Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nami kuweza kuchangia Wizara hii ya Kilimo. Nimesimama kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Mbeya, kila mtu hapa anafahamu Mkoa wa Mbeya ni mkoa ambao unaweza ukalisha nchi hii vizuri lakini bado nashangaa kwa nini Serikali haitaki kuwekeza zaidi katika mkoa huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda hasa kwa kuchambua Mkoa wa Mbeya nitazungumzia Wilaya ya Kyela. Wilaya ya Kyela ina mambo mengi ambayo yanaweza kulisaidia Taifa hili. Tunafahamu Ziwa Nyasa linatoa samaki wa aina nyingi ambapo kama tukiwekeza katika lile ziwa tunaweza tukasafirisha samaki katika nchi yetu wenyewe lakini katika soko la Afrika Mashariki. Tunafahamu Kyela kunapatikana cocoa, Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha hotuba yake atuambie ni nguvu gani amewekeza katika zao la cocoa. Tunajua cocoa inanunulika sana katika soko la dunia lakini mwananchi wa Kyela amefaidikaje na zao hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye mpunga, Wabunge mnafahamu kuna mahali mpaka tunadanganywa mpunga wa Kyela, kwa nini tusiwekeze katika mpunga huu kama unapendwa na una soko zuri kuweza kusaidia wale wakulima wadogo wadogo ambao pia wengi wao ni wanawake tukaweza tukapata zao hilo na faida yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua hii Benki ya Kilimo kwa nini isiende kusaidia wananchi wa Mkoa wa Mbeya. Wananchi wanapolima tatizo kubwa tunaona ni mitaji, twende mahali tuachane na kilimo cha jembe, tunahitaji kilimo cha kibiashara ili kuweza kumkwamua mwananchi katika kujiendeleza maisha yake ya kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la Benki ya Kilimo, najua ipo Dar es Salaam sijui kama ina matawi, kama ina matawi hayafanyi kazi, ukienda huko kwetu Rugwe, Kyela, Mbarali hakuna mwananchi anayeijua na wala hata kupata maelezo ya benki hii ikaweza kuwasaidia hawa wananchi. Naomba Wizara ichukue juhudi za makusudi kusaidia wanawake na wananchi wa Mkoa wa Mbeya waweze kujua maana ya kuwa na Benki ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia pembejeo. Pembejeo imekuwa ni tatizo kubwa sana katika Mkoa wa Mbeya. Kwanza haziji kwa wakati, pili nyingi ni feki, hata hatujaelewa Serikali imechukua hatua gani kwa wale walioleta pembejeo zisizofaa. Naomba kwa bajeti ya mwaka huu pembejeo zifike kwa wakati na zilizo bora kwa sababu hata Wabunge wenzangu wamelalamika mazao hayatoki mengi ni kwa sababu mbegu hizi si bora na hata hizi mbolea zinazokuja si sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara isimamie na ituambie inafanyaje na kama inaweza ikabadilisha mtindo ambao unatumika sasa wa ugawaji wa pembejeo kwa sababu wachache wananufaika na wakulima wanaingia kwenye nafasi ambayo haziwafikii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia suala la chai, nimezungumza mara nyingi katika Bunge lako Tukufu nikilalamika juu ya wakulima wa chai wadogo wanavyolalamika chai isivyowasaidia wao kama wakulima. Ni watu wachache sana wananufaika na zao la chai, mwananchi wa kawaida chai bado iko chini wakati chai inauzwa bei nzuri soko la dunia lakini sisi wenyewe Tanzania tunahitaji kunywa chai kwa nini chai isimnufaishe mkulima wa Mkoa wa Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia mazao, Mbeya ina mazao mengi sana. Sisi sote tunafahamu unapotaka kupata karoti unapata Mbeya, unapata viazi lakini linakuja tatizo kwenye soko, bei ya mkulima ni ndogo anayefaidika ni mtu wa katikati ambaye ni dalali. Tunawezaje kusaidia wakulima wakauza mazao yao kwa bei ambayo ni nzuri. Mwananchi wa kawaida anahangaika kulima mwisho wa siku anauza gunia la viazi Sh.25,000, Sh.20,000 au Sh.30,000 lakini ukija Dar es Salam gunia hilo hilo linauzwa kwa Sh.150,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali inamsaidiaje mwananchi huyu aweze kuuza kwa bei kubwa na tunajua kabisa mpaka sasa kuna watu wanatoka Kenya wanakuja huku kwenye masoko yetu na mashamba yetu bado wananunua kwa bei ndogo. Tunahitaji wateja waje lakini Serikali inawabanaje wanunue kwa bei inayomnufaisha mkulima wa kawaida?

Tunapozungumzia kilimo tunahitaji kuwekeza kwenye kilimo kweli kweli wala si katika maneno. Tunapozungumzia mpunga, tumezungumzia mpunga wa Kyela ulivyo mzuri lakini tuna Mbarali, Mbarali kuna shamba kubwa sana la mpunga lakini je Serikali imewasaidiaje wale wakulima wa Mbarali, imesaidiaje wale wakulima….

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)