Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu kwa mustakabali wa maisha ya wananchi wangu wa Mkoa wa Singida na Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye amenijaalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Naipongeza sana Serikali ya CCM na Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri na kubwa wanayoifanya ya kuwaletea Watanzania maendeleo ya haraka na yenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mfupi Serikali ya Awamu ya Tano imeweza kufanya mambo mengi na makubwa. Mfano, ujenzi wa reli ya kisasa, uboreshaji wa miundombinu ya barabara na madaraja, utoaji wa huduma bora za afya na elimu na kujenga nidhamu katika rasilimali za Taifa letu. Hii yote inaonesha jinsi gani Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alivyo makini na timu yake. Nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunatambua kwamba maji ni uhai katika maisha ya mwanadamu. Maeneo ambayo hayana maji hakuna maendeleo, shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii zinategemea uwepo wa maji, hivyo basi ningeishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kutunisha Mfuko wa Maji kwa kuongeza tozo ya maji ya lita ya petrol na diesel kutoka shilingi 50 hadi shilingi 100 ili kutunisha Mfuko huo kwani mfuko huo wa maji umekuwa ni mkombozi mkubwa kwa maendeleo ya miradi mingi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanufaika wengi wa Mfuko huu wa Maji ni wale wanaoishi mijini. Hata ukitazama katika kitabu cha bajeti ya maji ukurasa 192 hadi 193 unaweza ukaona kwamba miradi mingi iliyonufaika ni ile iliyoko mijini hivyo ningeiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupeleka angalau asilimia 70 ya makusanyo ya tozo hii iende maeneo ya Vijijini ambako ndiyo kwenye matatizo makubwa ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuweza kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 na kufanikisha malengo ya uchumi wa viwanda ni vema sasa Serikali ikaangalia uwezekano wa maeneo mengi kupata maji kwa urahisi. Vilevile kuunda chombo cha usimamizi wa miradi ya maji vijijini kama ilivyo REA ili kupambana na changamoto za maji vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wa Mkoa wa Singida ambao ni wachapakazi na wabunifu, kama maji yanapatikana wakati wote wanaweza kutumia fursa hii kwa kulima mazao ya chakula na biashara kwa mwaka mzima na kuongeza pato la Taifa. Lakini kwa Mkoa wa Singida mambo yamekuwa ndivyo sivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na adha kubwa wanayopata wananchi wa Mkoa wa Singida kutokana na ukosefu wa maji safi na salama, na changamoto nyingi zilizopo katika Mkoa wa Singida bodo bajeti ya mwaka huu ya miradi ya maendeleo ya maji imepunguzwa kutoka shilingi bilioni 6.7 kwa mwaka huu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja