Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Stephen Hillary Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nipo. Kwanza nianze kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Korogwe Vijijini kwa kuniamini na leo nipo hapa kwa mara ya pili Mungu awabariki sana, sitawaangusha, nitafanya kazi kwa jinsi walivyonituma.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nataka nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano pamoja na Mawaziri, safari hii wametupa nguvu ya kuonesha kabisa kwamba safari hii hapa ni kazi tu. Naomba kazi hii isiishie mijini iende vijijini ikaangalie kero za
wananchi.
Mimi nitajikita katika mambo matatu au manne makubwa. Sasa hivi Serikali ya Mheshimiwa Pombe Magufuli imeamua kufanya kazi, lakini naomba sana Serikali ihakikishe inamaliza kwanza zile ahadi za nyuma ambazo zilitolewa kwa wananchi. Kwa mfano, sasa hivi
watu wana mpango wa kujenga Bandari ya Bagamoyo, wangeacha kwanza Bandari ya Bagamoyo wangezijenga Bandari za Tanga pamoja na Mtwara ili iwe kiegesho kikubwa.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiyafanya haya Watanzania watatuelewa vizuri sana. Hatuwezi kila siku kuwa tunaanzisha vitu halafu vinaishia njiani. Kwa mfano, suala la reli, reli ni kitu muhimu sana kwa Watanzania, lakini inaangaliwa sana reli ya kati, inaachwa reli ya kutoka Tanga kwenda Arusha kwenda Musoma. Huko pia kuna maeneo ambayo wananchi wanafanya biashara, wananchi wana mizigo wanataka kubeba, wananchi wanataka kuona na wao wanapanda treni kama wanavyopanda wenzetu wa kati. Hii Tanzania ni moja, Watanzania ni wamoja, wakati wakiwa nje tunakuwa tofauti, lakini tukiwa hapa ndani wote tunatetea haki za Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nataka tuzungumzie mambo ya viwanda. Sasa hivi tunasema kwamba Tanzania ya viwanda, lakini kuna viwanda vingi vimekufa hakuna mpango wa aina yoyote ambao unaweza kuanzishwa naomba tusijenge viwanda vingine tuanze kwanza kuvifungua viwanda vya Mponde ambavyo vimefungwa kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawapati chai, chai hakuna mahali pa kuipeleka, Watanzania wamekosa kabisa kuamini. Naomba kwanza tuhakikishe tunawafungulia viwanda Watanzania, vile vilivyokuwa vimefungwa kule Tanga, kwa mfano, Kiwanda cha Chuma,
Kiwanda cha Omo, Kiwanda cha Mbao na viwanda vingi mpaka Kiwanda cha Blanketi kimefungwa. Sasa leo tukisema tunataka kuanzisha viwanda, wakati vya zamani bado, naomba kwanza Serikali yangu Tukufu, naipenda sana na safari hii imetupa nguvu sisi Wabunge, tunafanya kazi kwa kujiamini, wahakikishe kwanza vile viwanda vya zamani vyote vinaamshwa na Watanzania wengi wanapata kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni suala la mama ntilie na vijana. Serikali ya Mheshimiwa Pombe Magufuli iliamua kwamba, mama ntilie na hawa wanaofanya biashara ndogo ndogo wasishikwe ushuru. Sasa hivi inashangaza sana, watu badala ya kushika ushuru
mkubwa mkubwa katika maeneo, wanawakimbiza watu wa bodaboda na mama ntilie na wale akinamama ambao wanauza hata vitu vidogodogo, nyanya pia mtu analipa risiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye Jimbo langu aliwahakikishia Watanzania wanaoishi Korogwe kwamba ushuru mdogo mdogo utafutwa, lakini cha kushangaza watu wanauona huo ushuru mdogo mdogo wa kuwasumbua Watanzania wa hali ya chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali hii, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Mkuu ni mchezaji wangu wa mpira, anajua kabisa kero hizo kwa sababu huko kote tulizunguka naye na hata kwenye Jimbo langu alifika kunifungulia shule. Naomba sasa wale wanaoshika ushuru
mdogo mdogo waache, kwa sababu wakifanya hivyo na sisi Wabunge tuna nguvu sana ya kujenga hoja hapa ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la barabara ni suala muhimu sana. Kuna barabara ambayo toka mwaka 2010, Serikali ya CCM tulisema kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami, naomba iangaliwe sana hii barabara ya kutoka Korogwe kupitia Bumbuli kwenda mpaka Soni ili
iwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba vilevile katika suala la maji, tusianzishe miradi mingine, kuna mradi mkubwa wa kutoka Kilimanjaro kuja mpaka Mkoa wa Tanga kupitia Kata ya Mkomazi na Tarafa ya Mombo. Naomba Waheshimiwa Mawaziri mliopo, ni majembe ambayo tunayaamini kabisa, safari hii hakuna tena lelemama ni kazi, naomba mradi ule umaliziie ili Watanzania tuendelee kuipenda, maana sasa hivi Watanzania wote wanaipenda Serikali ya Chama cha Mapinduzi, kwa nini? Kwa sababu ya Jembe Magufuli. Sasa kwa haya naomba pia tuhakikishe kwamba tunakamilisha bila tatizo la aina yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la umeme ni muhimu sana. Mheshimiwa Profesa mwenzangu Muhongo umeshaniahidi leo hapa, nimekufuata kwako umeniambia vile vijiji vyangu vyote vilivyokosa umeme, safari hii vinapata umeme vyote. Sasa isiishie tu katika
mazungumzo yetu ya mimi na wewe, maana hapa tupo maprofesa wawili tu tuliohitimu kama wewe, naomba unikamilishie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona niyaseme haya kwa sababu, leo hapa tumekuja kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Pombe Magufuli. Naamini kabisa Watanzania wanataka kuona Tanzania ile ya juzi
siyo Tanzania ya kesho. Nikiongea mpaka kesho sitakuwa na lolote la maana la kuwasaidia ila ni kuiomba Serikali yangu kwamba yale yote yaliyoahidiwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais, tuyatekeleze kwa kipindi ili mwaka 2020, tuteremke tu maana safari hii tumepata shida kweli kweli. Mungu awabariki sana. (Makofi)