Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nichukue nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya mimi kutoa mapendekezo yangu katika mpango wa maendeleo ya Taifa 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika karne ya 17 hadi 18, Nchi ya Uingereza ilifanya mapinduzi makubwa katika kilimo. Mapinduzi haya baadaye katika karne ya 18 kwenda ya 19 ndiyo yaliyosababisha mapinduzi ya viwanda yaani Industrial revolution. Sasa maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba, kama tunataka kwenda kwenye uchumi wa kati, uchumi wa viwanda, nashawishika kusema kwamba ni lazima tujitahidi tuwe na viwanda ambavyo vinatokana na malighafi za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakapojikita kuzungumzia viwanda hivi vya uwekezaji wa kutoka nje ambavyo havitakuwa na malighafi kutoka ndani ya nchi, bado tutakuwa hatujasaidia nchi hasa katika suala zima la ajira. Kama tutawekeza kiasi cha kutosha katika kilimo, tija itaongezeka katika uzalishaji, malighafi itapatikana na mwisho wa siku tutapata hivyo viwanda ambavyo tunavikusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuwa na kilimo kinachotupeleka huko kama tutakuwa tunaendelea kusubiri kudra ya Mwenyezi Mungu ya mvua. Ni lazima tuwe na mipango madhubuti ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na mabwawa ya umwagiliaji. Hatuwezi tukaendesha kilimo chochote ambacho ni sustainable kinachoeleweka ambacho viwanda vitakuwa vinasubiri malighafi kama mvua zenyewe ni hizi ambazo lazima kwanza tusubiri miezi kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nishauri kwamba katika mpango nimesoma, sikuona mahali popote panapoonesha kuhusu kuyatumia Mabonde haya nane ambayo tunayo katika nchi yetu. Kwa hiyo niombe sana kwamba kuwe na mpango madhubuti wa kuhakikisha kwamba mabonde yale makubwa; Bonde la Mto Rufiji, Malagarasi, Mabonde ya Mto Ruvuma, Mabonde ya Mto Pangani na Mabonde mengine yote yanatumika vizuri kwa ajili ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili likifanyiwa vizuri ndilo litakalosaidia pia na vijana wengi kupata ajira kwa kujiajiri katika kilimo. Tutakapowezesha vijana kujiajiri katika kilimo maana yake tutapata malighafi ya mazao mbalimbali, hilo nalo litakuja kuchochea kwenye lile suala la viwanda kwa sababu mazao mengine yatahitaji kuchakatwa ili yaweze kudumu kwa muda mrefu, mazao mengine yatahitaji kufungashwa katika vifungashio vilivyo bora ili kuweza kupata masoko yenye tija na hapo moja kwa moja tunaongeza mnyororo wa thamani na kuongeza tija katika mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumze suala ambalo limeandikwa katika mapendekezo ya mpango ambalo ni suala la uvuvi. Katika ukurasa wa 29, uvuvi wanakusudia kuzalisha na kusambaza kwa wakulima vifanga 421,368 na katika maeneo ambayo wameyataja kujenga mabwawa hayo ya samaki 159; Mikoa ya Geita, mabwawa 23; Mkoa wa Ruvuma, mabwawa 51; Mkoa wa Mara, mabwawa 14; Mkoa wa Pwani, mabwawa 52; Mkoa wa Tanga, mabwawa mawili; Mkoa wa Dodoma, mabwawa matatu; Mkoa wa Morogoro, mabwawa matatu; Mkoa wa Tabora, mabwawa saba; Mkoa wa Dar es Salaam, mabwawa mawili na Mkoa wa Kigoma, bwawa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina wasiwasi kwamba wametumia vigezo gani lakini nataka nitoe concern yangu hapa. Mimi natoka Mkoa wa Tanga katika Wilaya ya Lushoto, sisi katika Wilaya ya Lushoto, Wilaya ya Korogwe, Wilaya ya Muheza, Handeni na Kilindi, Wilaya zote hizi hakuna mto ambao unaweza ukawafanya watu wakapata samaki. Kwa hiyo, kwa kiasi kikubwa tulitaraji kwamba na sisi angalau haya mabwawa yangekuja kwa wingi angalau kufika hata 10 na lakini mabwawa mawili kwa mkoa mzima sijui hata utalipeleka upande gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda hapa niliseme wazi; Mheshimiwa Naibu Waziri mwenye dhamana ya Mifugo na Uvuvi amesema hii ni blue economy sasa tunataka tuone unapokwenda kulitekeleza hili. Kule Lushoto kuna upungufu mkubwa wa madini chuma ambayo madini haya yanapatikana kwenye bidhaa