Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye Mpango wa Maendeleo ulioko mbele yetu wa mwaka 2018/2019. Nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima nikaweza kusimama tena mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwenye mpango wa Waziri ameweka vipaumbele vichache. Nami naomba nijaribu kuangalia vile vipaumbele kwa namna ambavyo vinaweza kuboreshwa zaidi. Kwanza naanza na hii ya kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu na hasa nikianza na suala la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matarajio yetu Wabunge na ni matarajio ya Watanzania kwamba, angalau mpango wa bajeti ujao uweze kwenda kuondoa kilio cha maji cha muda mrefu, kwa sababu kilio kimekuwa ni cha kila mahali. Kila Mbunge ndani ya Bunge hili Tukufu ana kilio cha maji na kiukweli maji ni uhai, maji ni uzima. Tunapokwenda kugusa suala ambalo tunagusa uhai wa Watanzania tusitegemee tunaambiwa kwamba, tunasubiri kupata wafadhili au tunaomba wafadhili, tutenge fedha ya ndani kwenda kukamilisha miradi ya maji ambayo imeanzwa ili tuweze kupata maji ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mpango ujao nategemea kabisa miradi mikubwa ile ambayo ilikuwa kwenye bajeti inafanyiwa upembuzi yakinifu na mambo mengine inakwenda kuwekewa fedha ya kutekelezwa ikiwepo mradi wa maji kutoka Malagarasi Mkoani Tabora kupeleka Wilaya ya Kaliua na Wilaya ya Urambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwenye bajeti ijayo kuwepo na fedha ya kutosha kuhakikisha kwamba, mradi huu unakamilika kwa sababu, Serikali inajua kwamba, ndani ya Mkoa wa Tabora ardhi haina visima vya maji kwa hiyo, njia pekee ni Mradi huu wa Maji wa Malagarasi na Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kuweza kupeleka katika Mkoa wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la usimamizi wa rasilimali ya misitu. Katika kipindi ambacho misitu yetu inateketea ni kipindi hiki. Nilitegemea kabisa kwamba, baada ya kuanzishwa kwa Wakala wa Misitu angalau lengo la Wakala wa Misitu, ilikuwa ni kuhakikisha kwamba, misitu inalindwa, inahifadhiwa, lakini inatunzwa kwa njia ambayo ni endelevu na matumizi endelevu. Sasa hivi tofauti na hapo Maafisa wa Misitu kwa maeneo mbalimbali kazi wanayofanya ni kugonga mihuri kwenye magogo, kwenye mbao, magogo yanaondoka tunabakiwa na vichaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwenye mpango ujao namna gani Serikali itahakikisha kwamba, inaweka mpango endelevu wa kulinda na kutunza misitu yetu, tunaenda kuwa jangwa. Leo tunapata madhara mengi sana ndani ya nchi yetu kutokana na mabadiliko ya tabianchi, hatujui chanzo ni nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchomaji wa mkaa umezidi na bahati mbaya sana leo Serikali imeweka mabango sehemu maeneo mbalimbali kuhalalisha mauzo ya mazao ya misitu wakati uvunaji wa misitu na utunzaji, kupanda miti ni tofauti. Tunapanda kidogo sana, hatutunzi, haikui, tunavuna kwa speed ya 100 percent, tuendako tunaenda kuwa jangwa. Naiomba sana Serikali tuhakikishe tunaweka mpango endelevu wa kutunza na kuhifadhi misitu yetu kwa sababu hali ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia chanzo kikubwa cha uharibifu wa misitu ni ukataji wa mkaa na hatujawa na mpango mbadala wa matumizi ya nishati, tunasema kila siku. Nimeona kwenye Mpango wa Serikali kwamba, tunakwenda kuwekwa kiwanda cha makaa ya mawe ya Mchuchuma. Ni miaka 15 tunasikia makaa ya Mchuchuma – makaa ya Mchuchuma, kwa nini hautekelezwi, miaka 15?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine ingekuwa ni solution kuhakikisha kwamba, watu wanapata nishati ya kutumia kwa sababu, umeme huwezi kupikia, gesi wanatumia wachache, mafuta ya taa hayashikiki, ni kuni na mkaa. Asilimia 80 ya Watanzania wanatumia kuni na mkaa, hebu Serikali mwakani itujie na mpango namna gani Watanzania wanatumia nishati tofauti na mkaa, ili kulinda misitu yetu, tunakwenda kuwa jangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la umeme. Nashukuru kwamba, umeme wa REA umeanza kusambaa maeneo mbalimbali, lakini ule umeme sasa hivi umekuwa ni ‘kimulimuli’ kwa sababu, ikinyesha mvua umeme hamna kwa sababu, speed yake ni ndogo