Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Waziri Dkt. Tizeba, Naibu Waziri Mheshimiwa Olenasha, Watendaji wote wa Wizara kwa kutuletea bajeti yao ili tuweze kuipitisha Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, napenda kuongelea kuhusu bima ya kilimo. Ni lini Serikali itaweka utaratibu wa kuwapatia elimu wananchi ili waweze kuweka bima kwa ajili ya kilimo? Kwa sababu kilimo chetu nchini kimekuwa hali ya hewa haitabiriki na pia Serikali haijaweza kuwa na uwezo wa kutoa pesa ya kutosha kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji. Tulipotembelea nchi ya China tulijifunza mengi yanayohusu kilimo mojawapo ni kuwaelimisha wananchi kuwa na Mashirika ya Bima ya Kilimo ili pia itawasaidia hata kukopesheka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Benki ya Kilimo. Tunaipongeza Serikali kwa kuanzisha Benki ya Kilimo nchini ambayo ilikuwa ndiyo kilio chetu na tukiamini ndiyo mkombozi kwa wakulima ambao ndiyo walio wengi. Ni kwa nini benki hii Makao Makuu yasiwekwe Dodoma ambako ndiyo katikati ya mikoa yote iwe rahisi na kuweza kufikika kirahisi? Vilevile ni kwa nini benki hii isiweze kufunguliwa madirisha katika mikoa na wilaya ili kuwatendea haki wakulima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kilimo cha umwagiliaji. Mkoa wa Iringa una eneo linaweza kumwagiliwa lenye jumla ya hekta 54,446, kati ya hekta hizo zinazomwagiliwa kwa sasa ni hekta 25,575 sawa na asilimia 47 ya eneo lote. Mazao makuu yanayolimwa kwa skimu za umwagiliaji ni pamoja na mpunga, mahindi, nyanya, vitunguu, mbogamboga na matunda. Mkoa wetu una jumla ya skimu za umwagiliaji 48 katika mchanganuo ufuatao; Iringa 32, Kilolo tisa (9), Mufindi tano (5) na Manispaa ya Iringa mbili (2).

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii miradi ya Manispaa ya Iringa ni miradi ya muda mrefu sana, Serikali imekuwa haitoi pesa kwa ajili ya miradi hii na tunategemea miradi hii ingeweza kusaidia vijana wetu hawa wa mjini waweze kujiajiri kupitia kilimo. Je, Serikali inatumia vigezo gani kutoa pesa kwa miradi hii ya kilimo cha umwagiliaji? Pia baadhi ya miradi ya umwagiliaji maji kutokamilika vyema na mingine haihitaji ukarabati wenye gharama kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za jumla katika kilimo katika Mkoa wetu wa Iringa ni kama zifuatazo:-

(a) Mtawanyiko mbaya wa mvua/ukame unaochangiwa na mabadiliko ya tabianchi;

(b) Uhaba wa mikopo yenye riba nafuu na isiyohitaji dhamana kubwa kwa kuwa wakulima wengi hukosa vitu vya kuwekea dhamana;

(c) Kuendelea kupungua kwa rutuba katika udongo suala linalosababisha wakulima wengi kuwa na mahitaji ya matumizi makubwa ya mbolea;

(d) Bei kubwa ya pembejeo za kilimo hasa mbolea na mbegu bora kunakosababisha wakulima gharama za uzalishaji wa mazao ya kilimo kuongezeka mara kwa mara;

(e) Magonjwa ya mimea hasa nyanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali inasaidiaje changamoto hizo kwa sababu asilimia 75 ya wananchi wa Iringa ni wakulima na ndiyo wanaochangia pato la mkoa.