuuelezea huu ukoje mpango, hata leo katika mijadala ya Maswali na Majibu limejitokeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niombe Serikali ifanye jitihada za makusudi ikauelezee mpango huu vizuri ili wazazi, wananchi waelewe majukumu yao ni yapi na nini kinatakiwa kufanyika mashuleni. Kwa sababu mmeshasema kuna changamoto na upungufu umeonekana basi mimi naamini Serikali itafanya kazi haraka iwezekanavyo kwa sababu tayari shule zimeshafunguliwa ili ziweze kuendelea vizuri na masomo. Naomba suala la elimu bure lifafanuliwe vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili niliwaahidi wananchi wangu wa Jimbo la Kavuu kwamba nitachangia chakula mashuleni. Nawaomba wale wote wanaopeleka propaganda hizi kwamba niliomba kwa sababu ya kupata Ubunge si kweli. Mimi ni mwalimu na najua maana ya elimu na nawahakikishia Wanakavuu ahadi zangu zote nitatekeleza kwa sababu ziko ndani ya uwezo wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende katika hotuba ya Mheshimiwa Rais ukurasa wa 11 inapoongelea kuunganisha barabara, Miji Mikuu ya Wilaya na Mikoa. Ukanda wa kwetu kule Rukwa, Katavi, Kigoma, Tabora bado barabara zetu hazijakaa vizuri. Barabara za ndani kati ya wilaya na wilaya bado hazijakaa vizuri. Naliongea hili na naomba Waziri wa Ujenzi kama yupo, nimeambiwa amekwenda kwenye dharura Kilombero lakini Serikali ipo, naomba ichukue hatua za dharura.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu hakuna mawasiliano kati ya Kata ya Ikuba, Chamalendi, Majimoto mpaka Mbede. Hivi ninavyoongea hakuna mawasiliano yoyote na ni eneo kubwa ambalo lina wananchi wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali ichukue hatua za dharura, waende wakaangalie, sina madaraja pale, madaraja manne yameporomoka kwa hiyo wananchi hawana mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu limetamkwa ndani ya Ilani na ndani ya mpango wa kutatua matatizo ya wananchi, naomba basi Serikali ijitahidi kwa kadri inavyoweza kuunganisha barabara za Mikoa, za Wilaya na maeneo mengine muhimu ya biashara. Nilishachangia katika Bunge lililopita, tutakapoweza kuunganisha barabara mpaka Kahama tutaweza kuuza mpunga na mahindi yetu sisi watu wa Katavi mpaka Darfur wanakopigana vita, hatutakuwa na shida tena ya soko la mazao yetu. Kwa hiyo, niwaombe kabisa mlichukulie kwa undani wake suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Serikali yangu kwa namna ya pekee ambavyo imejitahidi kusambaza umeme vijijini. Niiombe tu sasa, kasoro ndogo ndogo zipo hasa kwenye nguzo. Nguzo zile ni nyembamba sana, nyingine jamani hata mguu wangu ni mnene. Zile nguzi nyingine hazina hata kamba za ku-support hivyo nyingi zimelala, mradi ni mzuri sana. Mheshimiwa Waziri Muhongo najua uko hapa, tumekuwa tukishirikana mara nyingi katika kubadilishana mawazo, kule kwetu mvua ni nyingi mno, naomba mtuletee nguzo nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ni uwekaji wa nguzo zile, kijiji kinakuwa mbali nguzo inakuwa sehemu nyingine. Naomba wale mawakala wa REA kupitia kurugenzi husika ndani ya Wizara wafanye utafiti, waonane na watendaji wa maeneo husika kabla ya kuanza kuweka zile nguzo. Najua unakuja tu umeelekezwa, sasa sisi siyo robot, lazima tufanye mawasiliano na tuone hiki tunachokifanya hatupotezi pesa sanasana kinakwenda kulenga wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naongea hilo kwa sababu kwangu mimi kutoka Milumba mpaka Manga kwenda Kibaoni nguzo zimewekwa karibu na Mbuga ya Katavi ambako wananchi hawaruhusiwi kwenda kule na kijiji kiko upande wa pili. Kwa hiyo, naomba kama hilo linawezekana muongee na mkandarasi aliyepo kule aweze kuzihamisha nguzo hizo. Najua itakuwa ni gharama kwa sababu alipewa ushauri akawa mjeuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la