Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia naomba nimshauri Mheshimiwa Rais kwamba afanye uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini pamoja na hii nafasi ya Mheshimiwa Dkt. Possi, kwa sababu nimeona kuna baadhi ya Wabunge wa Chama cha Mapinduzi wanashindana kutafuta nafasi hizo kwa kushambulia upande huu. Kwa hiyo, naomba niseme tu kwamba afanye uteuzi huo haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ushauri huo, naomba niendelee sasa kuchangia bajeti ambayo iko mbele yetu. Naomba niseme tu kwamba katika bajeti hii, yako baadhi ya mambo ambayo nimeyaona kwa kweli hayatawasaidia Watanzania, naona tunaenda kuwaongezea Watanzania mzigo wa umaskini. Kwa mfano, liko jambo hili la ada ya leseni ya magari. Ada ya leseni ya magari kwenda kuihamisha kupeleka kwa wale watu wanaotumia mafuta ya taa, kupeleka kwa wanaotumia petrol na diesel, hapa hatujatatua tatizo tumeruka majivu na kukanyaga moto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba Watanzania walio wengi wanaoishi mijini na vijijini, wanatumia mafuta ya taa na ndio wengi hao maskini. Leo tumeamua kuwatwisha magunia ya mawe kwa kuwaongezea bei kwenye nishati hii ya mafuta ya taa. Umeme mmewanyima, hali ni mbaya kweli kweli! Hali ni ngumu huko vijijini, lakini leo unaenda kumpandishia Sh.40/
= kwenye mafuta ya taa. Hii siyo sahihi hata kidogo! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii alipokuwa anaingia madarakani Mheshimiwa Rais alisema kwamba yeye anawaonea huruma maskini. Alizungumza akasema yeye ni rafiki wa maskini. Sasa urafiki na maskini, huyu unayemtwisha mzigo huu wa kumwongezea Sh.40/= kwenye mafuta ya taa, ni masikini wa namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni nini? Tafsiri ni kwamba leo Tanzania wanaotumia magari hata asilimia 20 hawafiki. Unachukua asilimia 20 ya Watanzania wanaotumia magari unaenda kuwatwisha mzigo Watanzania zaidi ya asilimia 80 ambao hawana magari eti walipie hii motor vehicle. Hii siyo sahihi hata kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu niwaambie Watanzania, najua tu japokuwa hawanisikilizi, lakini najua tu watasikia hata kwa njia nyingine, kwamba ile Serikali ya Awamu ya Tano waliyotegemea kwamba ingeweza kuwasaidia sasa imeshawasaliti haina msaada tena kwao na hapo waangalie mbadala mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni jambo la ushuru wa Sh.10,000/= kwa nyumba ambazo hazifanyiwa uthamini. Yaani leo Watanzania walio wengi wanaoishi kwenye nyumba ambazo siyo bora, ukienda Mkoa huu wa Dodoma, ukienda huko Mtera kwa Mheshimiwa Lusinde, ukienda huko Chemba na maeneo mengine; na mikoa mingine; nimetoa mfano Dodoma tu, lakini yako na maeneo mengine pia, utakuta nyumba ni ya nyasi, juu wameweka udongo, wamejengea miti, leo huyu mwananchi eti unamwambia eti akatoe Sh.10,000/=, kwa kweli naomba tafadhali atakapokuwa anahitimisha, Mheshimiwa Waziri naomba mwombe Watanzania msamaha kwamba tulikosea, tuliteleza kidogo tulikuwa hatumaanishi hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unaposema walipe Sh.10,000/= kwa kila nyumba, ni kuwatwisha mzigo mzito sana maskini hawa. Hofu yangu kubwa sana ni kwamba ipo siku tutaambiwa tuanze kulipia pumzi tunayoivuta. Kama leo mnasema tuanze kulipia vibanda vyetu vidogo vidogo ambavyo tunavyo, leo vifaa vya ujenzi ni gharama, kila kitu ni gharama, lakini wanaopata shida zaidi ni watu maskini zaidi hawa wa vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafadhali naomba kama mimi labda sikuelewa vizuri, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha, atoe tamko kwamba hatukumaanisha tuichokiandika hapa, au wafute kabisa hiki kitu, kwa kweli watakuwa wamefanya jambo baya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la ukuaji wa uchumi usiopunguza umaskini. Leo tunasema kwamba uchumi wa Taifa letu unakuwa kwa asilimia saba. Uchumi huu ambao tunasema unakuwa kwa asilimia saba, lakini uchumi huu haupunguzi umaskini wa Watanzania wetu. Ni kwa nini uchumi haupunguzi umaskini wa Watanzania? Uchumi umebaki kukua kwenye makaratasi kwa sababu sekta ambazo zinachangia katika ukuaji wa uchumi ni sekta zile za utalii, sekta za mawasiliano, madini na fedha. Kwa hiyo, sekta hizi haziwagusi Watanzania walio wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungekuza uchumi wetu kupitia kilimo, naamini Watanzania wengi tungekuwa tumewasaidia kwa kiasi kikubwa sana. Mheshimiwa Waziri ninakuomba hii hotuba ya Upinzani tafadhali naomba uisome vizuri. Siku za nyuma mlikuwa mnasema hawa Wapinzani wanakuja na vihotuba vyao vidogo vidogo, makaratasi mawili, matatu; wengine wakaiita toilet paper, wengine wakafanya mambo ya ajabu ajabu; leo tumekuja na hii bajeti ya Upinzani mbadala. Mnasema mbona mmeweka kubwa sana? Mnaandika thesis, sijui mnafanya nini? Ninyi watu hamwaminiki! Naomba Waziri tafadhali, tumia hii hotuba ya Upinzani, hii ina vitu vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamechukua takwimu; kwa mfano takwimu zile za utafiti uliofanywa na REPOA. Ule utafiti unasema kwamba tukikuza kilimo kuanzia asilimia nane hadi kumi tutakuwa tumekata umaskini kwa asilimia 50 ndani ya miaka mitatu. Yaani ndani ya miaka mitatu tukikuza Sekta ya Kilimo kwa asilimia nane hadi asilimia kumi, ndani ya miaka mitatu tutakuwa tumeondoa umaskini kwa Tanzania zaidi ya asilimia 50. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli Serikali hii ina nia njema naomba tafadhali chukueni bajeti hii ya Upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, naomba kwa kuwa kuna watu wamezungumza, nami naomba nichangie kidogo kuhusu suala hili la makinikia suala la madini. Naomba tujiulize adui yetu ni nani? Adui yetu ni mwekezaji? Adui yetu ni sheria zetu? Adui yetu ni nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, adui yetu ni sheria tulizozitunga; Sheria za Madini na Sheria za raslimali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, adui namba mbili ni yule aliyetunga sheria hizi ambaye ni Serikali yetu hii ya Chama cha Mapinduzi. Hii ndiyo iliyotunga sheria hizi. Huyu ndiyo adui. Leo ziko sheria mbalimbali na kuna watu hawasomi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba kuna watu ambao hawasomi. Ziko Sheria za Madini; ninayo Sheria ya Madini hapa ya mwaka 1997. Mwaka 1997 kulikuwa na sheria mbili ambazo zilifanyiwa marekebisho. Iko Sheria ya mwaka 1997 ya Madini ambayo ni ya Uwekezaji kwenye Madini, lakini kuna Sheria nyingine ya Madini ya mwaka 1997 ambayo hii Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Fedha ambayo ilifuta kodi kwa wawekezaji wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Serikali imeamua kufuta kodi kwa wawekezaji wa madini inawatwisha mzigo Watanzania maskini. Hii siyo sahihi kabisa. Leo madini yetu tunapata mrabaha wa asilimia nne, kuna watu walishangilia Sheria hizi mbaya zinapotungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa hata kuona Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wale aliowaita wezi, anawaita Ikulu, anasema hawa jamaa ni jasiri sana. Leo wale wezi wamekuwa jasiri, anasema ni wanaume, lakini kuna wenzetu Wabunge wako humu ndani akina Mheshimiwa Ngeleja na wengine akina Chenge na wengine amesema wasisafiri, hawa watu wamezuiliwa passport zao kusafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo anakuja mtu ambaye ulisema ni mwizi, unasema ni mwanaume. Kumbe ukiliibia Taifa hili kama wewe ni Mwekezaji kutoka nje wewe ni mwanaume. Naomba niseme tu kwamba...

