Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Kiza Hussein Mayeye

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na ardhi kwa kunipa uzima na afya tele na kunifikisha mahali hapa siku hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nikishukuru chama change, Chama cha Wananchi (CUF) chini ya Mwenyekiti mahiri Profesa Ibrahim Lipumba pamoja na Naibu Katibu Mkuu Mheshimiwa Magdalena Sakaya kwa kusimamia vizuri Katiba ya Chama cha Wananchi (CUF). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe shukrani zangu za dhati kwa Wabunge wote wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano, kutupokea vizuri, kuwa pamoja na sisi, kutuelekeza na kutufundisha mambo mbalimbali toka tulivyoingia Bungeni mpaka siku hii ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri Dkt. Phillip Mpango kwa Mpango huu wa Maendeleo, Mpango huu ni mzuri lakini haimaanishi kila kitu kizuri hakina kasoro. Kwa hiyo, mimi nimpongeze lakini pia naomba nichangie kama ifuatavyo katika Mpango huu wa Maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa kwanza nataka nianzie katika suala zima la hawa wawekezaji. Serikali yetu inasisitiza na inasema kwamba tunahitaji wawekezaji. Kwa hiyo, ningeomba Serikali yetu iwape wawekezaji uwezo wa kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali katika nchi yetu ya Tanzania. Kuna maeneo ambayo kwa mfano ninakotoka Mkoa wa Kigoma, huu ni mkoa ambao uko katika plan hii ya Regional Economic Zone.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma mpaka sasa kuna zaidi ya heka 690 katika eneo la Kisezi ambalo limetengwa kwa shughuli hizi za uchumi. Ningemuomba Mheshimiwa Waziri, mhakikishe kwamba mnavutia wawekezaji katika eneo hili kwa sababu eneo hili ni potential, ni eneo ambalo tukilitumia vizuri kwa uchumi tutainua Pato la Taifa na hata mkoa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimwambie Mheshimiwa Waziri katika eneo hili la Kisezi tayari kuna mwekezaji ambaye anatengeneza umeme wa jua na mpaka sasa ameshatengeneza megawati tano, lakini kuna ukwamishaji. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, kama Serikali yetu inasema kwamba inatoa kipaumbele katika sekta binafsi ihakikishe umeme huu wa jua ambao mwekezaji huyu ameuweka katika eneo lile uweze kuunganishwa na TANESCO Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme huu TANESCO wanakataa kuunganisha, lakini mpaka leo Kigoma hatujaingia katika Gridi ya Taifa. Ningeomba tuingie katika mpango wa Gridi ya Taifa na sio Kigoma tu bali ni Mikoa yote ya Magharibi ikiwepo Sumbawanga, Katavi na Kigoma. Kwa hiyo, naomba katika Mpango huu mhakikishe kwamba mikoa hii tunaingia katika Gridi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia TANESCO Kigoma wanasema kwamba hawawezi kuunganisha umeme huu lakini katika akili ya kawaida unajiuliza ni kwa nini hawataki? Kwa sababu kama mwekezaji huyu anatumia shilingi 490 kwa unit moja TANESCO Kigoma inatumia shilingi 700 ka unit moja kwa akili ya kawaida unaona kabisa kwamba mwekezaji huyu umeme wake uko chini. Ni kwa nini Serikali haitaki mwekezaji huyu umeme wake uunganishwe TANESCO Mkoa wa Kigoma? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika maeneo yale ambayo Serikali imeyatenga kama maeneo ya maendeleo, nirudi Kigoma. Kigoma mpaka dakika hii bandari kavu imeanzishwa, hii Central Corridor, Umoja wa Nchi za Maziwa haya Makuu wamefikia uamuzi kwamba Kigoma iwe ni bandari ya mwisho kwa mantiki kwamba watu kutoka Burundi, Kongo badala ya kufuata mizigo Dar es Salaam wataweza kuifuata Kigoma na tayari eneo limetengwa la Katosho – Kahagwa, tunatengeneza kitu tunasema CIF Kigoma. Kwa hiyo, tutakuwa na bandari kavu pale na tayari watu wamepisha ujenzi. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri katika Mpango huu tuhakikishe kwamba bandari hii inaanza mara moja kwa sababu kupitia bandari hii vijana wa Kigoma watapata ajira lakini sio Kigoma tu Tanzania nzima kwa sababu huu mpango ni wa Taifa watapata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyeiti, pia nimwambie Waziri kwamba mbali na ajira mzunguko wa pesa utakuwa ni mkubwa katika Mji wa Kigoma na mzunguko wa pesa ukiwa mkubwa katika Mji wa Kigoma hilo ni Taifa, Taifa tutapata pato. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri ufanye unavyoweza bandari hii ianze mara moja. Labda ningejua, Wizara ya Fedha mpaka sasa mmejipangaje katika suala hili na Mamlaka ya Bandari imefikia wapi katika utekelezaji wa maamuzi haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia Mpango wa Mheshimiwa Waziri. Hakuna mahali ambapo nimeona kuna uwezeshaji wa kijana na mwanamke. Hakuna mtu asiyejua kwamba kijana ni mtu muhimu katika Taifa hili lakini hakuna mtu asiyejua kwamba mwanamke ni mtu muhimu katika familia na Taifa. Naomba sasa Serikali ije na Mpango madhubuti wa kumwezesha kijana huyu ambaye leo anamaliza shule lakini hana ajira na mama huyu ambaye amekaa nyumbani hana kazi. Tuandae mikakati ambayo itamwezesha mama, wote tunajua mama ni nani katika familia, ukimwezesha mama atasomesha watoto. Kwa hiyo, tuwe na vyanzo vya kuwasaidia akina mama, mabenki yatoe mikopo kwa akina mama. Kwa hiyo, ningeomba Mheshimiwa Waziri katika Mpango unaokuja umfikirie sana kijana na mama wa Kitanzania, SACCOS za akina mama Serikali iweze kuzisaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie tena suala la uwekezaji. Kumekuwa na maeneo mengi ambayo wawekezaji wanataka kwenda kuwekeza lakini hakuna ushirikiano mzuri. Kwa taarifa nilizozipata katika eneo hili hili la Kisezi, Mkoani Kigoma Serikali ya Japan inataka kuja kuwekeza, watengeneze bidhaa wao wenyewe na watafute masoko wao wenyewe masoko wao wenyewe na watumie uwanja wa ndege wa Kigoma. Hata hivyo, Serikali haioneshi ushirikiano na wawekezaji hawa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ningeomba kama kweli tunataka kusonga mbele katika maendeleo ya Taifa tutoe kipaumbele katika suala zima la uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika suala zima la kilimo. Hakuna mtu asiyejua kwamba kilimo ni uti wa mgongo. Wote hapa leo ni Mawaziri, Wabunge wengi tumesomeshwa na wazazi wetu kwa sababu ya kilimo. Naomba Mpango huu utakaokuja sasa muwasaidie wakulima, muwape pembejeo, mbolea, muwasaidie kupata masoko kwa sababu tunaposema leo tuna nchi ya viwanda, huwezi kuwa na viwanda kama wewe mwenyewe huna product za kupeleka kwenye kiwanda chako. Huwezi kusubiri mahindi kutoka Kenya, huwezi kusubiri korosho kutoka nchi jirani, tuhakikishe sisi wenyewe tunakuwa na product zetu ambazo tutazipeleka katika viwanda vyetu. Kwa hiyo, nimuombe sana Waziri, Wabunge wengi wameongelea kuhusu suala la kilimo, naomba kilimo kipewe kipaumbele, kilimo ni uti wa mgongo. Kama Serikali tunataka kusonga mbele tuhakikishe kilimo kinathaminiwa kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niongelee suala la elimu. Miundombinu ya elimu katika nchi yetu ni mibovu. Walimu wengi nyumba zao ni mbovu. Walimu hawa ndiyo wametufikisha mahali hapa leo. Walimu hawa ndiyo wamekutoa wewe Waziri, mimi Mbunge.

Kwa hiyo, naomba tuwathamini walimu kuanzia kwenye makazi, nyumba wanazokaa ni chache. Mikoa mingi ina changamoto walimu hawana nyumba na hata nyumba ambazo zipo unakuta haziko katika mazingira mazuri. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri atakapokuja na Mpango huu ahakikishe miundombinu kwa walimu, waongezewe mishahara lakini nyumba na makazi yawe mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika elimu nizungumzie suala la madarasa. Maeneo mengi hasa ya vijijini wanafunzi wanasomea nje, hakuna madarasa. Serikali ijitahidi kuweka madarasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nizungumzie miundombinu ya wanafunzi. Shule nyingi vijijini watoto hawana vyoo. Sasa jiulize kama tunashindwa kuweka matundu ya vyoo katika shule, binti huyu ambaye amekwenda shule, kwa sababu tayari kuna watoto wa darasa la saba wameshaanza kuona hali ya usichana wao, ameingia katika hali ya usichana hakuna maji, hakuna choo mnamweka katika mazingira gani binti huyu wa kike? Kwa hiyo, mnamfanya sasa huyu binti akishaingiwa na ile hali na wenzie wamemuona, kesho hawezi kurudi shule. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri mhakikishe mnawajali wanafunzi katika huduma za maji mashuleni, vyoo na hasa mtoto wa kike mumsaidie apate huduma hizi ili aweze kwenda shule kama watoto wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naomba kuunga mkono hoja, ahsante.