Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Rashid Ali Abdallah

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tumbe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachangia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kuangalia mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakulima Wadogo; Tanzania ni nchi ya wakulima na wafanyakazi lakini sekta hii ya kilimo inachukua asilimia 65.5 ya wakulima kama alivyosema Mheshimiwa Waziri katika ukurasa wa nne wa hotuba yake. Kwa maana hiyo, ajira hii kwa Taifa ni kubwa sana na kuna haja ya Serikali kupitia Wizara yake kufikiria hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wadogo wadogo wana juhudi kubwa za kilimo na kwa kiasi fulani wanazalisha sana. Tatizo mazao ya wakulima yanaharibika na kuoza kwa kukosa soko. Mazao kama mahindi, maembe, nyanya, mananasi; matunda haya yanapotea kila mwaka na hivyo wakulima hawa wanapata hasara kubwa na kupoteza nguvu zao. Kwa sababu hiyo ni lazima kuwepo na soko la wakulima wadogo wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Matumizi ya Ardhi; wakulima wengi sana wanatumia ardhi kinyume na mahitaji ya mazao yanayotakiwa. Ardhi ambayo inafaa kuotesha kunde wanaotesha mananasi na vinginevyo. Hivyo, ushauri wangu ni kwamba kuwe na utafiti kuhusu zao gani lioteshwe katika ardhi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Utunzaji Mbaya wa Chakula; ni jambo la kusikitisha sana kuona wakulima wakizuiliwa kuuza mahindi yao nje na matokeo yake yakanunuliwa na Serikali na kuhifadhiwa NFRA, tani 13.583 yenye thamani ya Sh.6,793,310,000/=. Mahindi haya yaliharibika na yamesababisha hasara kubwa kwa Serikali. Hata hivyo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi akizungumza na waandishi wa habari alisema anatarajia kuwa mahindi hayo hayakuharibika. Je, ni hatua gani Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi alichukua dhidi ya uzembe huu uliosababisha hasara kubwa kwa Serikali? (kwa kupoteza Sh.6.793,310,000/=)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Migogoro ya Wakulima na Wafugaji; kwa taarifa tunazo hekari milioni 88.6 za nchi kavu. Hekari milioni 60 ni mbuga zinazomfaa mfugaji. Mbuga hizi zina uwezo wa kulisha mifugo milioni 20 (livestock unit), zilizopo ni 17.1 milioni. Unit tulizonazo ni 20, kwa maana hiyo Serikali ina uwezo mkubwa wa kuondoa mzozo/mgogoro huu. Kwa hiyo zitumiwe hizo units milioni 17.1 kutoka units milioni 20 kutatua mgogoro huu wa wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uvuvi wa Bahari Kuu; meli za uvuvi wa Bahari Kuu zinatolewa leseni dollar 50,000 na kuruhusiwa kuvua samaki idadi yoyote na wale wa ziada wanatupwa. Mheshimiwa Waziri analijua hili, lakini agizo lake la samaki wa ziada waletwe nchini ni kwa sheria gani? Huu ni upotevu wa makusudi wa mazao ya bahari kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima kuwe na sheria maalum kwa idadi ya uvuvi wa samaki wa Bahari Kuu na kuwe na sheria inayowataka wavuvi kuwapeleka samaki wa ziada nchini kinyume na angazo la Waziri pekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.