Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Ester Michael Mmasi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii, nami niweze kuchangia kwenye Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda mbele kwenye mada zangu, kwanza kabisa kwa unyenyekevu mkubwa na kwa nia njema kabisa, naomba niwapongeze viongozi wetu, Mheshimiwa Waziri na Naibu wake namwona anatabasamu kwa sababu anafahamu ninafahamu jitihada
zake, ninafahamu kiu yako kuona vijana wa nchi hii wanashiriki rasmi kwenye sekta ya kilimo. Nawapongeza sana, vijana wanawapongeza sana. Pia wanasema kwamba, asiyejua kushukuru huyo ni mnyang’anyi. Mimi siwezi kuwa mnyang’anyi kwenye Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri, ninanukumbuka nilikuja hapa Dodoma nikawafuata pale Wizarani, ninyi mlinipa kibali cha kuweza ku-organize vijana wote nchini Tanzania, wakaja tukapanga mipango. Siyo hivyo tu, mlinisimamia na mimi nikafanikisha azma yangu ya kuanzisha vikundi vya ushirika katika nchi ya Tanzania. Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, mnafahamu nimeanzisha Ushirika wa Vijana Wahitimu, nimeanzisha kule Buchosa, Geita, Bukombe, siyo hivyo tu, nimeanzisha Kigoma ambapo huko pia nimetafuta shamba ekari 1,000, Mto Malagarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, wamenisaidia nimeanzisha ushirika Songea, Dodoma, nimeanzisha ushirika wa vijana graduates Mkoa wa Dar es Salaam, lakini Mheshimiwa Waziri naomba tu kukwambia kwamba, vijana wale bado wanakusikiliza, wamekupa macho yao yote na matumaini yao kwako. Ninaomba kwa moyo wa unyenyekevu kabisa, usiwaache vijana wale. Uliwapa matumaini makubwa, uliwasimamia na ukasema utawaongoza. Ninakuomba usimame mstari wa mbele uongoze Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi katika mawasilisho ya Wizara ya Viwanda tuliona kabisa mpango wa Serikali katika kufufua viwanda. Najiuliza kule Mkulazi ambapo mnasema tutazalisha tani 200,000 za sukari, hatuoni kwamba huu mradi utahitaji outgrowers kwa maana kwamba utahitaji malighafi kutoka nje ya Mkulazi project! Tunawaandaaje vijana hawa?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, shamba la Mbigiri, mmesema mtazalisha miwa tani 30,000 kwa mwaka, mmewaandaaje vijana hawa? Ukiangalia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 31(v) umesema moja ya mikakati katika Wizara ni kuona kwamba vijana wanashiriki kwenye sekta ya kilimo kikamilifu.

Mheshimiwa Waziri najiuliza leo, tukiwa katika mawasalisho ya bajeti zenu huu mwaka wa fedha unaoisha Juni, 30 tuliona mipango mingi, nikauliza hawa vijana watashirikije? Mkasema kwamba atapewa hati za kimila ili waweze kukopesheka katika mabenki. Najiuliza tukiangalia fungu la maendeleo, tumetenga shilingi bilioni 101, lakini zimeenda asilimia tatu tu. Fedha za kawaida tulitenga shilingi bilioni 109, tunaona zimeenda shilingi bilioni 62 sawa na asilimia 54. Ninajiuliza, kwa nini vote three matumizi ya kawaida yanakuwa ni makubwa, lakini fungu la maendeleo linakuwa hamna kitu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza leo, katika hii shilingi bilioni 150 mliyoitenga this year, mtatupa shilingi ngapi vijana hawa waweze kupatiwa hati za kimila na waweze kukopesheka kwenye mabenki? Mheshimiwa Waziri unafahamu na umekuwa ukituhutubia hapa kwamba NMB wametenga shilingi bilioni 500 katika kusaidia vijana, lakini wewe ni shahidi, nimezunguka NMB wananijua, kama wapo waniangalie, CRDB wananijua, nimezunguka na vijana wa Taifa hili hakuna wanakokopesheka. Hiki ni nini?

Mheshimiwa Waziri, ona huruma kwa vijana wako. Unafahamu vijana wanavyokulilia, umepokea simu za mchana na usiku, tibu kilio cha Watanzania, tibu kiu ya vijana hawa waweze kushiriki kwenye sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Waziri unaelewa, wamekuja vijana, mara ngapi wanakupigia simu? Vijana wako tayari wanataka kulima. Siyo hivyo tu, CRDB, Agribusiness Loans Unit, nimekwenda pale wananijua. Nime-mark time several times; nimefanya vikao na Makatibu Wakuu, wananijua, wako hapa waulize. Nimeongea nao usiku na mchana, vijana hawasaidiki katika nchi hii.