na nguvu yake ni ndogo. Tunaiomba Serikali kwenye mpango wa maendeleo ujao uje na mpango mkakati wa kujenga sub- stations maeneo mbalimbali kwa ajili ya kupokelea umeme na kusambazwa maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda Kaliua pamoja na kuwa walipata faraja wamepata umeme, lakini mvua ikinyesha unakatika, jua likiwa jingi unakatika kwa hiyo, hauna tija. Tunasema tunazungumzia uchumi wa viwanda, hatuwezi kuwa na uchumi wa viwanda kama umeme siyo wa uhakika. Kwa hiyo, naiomba Serikali ikiwepo kujenga kituo cha sub-station pale Kaliua pamoja na Urambo, mpango ambao umekuwepo tangu mwaka jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kwenye mpango ujao ukatekelezwe huu umeme wa REA ambao tunaendelea kuupata uweze kuwa na tija kuendesha viwanda vidogovidogo, lakini pia kuweza kusaidia wananchi kuweza kuutumia, usije ukawa ni kama mapambo, kama ambavyo sasa hivi unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la Vitambulisho vya Taifa. Mpango huu umeanza tangu mwaka 2019, mpaka leo ni miaka tisa speed yake ni taratibu sana. Tunajua umuhimu wa Vitambusho vya Taifa. Kwanza ni uraia wa Mtanzania, lakini pili tunaweza kutumia kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali. Leo ndani ya Taifa letu kuna watu wanaingia kinyemela kwenye mipaka wanaishi Tanzania kwa amani, kwa furaha, sio raia wa Tanzania. Hiyo ipo kabisa, ni nchi pekee ambayo unaweza kukuta kitu kama hiki. Kwa nini speed ya vitambulisho vya Taifa inaenda taratibu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitenga fedha nyingi sana zaidi ya milioni 200 kipindi kile, lakini mpaka leo speed ni taratibu sana. Bahati mbaya sana sasa hivi wananchi wanadaiwa fedha, ili uweze kuandikishwa utoe sh.5,000/=, sasa hivi mtu ananunua hata uraia wake kwa kweli, is nonsense.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali, kwanza suala la kuwalipisha wananchi kujaza fomu kwa ajili ya Vitambulisho vya Taifa liondoke, lakini pia mchakato huu ufike mwisho. Tuambiwe kabisa kwamba, idadi ya Watanzania wangapi mpaka leo wamepata vitambulisho vya Taifa, ni haki yao na siyo ombi. Tunaomba litekelezwe tuache kwenda speed ya taratibu kiasi hiki kwa suala la umuhimu kama kupata Vitambulisho vya Utaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la uanzishwaji wa Bandari ya Samaki. Tumekuwa tunaongea na kwenye mpango wa Waziri haipo. Tumekuwa tunasema njia tunayopoteza mapato mengi sana ni njia ya bahari kuu, uvuvi wa bahari kuu almost ni shamba la bibi, wanakuja wanavuna wanaondoka; hatujui wamevuna wangapi, mafuta wanajaza hukohuko, tumekuwa ni rasilimali ambayo hatuilishi iko pale ni kuiuza, kuisimamia na kupata fedha, tumeshindwa Serikali. Tunaiomba kwenye bajeti ijayo Serikali ije na Mpango wa Kujenga Bandari ya Samaki tuweze kuhakikisha bahari kuu samaki wale wananufaisha Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuache kuwa wazembe kiasi hiki. Ni miaka mingi, lakini kila mpango ukija haipo. Kwa hiyo, ni matarajio yangu kwamba, mwakani kwenye mpango huu unaokuja Waziri atatujia na mpango mkakati, mpango maalum kuhakikisha kwamba, tunakuwa na Bandari ya Samaki tuweze kuongeza Pato la Taifa, lakini pia tunufaike na rasilimali ambayo wenzetu wananufaika nayo wanakwenda kutajirika, sisi tunaendelea kuwa ni maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo. Ni kweli kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu, lakini kilimo chetu hakiendani na neno lenyewe uti wa mgongo. Kwanza kilimo cha Tanzania bado ni kilimo ambacho kinatumia jembe la mkono kwa kiasi kikubwa, lakini ni kilimo ambacho hata mazao yanayopatikana hayana masoko. Leo imekuwa ni kilio sasa mwananchi ananunua pembejeo mwenyewe, ananunua kila kitu mwenyewe, hata masoko ya mazao hakuna. Imekuwa ni maumivu makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ndani ya Mkoa wa Tabora particularly Wilaya ya Kaliua na maeneo mengine watu wanalia machozi, wamelima kwa jasho, wamevuna, leo tumbaku iko kwenye ma-godown haina soko, inaharibika, inashushwa thamani. Leo Serikali inasema habari ya kilimo, utasema nini kwa habari ya kilimo?