Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Jaku Hashim Ayoub

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nichukue fursa hii kukupongeza kwa dhati kwa kuniruhusu kuchangia hoja hii. Bila kuniruhusu nisingeweza kuchangia hoja hii kwa hiyo nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza tena Mheshimiwa Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada anazochukua kwa wananchi wake na kwa jinsi anavyowatumikia. Nichukue fursa hii tena kuwapongeza wale Mawaziri na Naibu Mawaziri waliopanda hivi juzi kwa kupata vyeo hivi na niwape pole waliokuwa wakitegemea, lakini hawajapata nafasi hizi mpaka muda huu. Niwaombe wasikate tamaa, Mwenyezi Mungu siyo Athumani lakini niwaambie tu uteuzi wao huu wanaujua nini maana yake? Uteuzi huu Mheshimiwa Rais aliotoa Mawaziri na Naibu Mawaziri ili wamsaidie kutumikia wananchi kinyume chake Mawaziri na Naibu Mawaziri simu mnazifunga, hamuwatumikii wananchi, siyo kitu kizuri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kaziteua Wizara kama Wizara ya Afya wenye matatizo ya afya waende afya, Wizara ya Elimu waende wenye matatizo na elimu, Wizara ya Ardhi waende wenye matatizo ya ardhi lakini kwa masikitiko simu ukimpigia Waziri hapokei, ukimpigia Naibu Waziri hapokei, humu ndani tumo sawasawa haya mambo yanageuka. Aliyeko mbele mngoje nyuma, aliyeko juu msubiri chini atateremka tu. Hivi vyeo ni dhamana na tutakwenda kuulizwa siku ikifika tumewatumikia vipi wananchi. Kuna milango mitatu ya kuingilia humu ndani ya Bunge hili, kuna Jimbo kutoka Ikulu, kuna Viti Maalum na uchaguzi wa wananchi, hiki chombo kina uzito kutokana na wananchi. Wananchi ndiyo waliopotupa dhamana ya kuja kusema matatizo yao humu ndani. Kuna siku tutakwenda kuulizwa hizi dhamana zetu tumezitumia vipi, haya mambo ya kupita tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika mchango wangu sasa kuhusu TRA. Mheshimiwa Waziri kwa masikitiko na unyonge mkubwa sana kitendo ulichokifanya cha kutatua kero ya Kenya na Tanzania kuhusu maziwa na cigarette umechukua muda mfupi sana, lakini kero ya Zanzibar bado kila Waziri kinamshinda. Leo Muungano wetu huu tunasema kwa mdomo tu tunataka uendelee kudumu kwa vitendo. Mali inayotoka Uganda, Kenya, Burundi, Zaire, Zambia ikiingia Tanzania wala huulizwi kitu, leo mali inayotoka Zanzibar ukiingia nayo Dar es Salaam utafikiri umeleta unga, huu uonevu wa aina gani? Dkt. Mpango Wazanzibari hamtufanyii haki. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mzanzibar kachukua gauni zake tatu anakuja hapo bandarini anaambiwa weka chini, tv tu moja, mbili anaonewa, hii haki ikoje? Nimpongeze sana dada yangu Mheshimiwa Saada Mkuya, kazungumza vizuri sana lakini huu Muungano tunaosema ni wa upande mmoja tu jamani? Tunasema huu Muungano uendelee kudumu na mimi nasema uendelee kudumu, Zanzibar ukiacha zao la karafuu tegemeo kubwa ni biashara. Wenzetu Tanzania Bara Alhamdulillah, endeleeni kushukuru tuna madini, mbuga na neema nyingi tunazo lakini leo biashara ile nguo tatu au nne, miche mitatu ya sabuni unasumbuliwa pale mwisho mchele unaonunua pale bandarini unalipishwa pana kimizani kidogo kimewekwa pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala siyo la upande mmoja Mheshimiwa Saada kazungumza bado hujafika Zanzibar, mimi nikuombe ufike. Pindipo utakapokusanya mapato Mheshimiwa Rais atakusifu, tuangalie biashara, huku kidogo, huku kidogo, kuku anataga yai moja ukamlazimisha mayai matatu utamuua, utakosa kuku. Chukua huku kidogo, huku kidogo pishi inajaa lakini kuku yule anataga yai moja, unamlazimisha leo leo atage matatu atakwenda wapi, tutaua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu twende Kariakoo ukaangalie milango ya maduka nani anaitaka saa hizi? Samora mlango ulikuwa unakodishwa bei kubwa sasa hivi milango imefungwa. Fikiri Mheshimiwa Waziri huu ni ushauri wangu wa bure wala sitaki kulipwa mimi. Kaa na wafanyabiashara utazame nini tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Muungano Zanzibar tunauhitaji kwa kila hali miongoni mwao ni mimi kutokana na udogo wetu, lakini mzigo utoke Kenya, Rwanda, Burundi hauulizwi kitu, mzigo ukitoka Zanzibar ukifika hapa aibu. TRA ni moja, formula yake ni moja, vigezo vyake ni vimoja, Waziri nikuombe kwa masikitiko makubwa, Wanzanzibar ukiacha karafuu wanategemea biashara. Juzi umetatua tatizo la Kenya kwa muda mfupi tu, leo unatuaacha sisi ndugu zako wa damu. Umetatua juzi tu tumekupongeza lakini litatue na hili pia. Taa huwashi nje, unawasha kwanza ndani ya nyumba yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawashaje nje kabla ya kuwasha ndani huwezi kuona na sadaka sisi tunasema inaanzia nyumbani ndipo utoe nje. Kwa hii kero dada yangu kazungumza sana hapa, fanya uwaite wafanyabiashara, wanafunga milango wanaanza kuondoka. Tembea na kama uko tayari tufuatane nikakuoneshe mlango huu umefungwa, huu umefungwa utahesabu milango mingapi. Tufike wakati tupunguze, tujihurumie jamani mapato tunahitaji wewe kusanya mapato mazuri uone Mheshimiwa Rais atakavyokusifu. Nchi inataka kwenda kwa mapato lakini tukianza kubana kwa marungu, leo watu wananyang’anywa komputa zao wanavamiwa na TRA, polisi imekuwa TRA sasa hivi watu wanasumbuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri sisi sote humu ndani vyeo vyetu vimoja tunaitwa Waheshimiwa tofauti tu ni Waziri na Waheshimiwa na haya mambo yanageuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, naomba kukaa.