Mheshimiwa Waziri unafahamu Benki ya Kilimo, tulitenga shilingi bilioni 60 lakini ombi la Dar es Salaam tu lilikuwepo bilioni 55. Ni nini hiki? Tukiwa wadogo tulisoma hadithi za Abunuasi, leo mimi na utu uzima wangu ukiniambia nisome kitabu cha Abunuasi siwezi kusoma. Mheshimiwa Waziri ninakuomba uangalie, Taifa linakutegemea.

Mheshimiwa Waziri, siyo hivyo tu, TIB, Women’s Bank tumeona, Women’s Bank sasa hivi ina-run the second with high growth rate in NPL; you know it! Mheshimwia Waziri unafahamu. Benki hii tuliambiwa kutakuwa na dirisha la akina mama waweze kukopesheka na waingie kwenye kilimo. Hamna kitu! TIB the same, it is running the third with higher NPL growth rate ambayo ina asilimia 52 Women’s Bank na hii TIB ina asilimia 32.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulifungwa vinywa hapa na Mheshimiwa Waziri wa Afya akatuambia kwamba CAG atafanya kazi atuletee ripoti. Waheshimiwa Wabunge wenzangu na akina mama wa Bunge hili, ninaombeni tusikae kimya, tuisemee Benki ya Wanawake. Wanawake wanatutegemea sisi tuwasemee. Tunajiuliza leo kama Benki ya Kilimo ilikuwa ina-operate under Central Bank guidelines, ilitakiwa iwe na Bodi. Benki hii inakuwa Head wa Risk Manager, kuna board members, watu hawa wamewajibishwa lini? Benki za Taifa hili zinakufa, wamama waende wapi? Vijana waende wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu. Tumeona mambo makubwa ambayo yametukatisha tama. Vijana hawa wanahangaika. Mmeongea kwenye Sera ya Ajira, lakini hakuna tumaini tena. Ninaowasemea hapa ni watoto wa maskini, pengine hatuwajui. Watoto wa maskini ni wale ambao tunapoenda kule kula nyama kwenye minada, ni wale watoto ambao wanakinga makombo yetu kwenye beseni, wanaenda nyumbani wanapika. Siamini kama kuna mtoto wa maskini ambaye anachungwa na mbwa kwenye nyumba yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wa maskini ni wale ambao tunapopeleka watoto wetu China, wanabeba mabegi, wanaenda airport wanawapungia watoto wa matajiri mikono. Hawa ndio watoto wa masikini ninaowasemea katika Bunge hili. Mheshimiwa Waziri tuna imani nawe, ukiamua inawezekana. Wizara yako ikiamua vijana wetu watashiriki rasmi kwenye Sekta ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anafahamu asilimia 75 ya wananchi wa Taifa hili ni wakulima, usiwaache; lakini asilimia 65 za ajira za uhakika zinapatikana kwenye Sekta ya Kilimo. Vijana wamenituma niwasemee. Vijana wamenituma nipaze sauti zao kwa niaba yao. Nakuomba kabisa utakapokuja kuhitimisha hapa, utuambie una mpango gani kwa vijana hawa waweze kushiriki kwenye project ya Mbigiri - Morogoro, utuambie vijana hawa watashiriki vipi kwenye National Milling ambayo umesema inafufuliwa hapa Dodoma. Malighafi hizi, vijana wana nguvu za kutoa malighafi kwenda kwenye viwanda hivi. Nakuomba uwashirikishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliongea habari ya AGOA, kuondolewa vikwazo vya kimasoko kwa nchi ya Marekani kupitia mlango wa SADC. Najiuliza, ni nani aliyeweza kufaidika kwenye mlango huu wa AGOA? Wanatoka Wahindi nchi ya India wanakuja Tanzania wananunua cashew nut yetu, wanapitia kwenye mradi huu wa AGOA, Watanzania tumebaki watazamaji!

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa linasikitika, linahuzunika, tusaidie Mheshimiwa Tizeba una uwezo. Mheshimiwa Olenasha mna uwezo na mna nguvu; na ninajua mna passion ya kweli katika Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha popote alipo na mama Ashatu Kijaji, tunawaomba kabisa kwa moyo wa dhati na unyenyekevu, Taifa linawaangalia. Toeni hela wasaidieni akina Mheshimiwa Olenasha wafanye kazi. Toeni hela Mheshimiwa Tizeba aweze kufanya kazi, Taifa linawaangalia. Ninaomba kwa moyo wa dhati na unyenyekevu, Bunge hili lisikie sauti ya vijana wa Tanzania hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani nisiendelee sana, pengine ninaweza nikafika sehemu nyingine. Naomba niishie hapo, naunga mkono hoja asilimia mia. Ahsante sana.