Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Kwanza nimshukuru Mungu kwa namna ya pekee ambavyo ametujalia mpaka tupo hapa na uhai tulionao.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, naomba niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Nsimbo kutoka Mkoa wa Katavi, kwa jinsi walivyoniamini. Nilivyowaeleza kwamba nitawatumikia, kazi tumekwishaianza, naomba waendelee kuniamini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, imesheheni mambo mazuri sana. Kwanza tukiangalia huduma za jamii na matatizo na kero ambazo zinazunguka jamii zote za Watanzania. Mimi namuunga mkono kwa hatua ambazo amechukua kuanza kushughulikia kero zetu, naamini Serikali anayoiongoza itafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba Mheshimiwa Rais atafanikiwa kwa sababu amelenga pia kuongeza mapato na kupunguza matumizi. Mtanzania yeyote mfanyabiashara huwa haitaji kupata hasara katika biashara anayoifanya. Siku zote ataangalia mauzo yaongezeke na apunguze gharama. Mheshimiwa Rais wetu ameliangalia hilo ili aweze kuboresha na kupeleka fedha nyingi kwenye miradi. Mimi namuunga mkono mapato yaongezeke na matumizi yapungue na sisi Wabunge tutaendelea kumshauri maeneo mengi ambayo yatakuwa na upotevu wa fedha ili ziweze kuongezeka na wananchi wetu waweze kufaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Nsimbo limezungukwa na kero nyingi sana. Kwanza, wananchi wangu zaidi ya 80% au 90% ni wakulima wa mazao ya biashara na mazao ya chakula. Ndiyo maana mkoa wetu ni moja ya mikoa inayotoa chakula kingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna matatizo ya ardhi kuchoka sana, maeneo mengi tumekuwa hatupati mazao ipasavyo. Pia kuna tatizo la pembejeo na tunamwomba Waziri wa Kilimo katika ile ziara yake ya Tabora afike mpaka Mkoa wa Katavi ili aweze kuliangalia suala hili. Tunajua Naibu Waziri alipita lakini ratiba yake ikuruhusu pia kukanyaga na Jimbo la Nsimbo. Wakulima wa tumbaku wanapata taabu sana, kodi ziko nyingi, makato mengi, mikopo unamlipia hata yule ambaye hakuhusu. Kwa hiyo, tunaomba awaangalie sana wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Nsimbo ni jipya, kuna kata zimeongezeka na mojawapo ni kata ambazo zilikuwa ni makazi ya wakimbizi lakini Serikali ya Awamu ya Nne ilitoa uraia na mwaka jana wamepiga kura, tumepata Madiwani. Hata hivyo, zile kata zina mahitaji mengi sana. Kwanza, bado ziko kwenye hadhi ya Mkuu wa Makazi, kwa hiyo sheria iliyopo pale ni ya Mkuu wa Makazi, utendaji wa Halmashauri pale ndani umekuwa hauendi ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Waziri wa TAMISEMI kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene, awasiliane na Waziri wa Mambo ya Ndani, kata au maeneo yaliyokuwa makazi ya wakimbizi ya Katumba, Mishamo na Bulyanhulu tuangalie jinsi gani hadhi za makazi ya wakimbizi zinafutwa yabakie kuwa maeneo huru ya raia. Wale raia ambao hawajapata uraia, nimkumbushe Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni aliahidi kwamba suala hili litashughulikiwa haraka ili waweze kupewa uraia.
