Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Gibson Blasius Meiseyeki

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arumeru-Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. GIBSON B. OLE-MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na zaidi pia kwa kulipatia jina langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa maombi kwa Mheshimiwa Waziri; nimkumbushe tu kwamba, kuna kile kilio chetu ambacho wananchi wa Kata yangu ya Bwawani walilia mbele ya Waziri Mkuu na wakaahidi kwamba mgogoro ule wa ardhi wangeufanyia kazi na yeye alikuja pale na akaagiza vijana wake waweze kufanya kazi ile. Hata hivyo, mpaka sasa ni zaidi ya miezi sita hatujapata mrejesho wowote. Kwa kweli wananchi wananisumbua sana kuhusiana na mgogoro ule wa ardhi ulioko pale Kata ya Bwawani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna wananchi wangu wa Kata za Oldonyosambu na Olkokola ambao ardhi yao ilitwaliwa na Jeshi na ilikuwa wapewe fidia, lakini baadhi yao hawakupata. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ningeomba badaye atuambie mahali ambapo imefikia, ili tuweze kupata majibu ya kuwapa wananchi wale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Arusha DC imezunguka Jiji la Arusha kwa pande zote. Kiukweli, influx ya wananchi sasa hivi katika Mji wa Arusha ni kubwa sana na wote asilimia zaidi ya 80 wanakuja Arumeru, hasa Jimbo langu la Arumeru Magharibi. Ardhi kule inazidi kuwa finyu na ninachokiona huko mbele ni migogoro zaidi za ardhi ikiwa kama hakutakuwa na jitihada za makusudi za kuhakikisha kwamba, wananchi wale wanaokuja maeneo yale ama wale wakazi wa maeneo ya Arusha ambao wengi wao ni wafugaji na wanapenda kulima, ardhi inazidi kuwa finyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri kwamba, kuwe na mpango wa kupata mapori au mashamba pori yale ambayo yapo, hayajaendelezwa, ili vijana hawa ambao wako tayari kufanya kazi za kilimo waweze kutengewa maeneo kule na ikiwezekana taarifa ziwafikie maana wako tayari kwenda mashambani popote, maporini kule, kwenda ku-establish mashamba ili kujipatia riziki zao. Hata hivyo, ukweli ni kwamba kwa sasa hivi mazingira ni kama vile wanabaniwa sana kiasi kwamba wanashindwa kupata mwelekeo kwamba ni namna gani wanaweza kupata maeneo kwa ajili ya kujiendeleza kwa kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tulikuwa kwenye Semina hapa ambayo Mheshimiwa Waziri wa Maliasili alituandalia. Wataalam wale maprofesa walikuja hapa walituambia kuwa nchi hii haina tatizo la ardhi. Hatuna matatizo ya ardhi ukilinganisha kilichopo na idadi ya watu na lilikuwa ni jambo la aibu sana, wamesema hapa tunachokikosa sisi ni mipango. Aliilinganisha Tanzania na akina Vietnam jinsi ambavyo wako kwenye eneo dogo, watu wengi na hawana migogoro hii ambayo kama sisi tuliyonayo na wale watu wanazalisha chakula mpaka sisi tunapewa huku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa jana tulikuwa na matatizo ya njaa, nchi yenye ardhi kubwa kama Tanzania halafu watu tunalialia na vibakuli vya kuombaomba chakula? Ifike wakati sasa Waheshimiwa muamue sasa kwamba, mnaipanga hii nchi ili Watanzania wengi ambao wana nguvu za kufanya kazi waweze kupata maeneo ya kufanya kazi za kilimo na mifugo, tena bila kugombana. Kuna nchi nyingi tu ambazo ni ndogo kwa size, zina watu wa kutosha, wengi lakini hawana migogoro kama tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba, Waheshimiwa Mawaziri, kama tulivyoomba katika bajeti iliyopita wakati ule Mheshimiwa Mwigulu akiwa kwenye kilimo yeye akiwapo hapo na Mheshimiwa Maghembe pale, kwamba washirikiane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mizengwe mingi sana katika nchi hii; yametengwa kwa ajili ya kilimo lakini maeneo hayo yana misitu, kuna miti lakini watu wananyimwa kukata miti, eneo la kulima utalimaje sasa kwenye miti, si lazima uikate? Likishakuwa declared kwamba ni eneo la maendelezo ya kilimo na mifugo basi Wizara ya Maliasili na Utalii isiende tena kupeleka pale wataalam wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale watu wana chokochoko nyingi sana, wako aggressive na wakati mwingine wanafanya biashara ambazo