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tuwe na mbinu na mikakati ya kuandaa masoko ya kilimo mapema kwa sababu, tunakwenda kwa takwimu ni lazima tujue tuna wakulima idadi gani, watazalisha kitu gani, tuwe tumejipanga kupata masoko ya uhakika kupitia kilimo cha mbaazi, kilimo cha mahindi, ni kilio kwa sababu tunahamasisha kilimo, lakini tuwe na mikakati ya masoko ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni lazima tuhakikishe kwamba, kilimo cha Watanzania kinakuwa ni kilimo ambacho kinatumia mechanization siyo kilimo cha jembe la mkono ambacho ni cha muda mrefu na pembejeo zipatikane kwa wakati ili watu walime kwa tija na waweze kunufaika na kilimo ambacho asilimia zaidi ya asilimia 75 kubwa ya Watanzania inategemea kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango ujao ni lazima kila zao la biashara tuwe tumeambiwa kwamba, masoko yako wapi ya uhakika. Sasa hivi naiomba Serikali sana tatizo la tumbaku ambalo liko sasa hivi Serikali ihakikishe namna yoyote kuhakikisha tumbaku ile inapata masoko, pia itafute madawa ipeleke kwa ajili ya kwenda kuitunza isiendelee kuharibika na ikiwezekana Serikali iinunue iitunze kwenye ma- godown yake wananchi wapewe fedha waendelee na maisha yao. Leo watoto wao hawaendi shule, leo wameshindwa hata kumudu vyakula, lakini tumbaku iko ndani na ni zao ambalo walihamasishwa walime.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana majibu anayotoa Waziri wa Kilimo yanasikitisha sana kwamba, watu walilima bila kuwa na makisio na anajua ni kwa nini watu walilima bila makisio. Sio majibu ya Waziri ya kutoa. Kwa hiyo, tunaomba aje na majibu mazuri, Serikali ije na majibu mazuri ni kwa nini tumbaku ya wakulima Tabora na mikoa mingine hainunuliwi wakati walihamasishwa kulima na wamelima kwa nguvu zao peke yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la utafiti. Huwezi kuwa na nchi ya maendeleo endelevu, ukawa na kilimo endelevu, ukawa na viwanda, ukawa na elimu nzuri bila kuwa na utafiti. Tumekuwa wazembe kama Taifa kuwekeza kwenye utafiti. Tunaomba bajeti ijayo tuhakikishe tunawekeza vizuri kwenye utafiti, vyuo vyetu vya utafiti nchi nzima viko hoi, miundombinu imeharibika, tunao wataalam wako pale wana elimu nzuri, hatuwatumii kwa sababu, hatuwekezi kwenye utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima kama Taifa tuwekeze kwenye utafiti tuweze kufanya kila kitu kwa kutumia utafiti, watu walime kwa utafiti, watu wauze kwa utafiti, watu wasome kwa kufanya utafiti. Suala la mwisho katika utafiti, vituo vyote vya utafiti vikarabatiwe pia, kuwepo na nyenzo na vitendeakazi elimu ambazo ziko pale na wataalam wale waweze kutumika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni suala la mikopo kwa elimu ya juu. Kiukweli kuna matatizo makubwa na wananchi wa Tanzania, wonyonge, maskini, wanalia sana. Nilifikiria kwamba, Serikali iliposema kwamba, kila mtoto anayekidhi vigezo atakwenda kupata mkopo, ni kweli ingekuwa hivyo, lakini leo wako wengi wamekidhi vigezo, lakini wamekosa mikopo. Unaposema unawapa watoto elfu 30 wakati umeacha elfu 37, majority wamerudi mitaani wanakwenda kufanya nini, hakuna mitaji ya biashara, wameshamaliza kusoma Form Six, kilimo hakilipi, wakilima biashara hamna, wakilima masoko hamna. Kiukweli hawa asilimia zaidi ya 30,000 ni wengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali ifanye utafiti wa kutosha kila mwaka ihakikishe kwamba, mwaka ujao wana-pass wanamaliza vyuo wanafunzi wangapi, form six na wataingia wangapi, ili ijipange kuendana na idadi ya watu ambao wanakidhi vigezo vya kuweza kupata mikopo. Vinginevyo itaendelea kuwa ni vurugu kwa sababu, kila mwaka watoto wetu wanaandamana, wanapigwa kwa sababu, ni haki yao wanadai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa kuwa watoto wanatamani kusoma na kitu pekee ambacho mzazi au Taifa unaweza kumpa mtoto wako ni elimu, vingine vyote ni bure, ukishindwa kumpa elimu ni basi. Kwa hiyo, pale ambapo watoto wetu wanamaliza shule wana matarajio ya kupewa elimu, basi Serikali ijipange vizuri iweze kutoa mikopo, ili kila mtoto mwenye kigezo cha kuweza kupata elimu apate elimu kwa ajili ya maisha yake ya hapo baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii.