Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

Hon. William Mganga Ngeleja

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

MHE. WILLIAM M. NGELEJA – MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SHERIA NDOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine tena ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Kama ambavyo umeridhia nifanye kazi hii kwa niaba ya Kamati yako unayoiongoza ya Sheria Ndogo naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufikia mahali hapa tulipofikia na hasa katika uhai wa Kamati yetu chini yako wewe.

Pili naendelea kuwapongeza na kuwashukuru sana viongozi wetu wa Bunge tukiongozwa na Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti kama kawaida. Tunaendelea kuwashukuru sana Wabunge wenzetu kwa ushirikiano ambao wametupa na hadi kufikia mahali hapa, taarifa yetu imechangiwa na baadhi ya Wajumbe kwa kadri ambavyo muda umeruhusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu tu nitambue kwamba waliopata nafasi ya kuchangia kwa kuzungumza ni Mheshimiwa Daniel Mtuka, Mheshimiwa Ester Mmasi, na kwa upande wa Serikali Mheshimiwa Mwenyekiti umemsikia Mheshimiwa Profesa Kabudi, Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na Mawaziri kwa ujumla waliozungumza kwa kuchangia katika taarifa hizi tatu ambazo zimewasilishwa.

Ninatambua mchango wa Mheshimiwa Ikupa, Mheshimiwa Kakunda hao ni Naibu Mawaziri lakini Mheshimiwa Waziri Jafo, Mheshimiwa Mkuchika wote hawa hakuna hata mmoja ambaye amepinga taarifa ya Kamati hizi na sisi kwa sababu ni sehemu ya Kamati hizi tatu tunatambua mchango wao tunasema ahsanteni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapofanya majumuisho pia tunakuwa tunajielekeza kwenye kile ambacho Serikali imezungumza. Kwa sababu pamoja na kwamba sisi tunafanya majumuisho ya taarifa hizi, lakini kwa kweli hoja nyingi ambazo Waheshimiwa Wabunge na sisi sehemu ya Kamati tulizozizungumza ufafanuzi wake umetolewa kupitia Waheshimiwa Mawaziri wakati wanachangia, na ndio utaratibu. Kwa hiyo, tunawapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri kwa kurahisisha kazi hii, na mimi naamini kazi hii haitafika dakika 15 kama ambavyo Mheshimiwa Mwenyekiti umesema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sisitize tu kwamba alichomalizia kukisema Mheshimiwa Jenista, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ni kweli kabisa Kamati yetu imekuwa ikifanya kazi ya uchambuzi, na asubuhi tulizungumza kwamba kwa kipindi cha mwaka mmoja tumefanya uchambuzi wa sheria ndogo 404. Katika sheria hizo 404 sheria 180 zilionekana kuwa na dosari ambazo zilihitaji marekebisho. Sasa ukipiga mahesabu ya haraka hizo sheria 180 maana yake unazungumzia asilimia 44 point kadhaa kuelekea kwenye asilimia 45.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake ni nini, kwa huu mfumo ambao tunao wa utungaji wa sheria ndogo kwa sababu hizi zinatungwa na mamlaka mbalimbali za Serikali, maana yake ni kwamba hizi ni dosari ambazo tumezibaini wakati zimeshaanza kufanyiwa kazi. Ukitaka kwenda zaidi unasema mpaka wakati ambapo tumependekeza marekebisho na Serikali ikafanya marekebisho yaliyofanywa baada ya Kamati kubaini na Waheshimiwa Wabunge kuridhia maana yake ni kwamba madhara hayo yameshawaumiza wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe ndiyo maana tunasisitiza kwamba Serikali iendelee kuimarisha vitengo vya sheria katika mamlaka mbalimbali na umakini wa utungwaji wa hizi sheria ndogo ili tupunguze hiyo fursa ya kuwa na dosari katika sheria zetu ndogo na hivyo kupunguza kabisa ikiwezekana kumaliza kabisa kuwaumiza wananchi kabla ya hizo sheria ndogo hazijafika Bungeni kwa utaratibu na mfumo tulionao sisi wa utungaji wa sheria ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaishukuru sana Serikali kwa kukubali, lakini kwa dhati kabisa kwa niaba yako Mheshimiwa Mwenyekiti naendelea kuwapongeza sana Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati yetu kwa muda waliojitolea. Kwa sababu kama wasingekuwa makini tusingeweza kubaini hii asilimia 45 ya dosari zilizomo katika Sheria Ndogo 180 kati ya sheria 404 tulizozifanyia kazi katika kipindi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nataja waliochangia kwa kuzungumza pia natambua mchango wa maandishi wa baadhi ya Wabunge wenzetu waliopata fursa hiyo; wa kwanza ni Mheshimiwa Rhoda Kunchela ambaye amechangia kwa maandishi na amezungumzia kasoro zinazopatikana katika baadhi ya Sheria ndogo, lakini pia Mheshimiwa Mary Deo Muro tunakushukuru kwa mchango wako wa maandishi, pia Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, hawa ni wale ambao walichangia kwa kuandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa sababu Serikali imekubali kwamba inaridhia maoni na ushauri wa Kamati; na kwa sababu maoni na ushauri huu tumezungumza kupitia taarifa yetu na hatimaye tumependekeza Azimio la Bunge kwenye maeneo ambayo tunapendekeza yakafanyiwe marekebisho naendelea kusisitiza kwamba Serikali ifanye hivyo kama tulivyoshauri kwamba kabla ya Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge la Jamhuri wa Tanzania tutakapokutana hapa hasa kwenye kamati, Serikali iwe imefanya jambo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea tena kusisistiza kwa Bunge na Watanzania kwa ujumla, kwamba Sheria ndogo hizi zina umuhimu wake. Mheshimiwa Profesa Kabudi Waziri wa Katiba na Sheria amesema, wakati anaunga mkono hoja na mchango wa Mheshimiwa Daniel Mtuka kwamba hizi sheria ndogo ama kanuni zinapochelewa kutungwa zina athiri na wakati mwingine zinakwaza utekelezaji wa sheria mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tumeona Sheria ya Madini kwa namna ambavyo ilikuwa imesimama utekelezwaji wake kwa sababu ya kanuni hazijatungwa kwa sababu ya sheria ndogo hazijatungwa, kwa hivyo ni muhimu sana sana kwamba kanuni ndogo zitungwe ama sheria ndogo zitungwe mapema kadri inavyowezekana na ziwashirishwe Bungeni ili tupunguze ile fursa ile ya kurekebisha dosari ambazo zinaweza kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo sisi kama Kamati kwa niaba yako tunapokea pongezi zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri kwa Kamati yako na Kamati zingine, lakini pia na sisi tunasisitiza nje ya taarifa hii nje ya yale ambayo tumeyaazimia kama sehemu ya maazimio na ambao tunaomba Bunge liliridhie Mheshimiwa Jenista Mhagama kama Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye eneo la ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali tunashukrani na pongezi zetu za dhati kwa kazi kubwa mliyoifanya. (Makofi)

