Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia mimi pamoja na Wabunge wenzangu kuonana mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili nikushukuru wewe kwa kunipa fursa hii ya kuchangia kutoa mawazo yangu kwenye Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2018/19. Tumeletewa mapendekezo nakumbuka Waziri Mpango ametusisitiza sanasana tumpe maoni yetu na mimi kama Mbunge tena Mbunge wa Dar es Salaama tena Kinondoni kwa wajanja, nimefurahi sana kupata nafasi hii na nitayazungumza na nayaangalia kwa kina sana mambo matatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo napenda tuliangalie kwa kina ni umaskini ambao naamini mapendekezo yetu au mapendekezo yangu nitakayoyatoa yanalenga namna gani tutapunguza umaskini kwa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, mimi kama Mbunge wa mjini napata nalo tabu sana ni ukosefu wa ajira, kwa hiyo nitaeleza namna gani Serikali ikifanya tunaweza tukapunguza au kuondoa tatizo la ajira. Jambo la tatu ambalo ni lengo kuu la msingi ni kuinua au kukuza uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia kitabu hiki cha Mheshimiwa Mpango, nampongeza ni mtaalam mzuri, lakini baada ya kukisoma sana tumeona mpango wetu maendeleo wa mwaka 2017/2018, tumetekeleza kwa asilimia 50 katika bajeti yetu ya maendeleo. Kwangu mimi naliona hili kama ni dosari kubwa, hivi ikiwa tunatengeneza mpango halafu tunakwenda kwenye utekelezaji, tunatekeleza kwa asilimia 50 tafsiri yake ni nini? Je, ingekuwa wataalam wengine mfano wataalam wa ujenzi Mainjinia nao wakatengeneza mpango wao halafu wakatekelezeka kwa asilimia 50 jengo litakuwepo, barabara itakuwepo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namweleza Mheshimiwa Mpango kama kuna mahali tunatakiwa tujirekebishe katika mapendekezo yangu mapendekezo haya tunayotoa mpango atakaotuletea 2018/2019 ahakikishe hatuwezi kutekeleza chini ya asilimia 80. Kupanga mpango ambao akautekeleza kwa asilimia 50 maana yake ametekeleza chini ya kiwango na kama mpango ni lengo kuleta maendeleo tusitegemee maendeleo kama yatakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ukuaji wetu wa uchumi ukiangalia hapa kuna chati ukurasa wa saba wa mapendekezo ya mpango inaonesha tulivyokuwa tuna grow chati inaonekana kuna kipindi tulifika mpaka 9.1; tukashuka, tukapanda mpaka 8.8 mwaka 2014; 2016 tulienda mpaka
7.7, 2017, tumeshuka; 2018 tumekwenda mpaka 7.0; mwaka 2017/2018 sasa hivi tunapanga kwenda 7.1.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutakuwa tunakuwa au tunaongeza ukuaji wa uchumi kwa 7.1 kutoka 7.0 maana yake Mheshimiwa Mpango anatukatisha tamaa kwamba hatuendi. Sasa mapendekezo yangu ni kwamba, lazima tujitahidi tuonekane curve inapanda twende angalau basi turudi pale tulipotoka 2016 tuje angalau 7.7 ili ionekane uchumi wetu unakua, kinyume chake atakuwa amekubaliana na matokeo kwamba sasa tunaanza kwenda chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia umaskini kwetu sisi Dar es Salaam, tunazungumza ukosefu wa ajira kwa vijana, vijana wengi hawana ajira. Serikali ukizungumza mpango hapa wanakwambia kuna vijana 1,000 wako VETA; kuna vijana 2,000 wako wapi; kuna vijana 3,000 wako wapi! Hivi kwa idadi ya vijana tuliyokuwa nayo Tanzania na kwa takwimu tunazopewa za vijana 2,000, 3,000 au 4,000 tutaondoa ukosefu wa ajira kwa vijana wetu lini? Hivi kama tunashindwa Dar es Salaam kwenye idadi ya watu milioni sita tunakuwa na Chuo cha VETA kimoja, idadi ya watu milioni sita, Dar es Salaam una chuo cha VETA kimoja, huu ukosefu wa ajira tunauondoaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, natamani sana Mheshimiwa Waziri akija, atuoneshe namna gani tatizo la ajira tutalipunguza kwa vijana wetu wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tu taarifa, ukitembelea Manispaa za mjini leo, Ilala, Kinondoni, Temeke, watendaji wetu (wataalam wetu wa biashara) wamefungua file la kufunga biashara…

T A A R I F A . . .

MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimu sana mtoa taarifa, dada yangu lakini taarifa yake inanipa tabu kwamba tuna programu nyingi za mafunzo ambazo hazitegemei VETA, tunategemea hawa vijana wanapelekwa kwa Profesa Maji Marefu? Si lazima hawa vijana wapate stadi? Namwambia Dar es Salaam tuna VETA moja, labda ningepewa taarifa kwamba ziko nane. Sasa hivi tuna Manispaa tano, VETA ziko tano, ningeichukua taarifa hiyo, lakini ananipa taarifa kwamba sehemu nyingine tusitegemee ufundi stadi peke yake, sasa tutegemee uganga? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mategemeo yangu ni kwamba ajira za vijana wetu zitatokana na weledi na ufundi watakaopewa na Serikali yetu sio kwa ujanja ujanja. Nakushukuru sana.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo la umaskini, katika jimbo langu pamoja na kwamba tuko mjini lakini wananchi wetu ni maskini sana. Umaskini huu unasababishwa wakati mwingine, Serikali haituangalii vizuri. Tuna pesa zimetengenezwa kwa ajili ya kuboresha Mji wa Dar es Salaam, tumeweka mabasi yaendayo kasi lakini tunashindwa kutenga fedha kwa ajili ya kugharamia mifereji midogo midogo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mto Msimbazi na wewe unaguswa moja kwa moja, juzi imenyesha mvua ndogo tu watu wana hali mbaya, maji yanaingia majumbani, wananchi wanapata hasara, vifaa vyao vinaharibika. Tuna Mto Kibangu na Dar es Salaam imeshakwisha labda mngetuambia mnataka kutupa viwanja Dar es Salaam mtatupa Dar es Salaam gani viwanja? Dar es Salaam viwanja vimekwisha! Hivi Serikali katika kutupunguzia umaskini inashindwaje kututengenezea angalau mifereji midogo midogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Benki ya Dunia DNDP wametuletea mradi wa kutengeneza Mto Ng’ombe au Mto Sinza…

T A A R I F A . . .

MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Leo wote wanaonipa taarifa ni katika watu ninaowaheshimu sana, lakini kati yangu mimi na yeye sijui nani na data. Mimi wikiendi hii nilikwenda Dar es Salaam, kamvua ka juzi tu kale tumeenda kuokoa vyombo. Hivi ninavyozungumza kijiko kinasafisha mto tena kwa hela ya Mfuko wa Jimbo – Mto Kibangu, nazungumza Mto Msimbazi! Sasa nani hana taarifa, ni mimi niliyetoa hela ya Mfuko wa Jimbo na kukodi kijiko kwa hela ya Mfuko wa Jimbo na kukodi kijiko kwa pesa ya Mfuko wa Jimbo? Au Mheshimiwa Waziri anazungumzia Wailes wakati mimi nazungumzia Mto Msimbazi? Nani ana taarifa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kusema nawaheshimu sana viongozi wangu hawa lakini ninachokisema, nasema kitu ambacho nimepata kwenye field. Nakushukuru sana na nategemea kwa sababu na wewe unahusika kwenye matatizo haya utakuwa makini sana kulinda muda wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi Serikali inaondoa vipi Watanzania kwenye umaskini kwa kudharau kilimo? Hivi tunawaondoa vipi Watanzania kwenye umaskini kwa kuweka masharti yaliyopitwa na wakati kwenye kilimo? Enzi zile za zamani, enzi ambazo Tanzania hatujitoshelezi kwa chakula, enzi zile za wakulima wadogo wadogo wanaolima kupata gunia sita, Serikali ilikuwa inahakikisha wananchi wakilima wasiuze mazao yao kwa sababu wakiuza hizo gunia sita ndani ya miezi miwili wanahemea njaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo Serikali inatoa amri ya kutokuuza mahindi kwa mfanyabiashara kama Sumry aliyeacha biashara ya mabasi akaenda kuwekeza kwenye kilimo, akalima heka 1,000 akalima heka 1,500 amepata mahindi unamwambia asiuze kwa ajili ya njaa? Huyu hakulima kwa sababu ya kutaka kula, alilima kwa sababu akauze! Sasa imefika wakati Serikali tusi-generalize, tusitoe order ambazo zimepitwa na wakati. Hizi order zilikuwa enzi zile za watu kuhemea njaa. Leo watu wanakwenda kulima kama biashara unamzuiaje asiuze? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kaka yangu Harun pale kalima mchele wake unamwambia asiuze atakufa njaa, Harun amelima kwa sababu ya kula? Sasa lazima Serikali iwe wazi, matamko ambayo tuna generalize kipindi hiki wananchi wanakwenda kulima kwa ajili ya kufanya biashara, tusiwakatishe tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, hivi utaondoaje umaskini bila ku-invest kwenye kilimo? Kilimo ndicho ambacho kina uwezo wa kuajiri watu wetu kwa asilimia zaidi ya 70. Kilimo ndicho ambacho kinaweza kikachukua kwa sababu sisi tuna eneo kubwa, sasa leo Serikali kama tulivyojikita kwenye Shirika letu la Ndege, kama tulivyojikita kwenye miundombinu, kama tulivyojikita kwenye umeme, vile vile Serikali ioneshe nia yake ya dhati kujikita kwenye kilimo kwa sababu huko ndiko vijana wetu watakwenda kupata ajira ya kutosha. Sio kwamba watu wanakwenda kulima halafu unaleta Sheria ambazo sio sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye kilimo hivi Serikali mpaka sasa hivi inashindwa kutuambia Watanzania tulime nini? Leo Watanzania tumewaambia wakalime mbaazi, mbaazi hazina soko. Leo Watanzania wanabuni, kuna watu nimesikia wanatoka mikoa ya mbali wanakwenda Mtwara kununua maeneo kwa ajili nao walime korosho kwa sababu baadhi ya mazao imeonekana bei haidumu, bei inayumba, sasa kwa nini Serikali isifanye utafiti, ikatuambia Watanzania limeni kitu fulani. Tusishangae baada ya Watanzania wengi kwenda kuamua kulima korosho tutaambiwa nayo korosho imeshuka bei, hili si jambo ambalo tunalitarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mpango yeye ndiye kazi yake, ndiyo kazi yake kutuelekeza Watanzania tulime nini kitu ambacho tutapata maslahi. Leo tunaambizana tulime mbaazi kumbe hata mkataba na Wahindi hamjaingia. Leo kuna watu wanaleta habari hapa kwamba Wachina wanataka mhogo, hivi ninyi Serikali mmeshazungumza na Wachina? Mmefanya nao mikataba? Tumekubaliana? Hivi leo kwenye kilimo hatuwekezi, leo kwenye uvuvi tumeshindwa kuweka mpango wa kununua meli, tulikubaliana hapa uvuvi wa bahari kuu, hamsemi chochote kwenye bahari kuu hapa zaidi ya kutoa elimu ndogo ndogo, hatuna meli hatuna viwanda vya samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo wafugaji, wafugaji hawa tunawaambia wapunguze ng’ombe wao, wanapunguzaje? Hilo soko la nyama liko wapi? Hivyo viwanda vya nyama viko wapi? Leo nyama yetu ya Tanzania inafika mahali hata kwenye migodi haikubaliki. Nyama ya Tanzania mpaka sasa hivi inakwatwa kwa shoka, hivi kweli Serikali mnafikiri umaskini huu tutauondoa kimuujiza? Umaskini huu utaondoka kwa Serikali kuhakikisha tunaangalia maeneo ambayo Watanzania wengi wapo tena wanafanya kwa gharama zao na Serikali kwenda kuwasaidia. Kama tutakuwa hatufanyi hivi, tutakuwa tunapotea sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo suala la elimu tumelifanya kama biashara. Zamani enzi za mwalimu vijana wote walikuwa wanasomeshwa na Serikali, imefika mahali Serikali ikasema vijana wanasoma wengi hela hatuna tunawakopesha, unamkopesha mtu ili alipe, si lazima achague cha kusoma? Tunawasomesha chochote, hela amechukua ya mkopo, ikishakuwa hela ya mkopo maana yake ni business, hivi sasa wewe umemsomesha mtu kwa hela ya mkopo halafu unamsomesha kutunga mashairi. Haya wamesoma watu 2,000 kutunga mashairi utawaajiri wapi? Unayo industry ya watunga mashairi wewe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanini sasa Serikali hatuji na sera, hatuji na maelekezo, Watanzania wanasoma kwa gharama ya kukopa ili alipe lazima aajiriwe, unamsomesha chochote, lazima tuwaelekeze Watanzania, wasome kitu gani ili wapate kuajiriwa, waweze kulipa zile pesa, lakini tunawaacha tu mtu anakuja anachagua chochote cha kusoma, akienda kwenye soko la ajira, anaambiwa hakuna ajira, halafu huyu mtu anatakiwa alipe mkopo na ndiyo maana haya mapesa…

T A A R I F A . . .

MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimepata bahati, wote wanaonipa taarifa watu wangu ninaowaheshimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilichokisema; hivi wewe unasema mashairi ni fani nzuri inaheshimika, mimi siidharau lakini je wewe unaheshimu kama unavyoniambia mie? Unawaajiri wangapi? Kwa sababu ninachosema, huyu mtu umemkopesha na ukishakopa dawa ya deni kulipa! Je, unahakikisha anachokisoma kitamwezesha kulipa? Hawa watu mtawaajri nyie Serikali hawa watunga mashairi? Kwa nini tusisomeshe madaktari ambao tunaweza kuwapeleka Zimbabwe, tunaweza tukawapeleka Malawi, kwa nini tusisomeshe Ma-engineer wa gesi ambao wana soko kubwa ulimwenguni, kwa nini tusisomeshe fani za kilimo ambazo zinaenda kutumika. Tunasomesha chochote! Halafu then akija kijana anatafuta ajira unamwambia Aah! Unajua hii fani yako hii kwenye ajira kweli haitakiwi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)