migogoro ya ardhi limeongelewa. Naomba Wizara ya Ardhi na Maliasili wafike kule kwangu kwani zaidi ya kata sita zinapakana na Mbuga ya Katavi na misitu ya hifadhi. Ndugu zangu wa Kavuu ni wafugaji na wakulima, wana ng‟ombe wengi ambao wanapitiliza wanakwenda mpaka mbugani. Nakumbuka Mheshimiwa Rais alipofungua kampeni kwangu alianzia Majimoto, alitamka, kama TANAPA ama askari wa TANAPA wanakamata ng‟ombe wale hawaruhusiwi kuwapiga risasi. Tunapowaua wale ng‟ombe tunawatia hasara wale wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali sasa, kama ile sheria ya kutoza faini labda imekuwa ni ndogo basi bora tukaongeza faini lakini wale ng‟ombe wakamatwe wakiwa wazima tuwatoze faini ili itusaidie sisi kufanya kazi. Utakamata ng‟ombe 70 unaua ng‟ombe 70 au mwenye ng‟ombe anaweza kuja akakwambia ng‟ombe wangu ni 500, sasa ukiwakamata wakiwa wazima ni rahisi kuwaangalia na kuwa-identify ukajua ni ng‟ombe wangapi wamekamatwa na wakatozwa faini. Pia tunaendelea kutoa elimu kwa ndugu zetu wasiingie katika mipaka ya mbuga lakini haya ni matatizo ambapo Bunge lililopita Kamati iliundwa kwa ajili ya kuyashughulikia. Nimuombe Mheshimiwa Rais ashughulikie migogoro hii haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye suala la afya hasa katika kuwahamasisha wananchi kukata bima za afya. Tuna mifuko ya aina mbalimbali, tuna ule mfuko wa CHF ambao tunawahamasisha wananchi wajiunge. Kitu kinachojitokeza na changamoto iliyopo katika mfuko huu ni kwamba kama nimejiandikisha Kata ya Majimoto siwezi kutibiwa Kata ya Usevya, kama nimejiandikisha Usevya siwezi kutibiwa Kata ya Mamba, kwa maana mfuko ule unakubana pale ulipojiandikishia tu na ugonjwa hauwezi kukuambia utakupata pale ulipo. Mimi naweza kuwa nimetoka Mamba nimekwenda Mpanda Mjini nimeugua, ama nimepata referral kwenda Mpanda Mjini, siwezi kutumia ile kadi. Naomba hili nalo Wizara mliangalie kwa undani tuone tunatatuaje tatizo hili, ni sugu na lina-embarrass wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia naomba niongelee Mfuko wa Jimbo ambao umeongelewa katika hotuba ya Rais ukurasa wa kumi kwamba mfuko huo sasa pesa itapatikana kwa wakati. Naomba Serikali ama Wizara husika isianze kuwa na kigugumizi, tutekeleze hili haraka iwezekanavyo ili tuweze kuwahudumia wananchi wetu kwa wakati muafaka kwa sababu tumesema „Hapa ni Kazi tu‟ na tufanye kazi kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la hati miliki za kimila, naomba Serikali iharakishe kuzitoa kwa wale wanaomiliki mashamba kihalali ili waweze kukopa na wajikwamue kutoka kwenye umaskini, japokuwa baadhi ya benki imekuwa hazizitambui.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe sana, aidha mtuelekeze ni wapi wananchi wenye zile hati za kimila wanaweza wakapata mikopo ili waweze kujiendeleza badala ya kwenda benki unaambiwa sisi hiki hatukitambui, unataka kuweka dhamana ndugu yako kakamatwa, haitambuliki. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali yangu, kwa spirit tuliyonayo mimi naamini tutashinda na naamini tutavuka malengo katika kutatua matatizo ya wananchi, la msingi ni ushirikiano.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu wa Kata ya Usevya, najua hamtaniona sasa hivi lakini baadaye mtaniona, niwaombe sana wazazi wangu wa Kata ya Usevya, hao wazazi wanaowaambia msichangie, mmojawapo anaitwa Bulimba, mwingine Emma Godfrey, najua wanatoka upande gani wa chama, ni walewale wasiotaka kuchangia maendeleo …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha
kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba muda kidogo. Wazazi wangu wa Usevya, naomba mtumie busara katika kuchangia suala la elimu.
NAIBU SPIKA: Samahani Mheshimiwa muda wako umekwisha, naomba ukae.
MHE. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)