Sisi tunaofanyia kazi eneo hilo tumeona mapungufu yaliyokuwepo kwenye miaka ya nyuma, lakini baada ya kufanya mabadiliko hasa kwenye Mtendaji Mkuu na timu na kuipanga timu upya katika hicho kitengo ama hiyo Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali tumeona mabadiliko makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunakwenda mbele kidogo, kama Wajumbe wa Kamati kwamba kwa sababu aliyepo sasa anakaimu; na kwa sababu anafanya kazi kubwa sisi kazi yetu ni kutoa maoni na kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitajali sana basi iongeze kasi ya mchakato ama kumthibitisha ama kumteua CEO ambaye ataisimamia hiyo idara ili maamuzi yote yafanyike. Kwa sababu tunafahamu kwamba kuna tofauti kubwa ya kuwa kaimu na kuwa mwenye mamlaka kamili. Kwa hivi sisi tunatoa mapendekezo yetu na ushauri wetu kwenu kwamba mlifanyie jambo hilo maamuzi ili kazi iendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na Waheshimiwa Wajumbe kwa ujumla, ukifuatailia taarifa zetu utakuta kwamba mambo tunayoyasisitiza yenye kasoro kubwa moja ni yale ambayo yanakiuka misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kasoro ambazo zinahusu ukiukwaji wa sheria mama, sheria ndogo ambazo zinatungwa na sheria nyingine za nchi, lakini pia yapo masuala ya kiuhariri na kiuandishi, pia ukiukwaji wa haki za binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunasema haya yote yanatokana tu na umakini, kukiwepo na umakini yote haya yatabainika. Ndiyo maana nasisitiza tena kwa mara nyingine kwamba sisi kama Kamati tuliipenda sana Kamati hii na tukafikia hatua ya kuomba kwa sababu tumefurahishwa na jinsi ambavyo changamoto zinazokuja mbele yetu na tunavyozifanyia kazi inaonekana ni jambo la heri sisi tuendelee kuwepo pale. Mheshimiwa Mtemi utakapokuwa una toa mwongozao wako wa mwisho pamoja na kwamba wewe ndiyo Presiding Officer leo, lakini kwa nafasi yako unayo nafasi pia ya kufikisha ujumbe na kuthibitisha haya ninayoyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo kwa mara nyingine tena yale ambayo yamejitokeza kwenye taarifa ya Kamati zetu na baadhi ya wachangiaji waliochangia hasa wa maandishi yanayohusu Kamati ya Katiba na Sheria nitayafikisha mahali pake. Yako mapendekezo ya kwenye marekebisho ya Sheria Ardhi na Sheria ya Ndoa; lakini kwa mazingira tuliyonayo naamini kwamba hayo ni masuala ambayo yanahitaji muda zaidi na kufuata utaratibu unao kubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naliomba tena kwa mara nyingine Bunge lako Tukufu liliridhie yale tuliopendekeza, tulioyatolea maoni na kutoa ushauri na hatimaye tukapendekeza kwamba Bunge liazime kama ambavyo taarifa yetu rasmi tulivyoiwasilisha inavyosomeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na kwa hatua hii naomba kutoa hoja kwa mara nyingine, ahsante.