Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha afya njema na kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu ili na mimi niweze kuchangia katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze kwa kumpongeza Waziri wa Mipango pamoja na Naibu wake, Katibu Mkuu pamoja na Manaibu wake, kwa kazi nzuri sana ambayo wanaifanya na pia ushirikiano ambao Kamati ya Bajeti wanaipatia. Napenda niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya Chama cha Mapinduzi iliahidi kujenga reli ya kati, sasa hivi tayari Mkandarasi wakujenga reli ya kati kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro yuko kazini na Mkandarasi wa kutoka Morogoro hadi Makutupora ameshapatikana, mkataba umesainiwa na kazi imeanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza tena Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi katika kuendeleza bandari zake. Nimeshiriki katika kuweka jiwe la msingi la upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na sasa hivi Mtwara inajengwa gati yenye urefu wa mita 300. Nina uhakika kabisa ndani ya miaka ya miwili bandari zote mbili upanuzi ukikamilika kwa kweli sekta yetu ya usafirishaji hasa kwa njia ya bahari itakuwa imeboreshwa sana na uchumi wetu utakua kwa sababu korosho zetu na bidhaa nyingine kutoka katika Mkoa wetu wa Mtwara kama saruji kutoka kiwanda cha Dangote itakuwa hakuna matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia niipongeze pia Serikali yangu kwa hatua ambayo imefikia katika miradi ya kielelezo ikiwemo mradi wa Liganga na Mchuchuma, ambapo vile vivutio ambavyo wawekezaji walikuwa wanavitaka tayari wamepewa na kazi inaanza. Ninachotaka kuomba kwa Serikali yangu kwamba chuma kutoka Liganga makubaliano kipitie Bandari ya Mtwara, ili kiweze kupitia bandari ya Mtwara hatuwezi kusafirisha chuma kwa kutumia magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe ile reli ya kutoka Mtwara kwenda Liganga na Mchuchuma na Bamba Bay iharakishwe. Kwa sababu upembuzi yakinifu umekamilika, maeneo ambayo yatapita hiyo reli wananchi tayari wameshafanyiwa tathmini ya mali zao. Kwa hiyo, naomba ule mchakato mwingine uendelee ili pale ambapo uzalishaji kule utakuwa tayari na njia za kusafirishia ziwe pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuipongeza Serikali yangu kwa kuweza kulifufua Shirika letu la Ndege, kwa kununua ndege ambazo wananchi wa Mtwara na hata wa Dodoma kwa sababu unaweza ukatoka Mtwara ukafika Dar es Salaam ukaunganisha kuja Dodoma, ukatoka Dodoma ukaenda Dar es Salaam ukafika Mtwara na ukaenda kupata lunch kule kwa watani zetu kule Songea. Kwa kweli naipongeza sana Serikali yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kuiomba Serikali sasa hivi kwa kweli bei ya korosho ni nzuri sana na kule kwetu sasa hivi kila mtu ni furaha. Kwa vile wanaojishirikisha katika kilimo cha korosho ni wengi, manufaa yanayopatikana kipindi cha ununuzi wa korosho yanaenda kwa wananchi walio wengi. Sasa niiombe Serikali yangu tufike mahali tuache kuzisafirisha korosho zikiwa ghafi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mpango wetu wa kupitia Mfuko wa Kuendeleza Zao la Korosho ambao ulipanga kujenga viwanda vitatu vya kubangua korosho, nimeona juzi wameanza kule Tunduru. Kwa hiyo, naomba na maeneo mengine ambayo walipanga wafanye ili tupate manufaa ya bei ya korosho iendane pamoja na ajira za viwandani kutoka katika viwanda vya korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza tena Serikali kwa kuanza mradi wa umeme wa Stigler’s Gorge, kama tunavyofahamu tunajenga reli ambayo itatumia umeme lakini tumeanza uchumi wa viwanda vyote hivyo vitahitaji umeme mkubwa, hivyo uanzishaji wa mradi wa Stiegler’s Gorge nadhani umekuja kwa wakati muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza tena kwa Serikali tunayo gesi nyingi inayozalishwa, tunaomba pia itumike pia katika kuboresha viwanda vyetu na pia katika kuhakikisha tunapata umeme wa kutosha. Katika Mkoa wetu wa Mtwara tumeahidiwa kujengewa megawati 300, tunaomba huo mradi uharakishwe kwa sababu sasa hivi Mtwara kuna changamoto kubwa sana ya umeme. Tumeahidiwa kuletewa megawati 20, lakini megawati 20 nina uhakika ndani ya miaka wiwili ijayo zitakuwa hazitoshi, kwa hiyo suluhisho la kudumu ni megawati 300. Kwa hiyo, tunaomba miradi hiyo yote iende sambamba kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu za Shirika la Kuhudumia Watoto (UNICEF) zinaonesha ifikapo mwaka 2050 tutakuwa na watoto chini ya umri wa miaka 18 wafikao milioni 58. Watanzania kwa ujumla watakuwa milioni 108.

Je, tumejiandaa kuweza kuwasomesha watoto hao, kuweza kuwalisha watoto hao na kuweza kuwatibu watoto hao? Kwa hiyo, naiomba Serikali iweke mikakati ya kuhakikisha kwamba ongezeko la watu linaenda sambamba na ukuaji wetu wa uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumalizia kuna watu wanasimama wanaulizia pesa katika maeneo yao, lakini baadhi yao ni walewale ambao waliikataa bajeti iliyopita. Swali langu kwao, hizo pesa wanazoziulizia kwenda katka maeneo yao ni zile walizozikataa au kuna bajeti nyingine waliipitisha huko? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama una watoto wanne…

T A A R I F A . . .

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani wapiga kura wake wamemsikia na ndicho alichokuwa anataka. Swali langu nililoliuliza hakulijibu. Nimeuliza bajeti ambayo wao wanataka iende katika maeneo yao, ni ile waliyoikataa au nyingine?

T A A R I F A . . .

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mtu amepewa kazi yake, kuna waliopewa kazi ya kukusanya pesa na sisi tumepewa kazi ya kuidhinisha pesa. Kama wewe hujaidhinisha hizo pesa, unategemea zinafika kwao kwa mitindo gani? Wao hawakuidhinisha pesa na kama Waswahili wanavyosema asiyetwanga na asile, wao wamezikataa pesa, tupeni sisi tulioidhinisha pesa hiyo ndiyo taarifa ninayompa. Hata hivyo, nafurahi sana ukizungumza halafu wanawake kwa waume wakasimama kukupa taarifa maana yake taarifa yako imefika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kupitisha bajeti unaweza ukakataa, unaweza ukakubali, unaweza ukasema huna maamuzi. Sasa kwa wao ambao walikikubali hiki wakakataa kile wangesema sina maamuzi, lakini wao wamekataa, ndio maana nikasema watafute maneno ya kwenda kuwaambia wapiga kura wao ni kwamba wao bajeti waliikataa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja na naomba Waziri wa Fedha miradi yangu ambayo nimeiomba kwenye Jimbo langu nipelekewe pesa kwa sababu niliunga mkono hoja.