Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maelezo ambayo Mheshimiwa Waziri ameyatoa katika hotuba yake, na katika vipaumbele ambavyo vimepangwa hivi vinne, nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza yeye pamoja na ofisi yake, lakini pia niipongeze Serikali kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wanaifanya kwa ajili ya kuhakikisha Watanzania wanapata maendeleo. Sambamba na haya, yapo maeneo ambayo ninapenda nitumie nafasi hii kumshauri Mheshimiwa Waziri na wadau wote ambao wanahusika katika kuendelea kutuletea shughuli za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapojadili viwanda huwezi kutenganisha na suala zima la kilimo. Moja ya vipaumbele vikubwa ambavyo tumeviweka kwenye mpango ni suala la uendelezaji wa viwanda vyetu. Kazi kubwa Mheshimiwa Rais wetu amekuwa anaifanya ya kuhakikisha tunafufua viwanda ambavyo vime-cease kufanya kazi, lakini pia kuhakikisha tunaleta wawekezaji wengine ambao wanafungua viwanda vipya, lakini bado zipo changamoto ambazo nilikuwa naziona; watu wa Wizara ambao wanatuwekea mipango hii lazima pia waangalie vipaumbele vyao waelekeze katika maeneo ambayo tayari tumeshaanza kuchukua hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika upande wa kilimo wa zao la korosho Ukanda wa Kusini, Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa sasa hivi shughuli kubwa ambayo inatuingizia kipato ni zao la korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji wengi wako kule, makampuni mengi yako kule, lakini pia hata kipato cha wananchi wetu kwa kipindi kama hiki kinakuwa ni kikubwa sana, lakini uwekezaji gani tumeufanya sisi kama Serikali ninafikiri ni jambo ambalo Wizara lazima sasa waaangalie na waelekeze nguvu zao na macho yao ili kuhakikisha zao hili linafanya vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kuishuru Serikali, mwaka jana kuja msimu huu wametusaidia kutua sulfur kwa ajili ya kuhakikisha tunafanya uzalishaji mkubwa. Hata hivyo bado ninaomba niishauri Wizara au nimshauri Mheshimiwa Dkt. Mpango waone umuhimu sasa wa kufungua kiwanda ambacho kitakwenda kuzalisha sulfur katika Mkoa wa Lindi. Sulfur hii itasaidia wakulima wengi wa maeneo yote ya mkoa na wale wote wanaotumia kulima zao hili waweze kupata huduma ya pembejeo kwa karibu na kwa gharama nafuu zaidi. Msimu huu tumepata bure, lakini bado tumekuwa na changamoto ya uchache wa sulfur tuliyopokea, lakini pia tumepata changamoto ya kuchelewa kwa sulfur ambayo kimsingi imeshusha kidogo uzalishaji wa zao hili kubwa la biashara ambalo sasa hivi angalau tunaweza kufanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe katika eneo hili la uwekezaji katika viwanda, moja ya vipaumbele vyetu hebu tuangalie namna ambavyo tunaweza tukatengeneza kiwanda cha sulfur na mipango hiyo tayari ilishakuwepo, muhimu ni kuanza utekelezaji. Kwa hiyo katika bajeti zetu na mipango yetu ninaomba hili wazo nililete ili tuweze kulipa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili katika kilimo ni suala zima la uanzishwaji pia wa viwanda vya magunia au vifungashio. Sasa hivi tunapata magunia kutoka nje, tunapata magunia kutoka maeneo ya mbali, hii imeleta shida sana pia kwa wakulima wetu katika msimu kama huu. Hii ni fursa nyingine ambayo Serikali ingeweza kutengeneza fedha kubwa sana kupitia utengenezaji wa kiwanda ambacho kitaenda kutoa magunia na kwa sababu mahitaji ni makubwa, basi ninaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha aone umuhimu sasa wa kuelekeza nguvu katika eneo hili la viwanda tuweze kupata kiwanda ambacho kitazalisha magunia na vifungashio vyote ambavyo vitawasaidia wakulima wetu wa zao hili la korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu katika kilimo, ninapenda pia kuzungumzia suala la kilimo cha mbaazi. Hili zao kwa muda mrefu tumekuja hapa Bungeni, tumelalamikia na kutoa maelekezo lakini bado majibu ya kutosheleza mpaka sasa hivi hatujapata. Leo hii ukienda katika Jimbo la Nachingwea kwa msimu mzima wakulima wamejitokeza, wamelima mbaazi nyingi sana ambao sasa hivi hazina soko na hazima kazi yoyote ya kufanya, lakini bado nasikitika kusema Wizara mpaka sasa hivi hawana kauli yoyote ambayo wameitoa juu ya zao hili la mbaazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri wetu wa Fedha, lakini pia Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Tizeba ni muhimu sasa atoke na atoe tamko rasmi la kusema nini hatma ya zao la mbaazi kwa wakulima wetu ambao tuliwahamasisha, wakajitokeza kuchukua muda wao, lakini pia wakaongeza mashamba yao na kulima zao ambalo mikataba imevunjwa, soko hakuna. Sasa hivi mbaaza kilo shilingi 150, shilingi 200, lakini nilitegemea Serikali itasema kwamba kama tumekosa wanunuzi ambao tulikuwa tunawategemea kutoka India nini mbadala wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama mwakilishi wa wananchi na kwa sababu wananchi wenyewe wanatusikiliza sasa tunafika wakati tunapata uvivu hata kuwahamasisha wananchi wetu waweze kuitikiwa wito wa kulima zao ambalo halina soko, lakini nilikuwa nataka nitoe ushauri ufuatao ili haya yote yaendane kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza watu wa Wizara ya Kilimo lazima watueleze idara zao zinazohusiana na utafiti zinafanya kazi gani, idara zao zinazohusika na suala la kutafuta masoko zinafanya kazi gani? Kama tulijua India watavunja mkataba wa kununua mbaazi kwa nini hawakutuambia? Na sheria au hatua gani zimechukuliwa pale mkataba unapovunjwa katikati? Ni harasa kiasi gani ambayo wakulima wetu wameipata kwa kuweka mazao yao ya mbaazi ghalani bila kununuliwa mpaka sasa hivi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba ushauri au kumtaka Mheshimiwa Waziri wa Kilimo aseme kwa msimu ujao tuna sababu ya kulima mbaazi? Kama tunakiwa tulime, tulime tani ngapi na tutazipeleka wapi? Vinginevyo hatutakwenda kuwashawishi tena wakulima wetu walime zao ambalo halina faida badala yake ni bora tukaelekeza nguvu kulima kitu ambacho kitaenda kuwasaidia wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka nilizungumzie ni eneo la zao la muhogo, Wachina wameshaingia mkataba wa kutaka muhogo kutoka nchi ya Tanzani. Moja maeneo ambayo tunalima mihogo kwa wingi na miogo bora ni pamoja na Mkoa wa Lindi hasa Wilaya ya Nachingwea. Ni vizuri sasa tunapojadili habari ya viwanda lazima tuseme tuna mkakati gani wa kweli kujenga kiwanda kitakachoshughulika na suala nzima la ununuzi wa mihogo na usindikaji wa mihogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi nikiangalia kablasha zote sijaona sehemu yoyote ambako tunaelekezwa au kuna maelekezo ambayo yataonesha nia thabiti ya Serikali katika kwenda kuwekeza ili wakulima wetu wapate sasa mazao mbadala badala ya kung’ang’ania kulima mbaazi ambazo tume-fail basi nizuri tukaelekeza nguvu katika mazao kama korosho pamoja na mihogo ambayo tunafikiri itatuletea tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie eneo ambalo linaenda sambamba na viwanda. Huwezi kujadili viwanda, huwezi kujadili uzalishaji wowote kama hatuwezi upatikanaji wa nishati ya uhakika. Bado Mkoa wa Lindi Wilaya ya Nachingwea na maeneo yote yanayozunguka kanda nzima tatizo la umeme limekuwa ni kiwazo kikubwa sana. Leo wananchi wetu hawatuelewi sisi wawakilishi wao, wananchi wetu hawaielewi Serikali inafanya nini ikiwa bado wananchi mpaka sasa hivi tunawahamasisha wafanye shughuli za kiuchumi lakini hawana umeme ambao zitawasaidia kufanya shughuli zao za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri kwa heshima na taadhima, tunatambua kazi inayofanyika na sisi tunathamini, lakini ni muhimu sasa tukalichukua hili kama jambo la dharura. Tumeaidiwa sana kwamba mitambo itafungwa mashine zitanunuliwa; gesi inatoka kwetu lakini bado Mikoa ya Lindi na Mtwara mpaka sasa hivi hali ni mbaya hali ya uchumi inadidimia kwa sababu hakuna umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, kama tatizo ni fedha tunaomba utupatie fedha au uwape watu wa Wizara fedha au uwape watu wa Wizara ya fedha waweze kwenda kurekebisha upatikanaji wa umeme ili wananchi waweze kuzalisha na waweze kufanya shughuli za kiuchumi. Sasa hivi hakuna shughuli inayofanyika ukienda katika maeneo yale, ndani ya dakika mbili umeme unakatika, imekuwa ni kero na ni imekuwa hadha kubwa sana kwa shughuli za maendeleo. Kila Mbunge atakae simama anayetoka kwenye maeneo hayo lazima atazunguza hoja ya umeme. Tunaomba sasa ifike wakati Mheshimiwa Waziri mipango tuayoipanga kikanda ni lazima sasa tuelekeze mambo muhimu ikiwemo hili eneo la nishati ambalo sisi tunafikiri kwetu ni jambo la msingi na ni jambo ambalo litatusaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kujadili viwanda, huwezi kujadili uchumi kama huna mawasiliano ya uhakika na yaliyo safi. Serikali imefanya kazi kubwa mimi natambua, kwa mwaka wa jana na mwaka wa juzi mpaka kufika sasa hivi ziko ahadi ambazo tayari zimeshaanza kutolewa na nina hakika zitatekelezwa. Hata hivyo naomba Mheshimiwa Waziri katika mipango uliyoipanga, ziko barabara za kimkakati na za kiuchumi ambazo huwezi kujadili maendeleo ya nchi hii ukaziacha barabara hizo bila kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunajadili namna ya kuunganisha barabara za Wilayani kwetu, barabara ya kutoka Nachingwea - Masasi, Nachingwea - Nanganga kwa muda mrefu tumehaidiwa kupata fedha lakini bado utekelezaji haujaanza. Kwa mara ya mwisho tayari tumeshaambiwa wakandarasi wamepatikana bado kupitisha tenda kwa ajili ya kwenda kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri jambo hili ni la msingi sana. Leo hii tunatoa tani kwa tani za korosho kutoka Nachingwea kupeleka Mtwara kupeleka Lindi, hakuna sehemu ambako tunazipitisha na zile korosho zikafika kwa usalama. Magari mengi yameacha kufanya kazi kwa sababu barabara ni mbovu. Ni fedha kiasi gani tunapoteza kwa sababu ya ubovu wa barabara? Tunaomba ahadi ya kutengenezewa kwa kiwango cha lami na bahati nzuri matamko ya viongozi wetu yameshatolewa, tunaomba utekelezaji uanze katika mwaka huu wa fedha kwa wale wakandarasi ambao wameshapewa hii kazi. Hapa muhimu ni kupata fedha kwa ajili ya kuanza kufanya kazi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka huu wa fedha tulichangiwa au tuliele…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)