Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Rais wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais mama yetu, dada yetu mpendwa, Mama Samia Suluhu Hassan kuwa mwanamke wa kwanza Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianzie na suala la kutatua kero na changamoto za muungano. Naomba kuipongeza Serikali kwa hatua zake na Kamati na Tume zilizoundwa katika kutatua kero na changamoto hizi za Muungano mpaka hapa tulipofikia ambapo sasa Zanzibar iko huru kujiunga na taasisi zozote za Kimataifa, inaruhusiwa kukopa, Tume ya Haki za Binadamu imeanzishwa Zanzibar na mengi mengineyo. Ninachosisitiza tu harakati hizi ziendelee katika kuboresha maslahi ya Watanzania nje na ndani ya Zanzibar.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mazingira si suala la Muungano lakini mazingira na mabadiliko ya tabianchi ni suala la Kimataifa. Zanzibar imo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo naomba jitihada zile za kuisaidia Zanzibar katika kunusuru visiwa vile iendelee. Kwa sababu utafiti uliofanywa tayari maeneo 48 ya visiwa vya Unguja na Pemba yameathirika kimazingira. Baadhi ya visima vya maji matamu vinatoa chumvi, baadhi ya mashamba yanatoa chumvi na kuna mmomonyoko wa ardhi. Hivyo basi, naomba jitihada hizi ziendelee katika kuinusuru Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila ya mazingira hakuna nchi. Hivyo naomba Wizara hii ya Mazingira iongezewe fedha katika kuinusuru nchi yetu na hasa katika maeneo ya fukwe za bahari na visiwa tengefu. Katika maeneo hayo wavuvi wanatumia uvuvi haramu, wanaharibu matumbawe na kuathiri mazingira ya visiwa hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashangaa, humu ndani ya Bunge tumekuja kutete maslahi ya Watanzania wote, lakini bado kuna wenzetu wanang‟ang‟ania madaraka. Tayari Kisiwa Panza na kwingine maji yameanza kufukia visiwa hivyo watatawala nini hawa visiwa hivi vikishafukiwa na bahari? Mimi naomba Jamhuri ya Muungano iingize nguvu zake zaidi katika kunusuru visiwa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijielekeze katika suala la Muungano. Imesemwa hapa Muungano wetu umefifia na hauna hali ya kuridhisha na wakati wowote unaweza ukavunjika. Mimi naamini Muungano wetu kwa nguvu za viongozi wetu na Watanzania wote umeimarika zaidi na una nguvu zaidi na unajulikana Kimataifa zaidi kuliko hapo mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie katika suala la majeshi. Kwanza napenda kumpongeza Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania. Napenda kumpongeza Waziri wa Ulinzi kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kulinda uhuru na usalama wa wananchi wa visiwa vya Zanzibar katika chaguzi zote mbili. Uchaguzi wa Zanzibar umefanyika kihalali kwa kufuata Katiba na sheria zote za uchaguzi. Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein ndiye Rais wa Zanzibar mpaka mwaka 2020. Naomba Bunge lako lisitumike kama mahali pa kujadili masuala ya Zanzibar, masuala ya Zanzibar yako kwenye Baraza la Wawakilishi.Wamesusa, watu wamekula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasikia malalamiko mengi kwamba Tume imevunja uchaguzi. Napenda niwakumbushe katika mwaka 2008 chama kimoja cha upinzani hapa Tanzania kilifuta matokeo ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa Vijana kwa sababu tu hawakumtaka ambaye anapendeza kwenye chama chao na wakakaa hawana Mwenyekiti mpaka mwaka 2011, hao pia wanafuata demokrasia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea suala la ulinzi katika maeneo tengefu, naomba litumike Jeshi la Ulinzi la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania katika kulinda hayo maeneo tengefu ya visiwa ambavyo wavuvi haramu hutumia kujificha kufanya uharibifu wa mazingira na pia maficho ya wahalifu. Naomba jambo hili litiliwe maanani kwa sababu wao ndiyo chanzo cha uharibifu wa mazingira katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kupitia Bunge lako Tukufu viongozi wetu mahiri wataendeleza mshikamano, udugu, upendo uliojengeka kwa miaka mingi mpaka kufikia miaka 52 ya Muungano wetu kwa vitendo. Mimi sina shaka na hilo, Serikali iko tayari na sisi raia tuko tayari kutii sheria za nchi. Kwa wale ambao hawatii sheria za nchi basi sheria itachukua mkondo wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba nimalizie kwa kuwaombea nguvu zaidi viongozi wetu wote, Mawaziri wetu wote na sisi Wabunge, sote tutekeleze majukumu yetu tuliyotumwa na wananchi na si kuwa walafi wa kutafuta madaraka kwa njia za mgongo wa nyuma. Uchaguzi umeshafanyika, wananchi wanahitaji maendeleo, hawahitaji porojo za kisiasa au za mwanasiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.