Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Deogratias Francis Ngalawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia huu mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kutoa shukrani zangu kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli kwa mambo yafuatayo ambayo yanafanyika sasa hivi kule Ludewa. Kuna barabara ya lami kutoka Njombe kwenda Ludewa - Manda, umeme wa Gridi ya Taifa ambao unatoka Makambako kwenda Songea unakatisha pale Madaba unakuja Ludewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuna miundombinu wezeshi ambayo inaweza ikaifanya chuma Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma kuanza kwa maana ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara za Madaba kwenda Mkiu na barabara kutoka Nkomang’ombe kuelekea Liganga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo kuna baadhi ya mambo ambayo napenda kuyaelezea kidogo hasa kuhusu makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga. Chuma Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma ni miradi kielelezo katika Serikali hii ya Awamu ya Tano lakini bado hatujaona mpango ambao unaweza ukaonesha kwamba chuma Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma yanaanza lini. Kwa sababu hii project, project inatakiwa iwe na mwanzo pia iwe na mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali bado haijaweka ule utaratibu mzuri wa kusema kwamba katika kipindi hiki cha miaka mitano, mwaka huu tunafanya kitu hiki, mwaka wa pili hiki, mwaka wa tatu mpaka ule wa tano. Kwa hiyo, statement ambayo inakuja ni statement ya jumla sana kiasi ambacho sasa hata ku-access huu mpango ambao ni mradi kielelezo cha Taifa inakuwa ni mgumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa Serikali sasa ianishe kwamba kwamba kwa sababu huu leo ni mwaka wa pili unakwisha tunaelekea kwenye mwaka wa tatu, bado hatujaona zile activities ambazo zinatakiwa zifanyike katika huu mradi husika. Tukiweka na kuainisha maana yake tutakuwa tumeweka vizuri kiasi ambacho unaweza sasa kufanya tathmini kwamba mwaka huu tunafanya hiki, mwaka wa pili tunafanya hiki na hata kama tunakwama sehemu tunakuwa tunajua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye hilo ningependa tu Serikali ije na ile mipango kwa sababu kuna eneo pale ambalo wananchi wetu wamepisha mpaka leo bado hawajalipwa fidia na wala hatujui fidia ile italipwa lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna huu mpango ambao tumesema kuna Power Purchase Agreement, ni kweli tunapata maelezo lakini hatujui kwamba sasa hiyo Power Purchase Agreement itakamilika lini kiasi ambacho sasa itapelekea ile Government Notice kutoka. Naamini kwamba hii yote ipo ndani ya uwezo wa Serikali, Serikali ikijipanga haya mambo yanaweza yakaisha na mwisho wa siku hata hawa watu ambao wamepisha ile miradi kwa sababu yale maeneo waliyoyapisha ni makubwa kiasi ambacho sasa wanashindwa kufanya kitu chochote na hawajui kwamba fidia yao watalipwa lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulichangia ni juu ya suala la zao la mahindi. Nyanda za Juu Kusini ambako Ludewa ipo, zao la mahindi ni zao la biashara. Kwa wengine wanaweza wakasema kwamba ni zao la chakula, lakini hakuna zao kubwa na muhimu ambalo linatiliwa nguvu kubwa na wananchi wetu kama zao la mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba tunapolima mahindi yanapotosheleza kwa chakula, mengine yanayosalia ndiyo ambayo yanaenda kwenye biashara ambazo zinawafanya watu wetu walipe ada, wajenge nyumba na wafanye maendeleo yao mengine. Kipindi cha sasa wananchi wetu wame-stuck na walikuwa wanaitegemea Serikali kwa kiasi kikubwa kununua yale mahindi, sasa hivi mahindi hayanunuliwi na mwisho wa siku sasa inabaki kwamba uchumi wa wananchi mmoja mmoja na uchumi wa maeneo husika unabaki ku-stuck.