za samaki na ndiyo maana sisi kule ukivunjika mguu, ili mguu huo uungwe unaweza ukachukua hata miezi miwili tofauti na watu walioko katika Mikoa ya Pwani ambako wanapata samaki kwa wingi, miguu inaunga haraka kwa sababu madini ya chuma yanapatikana katika samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili tunaona kwamba, upande mmoja Serikali ikilifanya vizuri inakuja kutibu tatizo ambalo linaweza likatokea siku za mbeleni. Kwa hiyo niombe sana kwenye mpango hili la mabwawa kwa Mkoa wa Tanga yaongezwe ili tupate mabwawa ya kutosha zaidi. Kama nilivyosema ni Wilaya tatu pekee, Kilindi, Tanga Mjini na Pangani ndiyo ambazo ziko pembezoni mwa bahari hizi Wilaya nyingine zote zilizobaki ziko mbali na bahari kwa hiyo tunahitaji na sisi mabwawa kwa ajili ya ufugaji wa samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la miundombinu. Miundombinu ya barabara ni suala muhimu sana ili kuwezesha mazao kuweza ku-flow kutoka vijijini na kwenda kwenye masoko au kwenda kwenye viwanda. Hata hivyo, nataka nitoe sikitiko langu kwamba, katika mvua za masika za mwaka huu tulipata tatizo kubwa la maporomoko katika Wilaya ya Lushoto. Barabara ilijifunga kiasi cha wiki moja kwamba hakukuwa na mawasiliano katika ya Lushoto na maeneo mengine ya nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma katika mpango sikuona hili suala mahali popote ambapo limegusiwa kwa sababu tulishazungumza kwamba tunahitaji ile barabara iboreshwe, iongezwe upana pia tupate barabara mbadala ya kuweza kuunganisha Lushoto na maeneo mengine. Hii inawezekana tu kama ile barabara ambayo tunaiomba kutoka Korogwe kwenda Mashewa kwenda mpaka Bumbuli itafanikiwa na barabara hii iko katika Ilani ya Chama lakini mpaka sasa bado hatujaiona katika mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika Wilaya ya Lushoto inaweza ikaunganishwa na Wilaya ya Mkinga kwenda mpaka Tanga. Kwa hiyo hili nalo ni muhimu kwamba liingizwe katika mipango ya baadaye ya Serikali, tuunganishe Wilaya ya Tanga Mjini, kuungana na Mkinga, Mkinga iunganishwe na Lushoto lakini wakati huo huo Wilaya ya Lushoto iunganishwe na Same kwa maana ya Mkoa wa Kilimanjaro ili kuweza kuunganisha mikoa hii kwa pamoja na kuweza kufikia yale malengo ambayo tutayakusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nitoe rai sana kwamba kwa upande wa barabara kwa Wilaya ya Lushoto bado tunauhitaji wa barabara ya kutoka Lushoto kwenda Mlalo kwa kiwango cha lami. Kwa sasa hivi barabara hii inajengwa kilometa mbili mbili kila mkoa kiasi kwamba itachukua miaka mingi, kilometa 42 ina maana itachukua zaidi ya miaka 21.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sasa kwamba barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi hii kwa sababu sisi ni wazalishaji wa mboga mboga na matunda na ni mazao haya ambayo ni rahisi sana kuoza, tunahitaji tupate barabara madhubuti sisi viazi hatulimi vya vuli. Tunalima viazi kwenye vitivo, tunalima viazi ambavyo vinapatikana mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo viazi, carrot, spices zote ambazo unaziona zimejaa katika super market na masoko makubwa nyingi sna zinatoka katika Wilaya ya Lushoto, lakini tatizo kubwa ni barabara. Barabara inatia watu umaskini kwa sababu kama barabara itakuwa siyo madhubuti ndani ya siku moja tayari mtu anaweza akapata hasara kubwa kulingana na aina ya mazao ambayo tunalima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la usambazaji umeme vijijini. Nimezungumza na watu wa REA wametuhakikishia kwamba wao wako vizuri, wamejipanga na Makandarasi wa kutosha wapo, tatizo kubwa ni Serikali haiachii pesa. Disbursement ya pesa bado siyo nzuri na hapa tunazungumza kwamba ikifika mwaka 2020/2021 mradi wa REA utakuwa umefika mwisho, tujione sasa kutoka sasa ni miaka mingapi imebaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitoe rai kwamba Serikali iachie Mafungu, Mheshimiwa Mpango tafadhali sana aachie mafungu ili tuweze kukamilisha hii program ya umeme vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni program muhimu sana kwa hili suala zima la kuleta mapinduzi ya viwanda kwa sababu tutakapokuwa na viwanda vidogo vidogo hata haya mazao ambayo tunasema kwamba ni rahisi kuoza, yataweza kuchakatwa na kuongezewa ubora yaweze kudumu kwa muda mrefu zaidi. Kwa hiyo suala la watu wa REA kuwezeshwa ili waweze kwenda na kasi ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa nizungumzie katika mpango ni suala zima la usafiri wa anga. Hapa inazungumzwa kwamba katika ile mikoa kumi na moja na sisi Mkoa wa Tanga upo. Niombe sana kwa Wizara husika ya Uchukuzi kwamba tunaomba sasa na sisi tuanze kuingizwa katika ratiba ya kupata ndege hizi za ATCL.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika letu hili tumeona mapinduzi makubwa yamefanyika, sasa ni rahisi kwenda Mikoa ta Ruvuma, kwenda Mkoa wa Dodoma, Tabora, Kigoma, Bukoba na kule Songwe, lakini bado tunataka tupate connection kati ya Dar es Salaam, Zanzibar, Tanga mpaka Mombasa. Hii ni muhimu sana na itasaidia sana kwamba kwa kuwa sisi tuko mpakani na nchi jirani ya Kenya, uwepo wa kiwanja cha ndege ambacho kinafanya kazi na ndege kutua itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tuna mradi mkubwa wa bomba la mafuta, sasa tunataraji kwamba kwa namna yoyote ile Makampuni mbalimbali ambayo yamewekeza katika ujenzi wa hili bomba watahitaji kusafiri. Sasa tusingetaraji kwamba waanze kupoteza muda mrefu wa kusafiri na mabasi kutoka Dar es Salaam kuja Tanga. Kwa hiyo, hili nawaomba sana mliingize katika taratibu zenu na sisi tuweze kufaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la ufugaji hasa huu wa ng’ombe kwamba bado kama Taifa hatujasimama mahali sahihi kuwahudumia wafugaji. Wafugaji kama bado wanaonekana kama ni wageni katika hili Taifa. Sera zetu ziko wazi lakini bado naona Wizara inapata kigugumizi pamoja na Serikali kutoa miongozo mahususi hasa kuanzia katika ngazi za Halmashauri kuainisha maeneo mahususi kwa ajili ya kulisha mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kila mtu ambapo anaenda kutafuta eneo anaonyeshwa eneo lililo wazi lakini unakuta hakuna eneo ambalo liko wazi. Maeneo haya ambayo yako wazi ndiyo maeneo ambayo wafugaji wanayatumia lakini kama leo mtu anakwenda TIC kuomba eneo la uwekezaji anaelekezwa kwenye Halmashauri fulani, matokeo yake ni kwamba anapewa maeneo ambayo kimsingi ni maeneo ambayo yalikuwa yanatumiwa na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba sasa kuwe na utaratibu mzuri wa kuweza kuwa-accommodate hawa wafugaji wetu ili tuweze kuona na wao wanatoa mchango gani kwa Taifa hili. Mimi katika Halmashauri yangu nina Kata tatu ambazo zina wafugaji. Naweza nikatoa ushahidi namna gani ambavyo wafugaji hawa wamsaidia katika pato la Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, kwanza ni wepesi sana kushiriki katika shughuli za maendeleo, lakini namna bora ya kuwawezesha ni kuwajengea malambo, kuwajengea sehemu za majosho na kuwatengea maeneo mapana ambayo hasa wakati wa kiangazi wanaweza wakapata eneo zuri la kulisha mifugo yao. Sasa pale Serikali inaweza tu ikawa na wajibu mdogo wa kwenda kukusanya mapato na ushuru katika watu hawa. Lakini ni suala muhimu sana tunapozungumza uboreshaji wa Kiwanda cha Gereza la Kalanga kule Moshi sasa kama hakuna ngozi sijui kama watafanya kazi ya namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado pia tunahitaji kuwa na Taifa ambalo watu wanakunywa maziwa, bado Watanzania wanaokunywa maziwa ni wachache sana tena wengi wanakunywa baada ya kushauriwa na daktari. Isifike hatua kwamba hili ni Taifa ambalo watu wanakunywa maziwa baada ya kushauriwa na daktari, liwe ni Taifa ambalo lina tamaduni hizo za kuongeza vitu vyenye vitamini katika miili yao na kuweza pia kuondoa maradhi mbalimbali ambayo yatatupunguzia hata gharama za matibabu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana naomba hili alichukue kwa umakini mkubwa ili tuweze kuwasaidia wafugaji wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.