TAARIFA . . .

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba huyu bwana nadhani mara nyingi sana vyombo vya habari hafuatilii; taarifa ya habari hasikilizi, magazeti hasomi, WhatsApp haangalii. Kwa hiyo, naikataa taarifa yake ambayo ni ya kijinga kabisa na ya kitoto. Siwezi kuipokea taarifa kama hiyo. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba nchi yetu ilipofika...

TAARIFA . . .

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia tujaribu kupitia Dispensary wote hata ambao hawajui kwamba Acacia na Barrick wame-share hisa. Naomba niendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili niliache niendelee sasa kwenye mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako Watanzania wengi waliofungwa kwa kuiba kuku, ng’ombe na vitu vingine, tukawaite wale tufanye nao negotiation pia basi. Tuwaite Watanzania walioba tufanye nao negotiation. Kama tunasema huyu ni mwizi ,tukae mezani tufanye negotiation, tuwachukue na walioiba na wengine. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tu, kwamba haya mambo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze suala la mwisho; hilo la madini nadhani na wengine pia wamezungumza nitazungumza baadaye. Niseme tu kwamba kwa kweli bajeti hii imewasahau wafanyakazi wa Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Utumishi alisema kwamba mwaka huu anaajiri 56,000 lakini hatujaambiwa tarehe ya kuajiri ni lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, akiwa Mtumishi namba moja, leo hajaajiri, watu wamehitimu vyuo, hawaajiri kwa nini?