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa Serikali ije na mpango wa kuhakikisha kwamba mahindi yale ambayo wakulima tuliwahamasisha walime kwa kiasi kikubwa basi yanunuliwe sasa. Hali ni ngumu kwa wananchi wetu kule na tunaulizwa maswali mengi sana na bahati mbaya zaidi sasa hivi Serikali imezuia kuuza haya mahindi kwenye maeneo mengine. Tunaweza tukasema hivyo kwa sababu kuzuia kwake hatujapewa sasa altelnative kama lipo soko la ndani basi soko hilo lipo wapi ili mwisho wa siku hawa watu wetu waweze kuuza mahindi yao ili tupate faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni juu ya suala la maji. Maeneo ya kusini kuna ufadhili mkubwa sana ambao wananchi au Serikali inapata kutoka kwa donor funded. Kwa hiyo, katika ufadhili huo kuna sehemu ambayo Serikali inatakiwa ichangie, tunajikuta sasa kuna miradi mingi, kuna proposal nyingi tunaziandika lakini inapofika sasa kuchangia Serikali tunakwama sana na wale wafadhili wanatupa support ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sasa Serikali pindi tunapokuwa tunaleta kwenye meza zenu kwa wataalam na kwenye mamlaka husika, basi tupewe ushirikiano wa kutosha ili tuweze kutatua hili tatizo la maji kwa sababu hawa wadau wana-support kwa kiasi kikubwa ili mwisho wa siku matatizo na kero za maji ziweze kwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia uchumi wa viwanda maana yake ni lazima twende kwenye mapinduzi makubwa ya kilimo. Sasa kitendo cha kutokununua mazao ya wakulima au kutokutafuta masoko, uwezekano ni mkubwa sana wa kuona kwamba hatutaweza kufanikiwa kwa kiasi kile ambacho tumekilenga. Hii ni kwa sababu wananchi wanakosa matumaini, wanakata tamaa na mwisho wa siku sasa drop inakuwa kubwa katika kuhakikisha kwamba hawa watu wanaendelea ku-concentrate na ile motivation inakuwa hamna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani sasa Serikali ije na mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba tunatengeneza utaratibu mzuri (platform) ya kuhakikisha kila ambacho kinazalishwa kinakuwa kipo motivated ili mwisho wa siku tuweze kuendelea na kuhamasisha hawa watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara kandokando ya Ziwa Nyasa; kule wananchi wamejitolea kwa kiasi kikubwa kulima kwa majembe ya mkono. Kwa hiyo, pindi mara nyingi tunapoomba msaada kwamba hawa watu wasaidiwe kutokana na kero ambayo inawakuta mpaka imefikia kipindi wao wenyewe wanaamua kuchukua uamuzi tuwasaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru TASAF; tumelima barabara ya kilometa 28 lakini tunashukuru TASAF kwa kuweza kutu-support na matokeo yake sasa tunatumia zana ambazo ni mashine kwa maana ya grader na excavators ili kuhakikisha kwamba tunazipanua hizi. Vilevile katika maeneo mengine ambako wananchi wanajitolea zaidi, tunaomba mkono wa Serikali ufike kwa sababu kero hiyo ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Ludewa kuna Vijiji 15 ambavyo havijawahi kuona gari toka kuumbwa kwa ulimwengu. Sasa imefikia wananchi wameamua sasa kushika majembe na sululu ili waweze kupata hizo barabara. Kwa hiyo, naiomba Serikali kwenye maeneo kama hayo tunapokuja kuomba msaada kwa sababu ile ni kazi ya Serikali na wananchi basi tushirikiane na wananchi hawa kuwatia moyo kuhakikisha kwamba haya malengo yanakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo nalizungumza ni lile eneo ambalo ni kando kando ya Ziwa Nyasa ambalo ni mpakani mwa Malawi na Tanzania, ni eneo muhimu kiulinzi na kiusalama. Kwa hiyo, wananchi wanapochukua hatua hizo tunaamini kwamba Serikali ije nayo ituunge mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuishukuru Serikali lile eneo la mwambao wa Ziwa Nyasa ambalo ni eneo kubwa kuliko eneo lingine lolote, tulikuwa hatuna mtandao wa mawasiliano ya simu; tunaishukuru Serikali sasa hivi angalau asilimia 75 ya eneo hilo sasa kuna mtandao wa simu. Nipongeze na niweze kuishukuru kwa hayo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono mapendekezo. Ahsante.