ni kichaa kule kwenye mashamba. Kwa hiyo, Waheshimiwa Mawaziri ningewaomba washirikiane. Maeneo ya kilimo kama kuna misitu, kama kuna miti huko na tayari wamesha-declare ni eneo la kilimo na ufugaji basi watu wa maliasili wasiwe wanaingia sana kule, hii mizozano hii inaleta fracas kwa wananchi wanashindwa kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningewaomba wakae pamoja ili wananchi waweze ku-explore na ku-enjoy matunda ambayo nchi hii inaweza ikawapa. Tuna ardhi kubwa, maeneo ni mengi, hakuna sababu ya sisi kugombana. Viongozi ama tuseme watu wanapokaa kwenye madawati yao wasiwe wanakaa pale wanakuwa kama obstacles, watu wamekaa tu! Mtu akishakaa anakuwa bwanyenye kazi yake ni kuzuia watu wengine wasi-develop, wanakosa nafasi ya kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kila mmoja kwenye nafasi yake awe ni chachu ya mtu mwingine kunufaika na chochote ambacho kinapatikana kwenye nchi hii na asikae pale anakuwa kama kizingiti kuzuia mtu. Kuna wivu sana wa kimaendeleo kwenye nchi hii. Kwa hiyo tusaidiane, vijana wapewe nafasi na vijana wako wengi na hawana kazi, tutengeneze ajira ili watu waweze kuzipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Waziri ni Shirika la Nyumba na Mheshimiwa Angela Kairuki hapa inaweza ikamhusu pia. Tunawapeleka Walimu, Madaktari, na Manesi vijijini; maeneo yetu mengine kwa kweli ni maeneo ambayo si mazuri kwa maisha ya binaadamu. Kule hakuna nyumba, hakuna maji. Kuna kata zangu nyingine kwa kweli ni za ajabu sana, hakuna barabara, hakuna umeme, hakuna maji, Kata za Bwawani, lakini bado kuna shule kule, kuna zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumwomba Mheshimiwa Waziri Shirika lako la Nyumba, ikiwezekana lifanye makubaliano, sisi Halmashauri ya Arusha DC tuko tayari kama ataruhusu tuingie mikataba, watujengee nyumba nzuri kwa ajili ya wafanyakazi kwenye maeneo yale, halafu sisi kwa kutumia vyanzo vyetu vya ndani tuweze kuwa- fund, kuwalipa kama ni kodi, kama ni kulipa instalment ya kununua zile nyumba, pengine baada ya miaka 10 kadhaa hivi tutakuwa tumeshazinunua na wafanyakazi wanakuwa wako comfortable kule vijijini. Maana sasa hivi huwezi kumchukua mtu ana degree yake nzima, nzuri safi tu, hajachakachua cheti wala nini halafu unampeleka kwenye nyumba za udongo, nyingine hazina madirisha, hakuna umeme, hakuna solar, hakuna kitu halafu unataka afundishe shule yetu ya kata iliyoko kule! Kwa hiyo, wanapata shida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri Serikali iangalie utaratibu badala ya kujenga majumba tu mijini huku ambako tayari watu binafsi wamewekeza na nyumba bado si tatizo sana, tukawekeze hizi nyumba kwenye maeneo ambayo yana challenges nyingi ili nyumba ziwe nzuri, wataalam angalau wawe comfortable kwenda kufanya kazi vijijini na huduma ziweze kutolewa ambazo zinaeleweka kwenye vijiji vyetu. Kwa hiyo, naomba hilo lizingatiwe pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliomba kwamba, miingiliano ile ya kwenye Wizara kidogo iwe controlled ili tuweze ku-enjoy matunda ambayo yako kwenye nchi hii. Kwa hiyo kwa leo niseme tu Mheshimiwa Waziri ningefurahi sana kama akinijibu yale maombi yangu ya Kata yangu ya Bwawani na wale ambao wanahitajika kufidiwa katika eneo ambalo jeshi limechukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana na ningefurahi siku moja nisimame hapa nimsifu kama alivyosifiwa na akina Mheshimiwa Mdee; mimi bado hajanigusa, kwa hiyo naomba na mimi aniguse ili nikija hapa Bunge lijalo na mimi nimsifie kidogo. Arumeru tuna shida sana, nikimpa nafasi Mheshimiwa Nassari hapa ataongea mpaka asubuhi, ni kwa sababu ya ongezeko kubwa la wananchi katika Mkoa wa Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tu watutanue, mapori yako mengi ambayo hayana hata mipango mingine hamna…

Yes! Tutanuliwe kule, kwamba yale maeneo ambayo yako wazi yanafaa kwa kilimo kwa sababu kiukweli hata sehemu za kuzikia siku hizi ni tatizo. Katika viunga vya Mji wa Arusha sasa hivi tunakwenda kuzikana Manispaa kwa sababu, ardhi imekuwa ni finyu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hayo tu machache kwa leo. Nakushukuru sana kwa kunipa fursa.