Kwa hiyo, tunaomba sana ahadi ya Mheshimiwa Rais itekelezwe wale ambao bado wapate uraia na makazi hayo ya wakimbizi hadhi yake ya ukimbizi iondoke ibakie eneo huru.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu lina kata 12 tuna vituo vya afya viwili tu na zahanati ni chache mno, vijiji vingi havina zahanati. Kwa hiyo, taabu ya huduma kwa mama zangu ambao ndio mara nyingi wanahitaji huduma za afya, imekuwa ni shida. Vilevile Jimbo langu la Nsimbo, sekondari ya juu hakuna na sekondari za kawaida ziko chache mno na tuna kata mpya. Kwa hiyo, tunaomba Serikali katika bajeti hii iliangalie kwa jicho zuri kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakumbwa na shida ya miundombinu na Jimbo la pili baada ya Mheshimiwa Rais kufungua kampeni mwaka jana lilikuwa ni la Nsimbo baada ya Jimbo la Mpanda Vijijini. Nilimwomba barabara kutokea Kanoge – Mnyake - Msaginya na aliahidi itatengenezwa kwa fedha za ndani. Nami nitamwomba Waziri ndugu yangu Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa anisaidie liingie kwenye bajeti ya mwaka huu 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo mengi, tunashukuru Serikali ya Awamu ya Nne, alhamdulillah imetupa majimbo, Halmashauri na pia umeme. Nimshukuru Mheshimiwa Profesa Muhongo kwa umeme wa vijijini, kata nne zimepata umeme lakini pia tupate umeme kwenye kata zilizobakia. Vilevile Halmashauri yangu inahitaji Wakuu wa Idara, kati ya Wakuu wa Idara 19 waliopo ni nane tu wengine wanakaimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais, naomba tuangalie suala la viwanda ambalo lipo hata kwenye Mpango wa Miaka Mitano, tumesahau pia kuangalia viwanda vidogo vidogo. Kuna maeneo mengi ambayo tunahitaji viwanda vidogo vidogo, kama dada yangu Mheshimiwa Hasna alivyochangia jana kuhusu Kigoma kwa lile zao ambalo linatengeneza sabuni, basi tuangalie viwanda vidogo vidogo kulingana na maeneo yetu tulipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nichangie suala la bandari, kuna mpango wa Serikali wa kujenga bandari ya Bagamoyo lakini tujue faida na hasara zitakuwaje katika uchumi wa nchi yetu. Tukiweka mwekezaji maana yake mpaka arudishe gharama yake, tuangalie na bandari tuliyonayo tutakosa mapato kiasi gani? Tunaiomba Serikali iangalie suala hili kwa jicho la karibu zaidi.
Katika hotuba ya Mheshimiwa Rais alizungumzia Air Tanzania. Air Tanzania kwa muda mrefu imekuwa inaenda kwa ufadhili wa Serikali, ndege moja gharama kubwa za uendeshaji. Serikali imepanga kununua ndege nyingine mbili kwa katika Mpango wake wa Miaka Mitano. Tusiende kihasara, ni bora watumishi waliopo walipwe, waende wakaanze maisha mapya tubakize wafanyakazi wachache ili Air Tanzania ifanye kazi kibiashara na kwa faida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la kodi kwa wastaafu, mtu amefanya kazi miaka 30, miaka 20 analipia kodi, lakini anakuja kwenye mafao ya kustaafu pia napo anakatwa kodi na hata TRA ukiuliza formula sahihi hakuna mahali ambapo pamenyooka kuhusiana na kodi hii. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iwasamehe wastaafu kodi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Serikali, miundombinu kwenye jimbo langu ni shida na sasa hivi Mto Koga umejaa na kuna watu wamepoteza maisha. Kwa hiyo, tunaomba reli yetu kama ilivyoahidiwa treni ipite wakati wote, fedha za dharura zije, barabara ziweze kupitika, Mkoa wa Katavi tumekuwa kama tuko kisiwani. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali kwa kupitia Wizara mtuangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia ni kuwa ajira ni kitu muhimu kwa watu wote. Kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi tuliahidi kwamba Serikali italeta mikopo (revolving fund) ya jumla ya shilingi milioni 50. Kwa hiyo, tunaomba utaratibu uandaliwe haraka, mfuko huo uanzishwe tuupitishe ili watu wetu waweze kupata mikopo na kufanya kazi ambazo zitawasaidia katika kunyanyua uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ajira jimbo langu lina wachimbaji wadogo wa dhahabu lakini Serikali imewapeleka Kaparamsenga kwenye copper. Hiyo haina msaada na sasa hivi kuna mwombaji mpya Kijani Investment kwa eneo lililokuwa linamilikiwa na GBA.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iachie wachimbaji wadogo wadogo eneo hilo, ni kilometa kumi tu kutoka Mpanda Mjini. Bahati nzuri ndugu yangu, kaka yangu, Mheshimiwa Profesa Muhongo barua imekuja ofisini kwako ya Chama cha Wachimbaji wadogo wadogo, wakiliomba hilo eneo wapewe wao badala ya kampuni mpya ya Kijani Investment. Maana wao hawana uwezo wa kwenda kuchimba copper, mashapo hayo ya copper hawawezi, inahitaji uwekezaji mkubwa sana. Kwa hiyo, tunaomba waachiwe sehemu ambayo wataweza kupata fedha kidogo kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao, dhahabu ni rahisi kuliko copper.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niiombe Serikali, Halmashauri zetu zinapewa ceilling ya bajeti lakini Serikali huwa haiangalii mahitaji husika ya kila halmashari. Kwa hiyo, Serikali ifanye upembuzi mzuri ili hizi ceilling za bajeti inazotoa iangalie na uhalisia wa mahitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais, ahsante sana. (Makofi)