Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Naanza na NFRA. Kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo hayatabiriki naomba sasa hii NFRA iongezewe nguvu, iongezewe fedha ili kwanza iweze kununua mazao ya kutosha na kwa wakati na kwa bei muafaka. Pili iongezewe fedha ili tuweze kuhifadhi mazao yetu kwa njia za kisasa zaidi na tuepukane na ile kuhifadhi katika maghala twende kisasa zaidi ambapo mazao yetu yatakaa kwa muda mrefu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu ukulima na ufugaji unaohifadhi mazingira. Nashauri Wizara ya Kilimo ishirikiane na Wizara ya Maji hawa wafugaji ambao wana mifugo mingi wahamasishwe na wapewe elimu ya kuhifadhi maji ya mvua kwa ajili ya mifugo yao huko wanakoishi. Katika ukulima nashauri Serikali ihimize zaidi hasa wale wanunuzi wakubwa mfano wa tumbaku, waje na yale majiko ya kisasa ya kukaushia tumbaku ili kuepusha ukataji wa miti yetu kiholela ambayo inatumika kukaushia tumbaku. Naomba yale majiko ya tumbaku yapewe hamasa zaidi ili yatumike tumbaku yetu ikaushwe kwa majiko ambayo hayahitaji kukata miti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza uvuvi wa bahari kuu kwa Serikali kuamua kwa makusudi kujenga au kuendeleza gati namba sita na gati namba tatu ya kule Zanzibar kwa ajili ya kupokea na kuhifadhi samaki wa bahari kuu. Naomba hili Serikali ilitilie mkazo, hizo bandari zimalizike kwa haraka ili nchi yetu iweze kupata mapato ya fedha za kigeni na ajira kwa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba Serikali yetu ina dhamira ya dhati kabisa katika kumsaidia mkulima na mvuvi wa Tanzania. Kwa maana hiyo kwa makusudi imeondoa tozo mbalimbali na kodi mbalimbali zitakazomsaidia mvuvi na mkulima. Dhamira nyingine ya dhati ni kuweka ununuzi wa pamoja wa mbolea, hizi zote ni mojawapo ya dhamira za dhati za kuwasaidia wakulima wetu na mvuvi ili waondokane na tabu ndogo ndogo zinazowakabili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na naipongeza Wizara kwa marekebisho ya baadhi ya kanuni za mamlaka katika uvuvi wa bahari kuu. Naomba Kanuni hizi zitumike kwa haraka ipasavyo ili ziweze kutuletea mapato katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongeza kwenye Benki ya Kilimo, nashauri benki hii iongezewe mtaji ili iweze kusaidia wananchi kulima ikiwemo kuhamasisha vikundi vidogo vidogo vya vijana na wanawake kuwapa mkopo ili Wizara ya Kilimo itoe utaalam wa ukulima na utengenezaji wa mbegu bora ili wananchi wetu wapate mbegu bora ambazo zitaendana na soko, uchumi wa kati na uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.