Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Mbarouk Salim Ali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Wete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MBAROUK SALIM ALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mheshimiwa Spika, uwazi ni nyenzo muhimu ya Utawala Bora. Mtawala yeyote, ambaye utendaji wake ni wa kifichokificho, huwa anatiliwa shaka kwamba kuna jambo ambalo halistahili analofanya kwa siri na mtawala wa aina hiyo huwa haaminiki na wale walio chini yake.
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya CCM imevunja kanuni muhimu ya utawala bora ambayo ni uwazi (transparency) katika uendeshaji wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa Mbunge katika Bunge la Kumi na namshukuru Mungu nimerudi tena katika Bunge hili la Kumi na Moja. Kwa miaka yote mitano ya uhai wa Bunge la Kumi suala la kukosekana kwa uwazi katika Mikataba mikubwa ya uwekezaji katika sekta za nishati, madini na uvunaji wa maliasili nyingine limeitia doa Serikali hii ya CCM kwamba pengine ina ajenda ya siri ya kuwaibia wananchi kupitia mikataba hiyo ndiyo maana mara zote haikubali kuweka mikataba hiyo wazi ili wananchi waijue.
Mheshimiwa Spika, Wabunge humu walishapendekeza kwamba mikataba yote ambayo Serikali inaingia na wawekezaji katika nchi yetu iletwe Bungeni ili ijadiliwe kwa uwazi ili kuliepusha Taifa na hasara kubwa inayotokana na wizi wa hila unaofanyika kwenye mikataba inayosainiwa kwa siri.
Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa Bunge la Kumi lilimaliza muda wake bila kutuletea Mkataba hata mmoja Bungeni. Bunge la Kumi na Moja limeanza, Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani mambo ni yale yale, hakuna uwazi katika mikataba mikubwa ya uwekezaji.
Mheshimiwa Spika, binafsi napata shida kuelewa Serikali inapata wapi ujasiri wa kutumbua majipu ya watu wengine wakati kuficha mikataba ya uwekezaji nalo ni jipu tena lililoiva? Nafikiri kama Serikali iko serious kukomesha ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma ingeanza kujitumbua yenyewe kwa kushindwa kuweka wazi mikataba hiyo ambayo inasadikiwa kulinyonya Taifa na kuliacha hoi kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, nataka Serikali ijue kwamba kitendo cha kukosekana kwa uwazi katika Mikataba, kinaiondolea sifa ya utawala bora.
Mheshimiwa Spika, natambua kwamba katika utendaji wa Serikali kuna masuala fulani fulani ambayo huwa ni siri. Masuala hayo ni yale yahusuyo Menejimenti ya Rasilimali Watu ili kuhifadhi taarifa binafsi za Watumishi, lakini hakuna usiri katika masuala yahusuyo miradi au mikataba inayotekelezwa kwa kutumia fedha za umma.
Mheshimiwa Spika, unapoweka usiri katika masuala hayo, harufu ya ufisadi na ubadhirifu inaanza kusikika. Kwa hiyo, kitendo cha Serikali hii kutokuwa na uwazi, kunaifanya ikose mamlaka ya kimaadili (moral authority) ya kusema kwamba inapambana na ufisadi wakati ufisadi wenyewe umejificha kwenye mikataba hiyo ambayo Serikali inafanya kwa siri.