Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi kwa Waziri na Wataalam wake wote. Pamoja na hotuba yao nzuri, napongeza hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani na Kamati ya Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, rushwa ni adui wa haki. Wananchi wengi wanakosa haki zao za msingi karibu kila mahali hasa kwenye vyombo vya kutoa haki; Mahakimu wengi wanaongoza kwa rushwa, mahospitalini, kwenye kutafuta kazi; kwenye makampuni wapo wanaopoteza maisha sababu ameshindwa kutoa rushwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, TAKUKURU haina meno – haina mamlaka ya kushtaki, ni mpaka ipeleke faili kwa DPP. Serikali ieleze ni lini sheria ya TAKUKURU italetwa Bungeni ili wapewe meno?
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa MKURABITA kwa kiasi kikubwa haujaweza kusaidia wananchi wa chini (wanyonge). Pamoja na kuwa na dhamira nzuri, lakini bado wananchi wengi wanakosa mikopo Benki, pamoja na kuwa na nyumba ambazo hazina hati na viwanja ambavyo havijajengwa. Ni kwa nini wananchi hawa wanakosa mikopo kwenye Taasisi za fedha wakati kuna MKURABITA?
Mheshimiwa Naibu Spika, Wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hawakulipwa mafao yao. Ni miaka 30 na zaidi sasa wanadai haki zao bila mafanikio. Serikali ya Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamini Mkapa, Rais Mstaafu aliwalipa robo. Serikali ya Awamu ya Nne iliwapiga mabomu wazee hawa walipokwenda Ikulu kudai mafao yao. Hii ni aibu kubwa kwa Taifa kuwapiga wazee waliotumikia nchi yao kwa uaminifu bila wizi wala ufisadi na wengi wao ni maskini. Serikali hii itawalipa lini wastaafu hawa mafao yao ambayo ni haki yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa TASAF umesaidia wananchi maskini na watoto, baadhi wameweza kwenda shule. Serikali itoe tamko na agizo kwa Kamati za Mfuko wa TASAF wanaoiba fedha za wahitaji. Utaratibu wa kuibua wahitaji kwenye mikutano ya hadhara usimamiwe na Serikali. Watendaji wanaweka watu/familia zao zenye uwezo. Familia zote maskini zipate nafasi katika Mfuko huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Walimu wengi walioajiriwa mwaka 2014/2015, katika Wilaya ya Kaliua, hawajapata mishahara yao ya mwezi Mei na Juni. Orodha na majina yao yako Utumishi. Ni kwa nini hawalipwi mishahara yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia suala la kuchelewesha mishahara ya Walimu inawakatisha tamaa na kuondoa moyo wa kazi na kwa kuzingatia mazingira ya kazi yao, ni magumu na mishahara ni midogo. Vile vile Walimu hawapandishwi madaraja kwa wakati na hivyo kutopandisha mishahara yao kwa wakati. Hakuna Taifa bila Walimu!
Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo cha Serikali kuzuia Watanzania kuona Bunge Live ni kuwanyima wananchi haki yao ya msingi kuona/kutazama chombo chao cha Uwakilishi. Hili Bunge ni chombo pekee ambapo kila Mtanzania anawakilishwa, wana haki ya kujua nini kinaendelea. Kama suala ni bajeti ya Serikali ya TBC1; kuna vyombo vya binafsi. Kwa nini wanakatazwa kuonyesha? Serikali inaogopa nini? Inaficha nini? Hii ni aibu kubwa na huo utawala bora uko wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Kaliua kuna maeneo wananchi (Wasukuma) wanajichukulia hatua mkononi na kuwatoa Viongozi waliochaguliwa kwenye nafasi zao na kutaka kuwaua/kuwajeruhi na hakuna hatua za kiserikali zinazochukuliwa kwa watu hawa. Matukio yote yameripotiwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Kaliua na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa. Serikali ichukue hatua mapema kuondoa kasumba hii.