Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Juma Othman Hija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika mpango huu wa maendeleo. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa juhudi kubwa anayochukua katika kuongoza nchi hii. Namuombea Mungu ampe uwezo na afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii ya Fedha, Naibu Waziri na watendaji wake wote kwa umakini wa kuandika na kuwasilisha Mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia Mpango huu napenda kusisitiza maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kuhusu kuongeza uwezo wa kupambana na umaskini kwa wananchi. Miongoni mwa kundi kubwa la wananchi wa Tanzania ni wafanyabiashara na wakulima. Hivyo, ni vyema Serikali kuendelea kuchukua juhudi za makusudi kuwawekea mazingira mazuri ya kufanikisha shughuli zao. Serikali inapaswa kuwawekea utaratibu maalum wa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu ili waweze kufanya biashara zao kwa utulivu na kuweza kujipatia kipato kuweza kupunguza umaskini, hasa wafanyabiashara walio wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sekta ya uvuvi, sekta hii bado haijaonesha mafanikio katika kuwaendeleza na kuwanyanyua wavuvi wa nchi hii. Bado mpaka leo wavuvi wanahangaika kwa kukosa vifaa vya uvuvi vya kisasa. Hivyo, naiomba Serikali ichukue juhudi za makusudi kuwaendeleza wavuvi kwa kuwapatia zana za kisasa. Aidha, Serikali iunde benki ya wavuvi, ili iweze kuwakopesha wavuvi kwa kuweza kumudu kununua vifaa vya kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miradi ya maendeleo, Serikali ina nia nzuri katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo, lakini miradi mingi katika nchi yetu inakosa ufanisi kwa sababu kadhaa. Moja kati ya sababu hizo ni upatikanaji wa fedha kwa wakati. Hivyo, naiomba Serikali kupeleka pesa kwa wakati katika taasisi husika ili kuweza kwenda na wakati wa mipango kazi ya miradi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.