Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa kumpongeza Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu, Manaibu Makatibu Wakuu, pamoja na Uongozi mzima wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa hotuba yao nzuri ya mwaka wa fedha 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kwa leo nichangie eneo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Hili ni eneo muhimu sana na ni sawa na mishipa ya binadamu inavyopitisha damu. Mapato yanayotokana na kodi mbalimbali ndiyo ambayo yanaweza kupeleka maendeleo ya dhati ya nchi yetu. Naishauri Wizara kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania bado haijaweza kuinua wigo wa kukusanya mapato kwa sababu bado kuna maeneo mengi ambayo wenzetu wa TRA hawajaweka utaratibu wa kukusanya mapato, nako ni sekta isiyo rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko kuna mapato mengi sana, lakini TRA hawakusanyi kodi, mfano ni watoa huduma za ushauri (consultants), wafanyabiashara ndogo ndogo; jamii yote hii inatumia miundombinu kama barabara, hospitali na kadhalika ambazo zinajengwa kutokana na sekta rasmi. Nadhani umefika wakati sasa Wizara kupitia TRA waandae mazingira rafiki ya sekta isiyo rasmi iwe sehemu ya kuongeza chanzo cha mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ni muhimu katika kukusanya mapato na ambalo halijawekewa mkazo mkubwa ni kutumia EFDs machine. Mfano wa kutumia mashine za kielektroniki katika kukusanya mapato ya Serikali ni vyanzo muhimu sana. Bado Wizara kupitia TRA haijasimamia utaratibu wa kutumia mashine hizi kwa mantiki kwamba siyo taasisi zote pamoja na watu binafsi wenye kuendesha biashara kubwa na ndogo, wanaotumia mashine hizi. Hili linaisababishia Serikali upotevu wa mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri ahakikishe mashine hizi zinapatikana kwa wingi na kwa bei za chini ili kila mtu aweze kununua na kutumia. Mfano ni mahoteli mengi hata hapa Dodoma hawatumii stakabadhi za EFDs na sijaona kama wenzetu Mamlaka ya Mapato wakichukua jitihada za dhati za ukaguzi. Tulichukulie suala hili kwa umakini mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia nichangie juu ya bajeti za Wizara na taasisi zetu kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Utaona kwamba kiasi kilichopelekwa kwa ajili ya matumizi mengineyo na fedha za maendeleo, takriban utaona ni asilimia 50 au pungufu ndizo zilizopelekwa. Hii inatoa tafsiri kwamba bajeti yetu haitoi uhalisia wa makisio yetu. Nashauri sasa tuweke bajeti ambayo itaakisi uhalisia japokuwa asilimia 80 hii itasaidia kufikia malengo ya Serikali yetu, kuliko kuweko makisio makubwa ambayo ni nadra kuyafikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.