Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bismillah Rahman Rahim.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya mwanzo siku ya leo kuchangia hotuba iliyo mbele yetu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nami nitajikita zaidi katika ukurasa wa 10 - 12 katika hotuba yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze na historia fupi ili wale ambao wana mtazamo finyu waweze kuelewa historia ilisemaje au historia inasemaje. Nasema Taifa la Zanzibar lilianza miaka mingi sana, ni Taifa lenye historia ndefu na ilianza kabla hata ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo miaka 2,000 iliyopita. Ukitaka kuipima historia ya Zanzibar basi itakuchukua muda mrefu, lakini mimi nitaanza hapa kwenye karne ya 18 na 19 ambapo walio wengi wanaweza kukumbuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watakumbuka kwamba Zanzibar ilikuwa ni center ya biashara kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, Zanzibar ilikuwa ni Taifa lenye Mabalozi wake miaka hiyo lakini Zanzibar ilikuwa na mfumo madhubuti wa kiuchumi na kiulinzi. Kwa hiyo, Zanzibar lilikuwa Taifa kubwa na litaendelea kuwa Taifa, historia inasema hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwarejeshe kidogo waelewe ninaposema kwamba Zanzibar lilikuwa Taifa na lilikuwa na nguvu za kijeshi na kiuchumi. Zanzibar katika karne ya 18 ilikuwa tayari ina jeshi lake kubwa na ina manuwari za kivita. Zanzibar ilikuwa na Jeshi la Ardhini lililokuwa linaongozwa na Jenerali Sir Lloyd William Matthews ambaye alifariki na kuzikwa Zanzibar na kaburi lake lipo pale pale Zanzibar na jeshi hilo lilikuwa linaitwa Blue Jacket.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kulikuwa na Jeshi la Baharini ambalo lilikuwa na manuwari kumi za kivita. Kulikuwa na manuwari inaitwa Liverpool ambayo ilitengenezwa India mwaka 1826 ikiwa ina uwezo wa kuchukua mabaharia 150 na mizinga 74 lakini kulikuwa na Prince Regency, Victoria, Shaalam, Coral lean, Rahman, Pied Montez, Mustapha, Atenamise na Crew. Zote hizi zilikuwa ni manuwari za kijeshi, katika karne ya 18, Zanzibar tayari ni nchi na ina vifaa kama hivyo vya kijeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Zanzibar ilikuwa na majemedari wa kivita ambao walipigana vita. Waliosoma historia wanaweza kukumbuka kwamba Zanzibar kulitokea vita baina ya kabila la Mazrui na mpaka kufikia Kisiwa cha Pemba kikatekwa, lakini majemedari hawa ni miongoni mwa majemedari waliopigana vita hiyo na kukikomboa Kisiwa cha Pemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na jemedari wa mwanzo Jenerali Mohamed Juma, Jemedari Khalef bin Nassor, Jenerali Mohamed bin Nassor, Jenerali Hamad bin Ahmed, Jenerali Abdallah Sleyum, Jenerali Khalid bin Said, Jenerali Nassor Sleyum, Jenerali Hemed Sleyum na Jenerali Jen Tagai. Wote hawa walikuwa ni majemedari wa kivita ambao walikuwa katika majeshi ya Taifa la Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiuchumi Zanzibar ilikuwa ni Taifa ambalo linajiendesha kibiashara. Mpaka karne ya 18 na 19 Zanzibar ilikuwa inaweza kufanya biashara zake na Bara Hindi, Uarabuni, Uchina, Japan na walikuwa na mikataba ya kibiashara katika nchi hizo. Kwa upande wa Afrika Mashariki na Kati Zanzibar ndiyo ilikuwa kitovu cha biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naileta historia hii ili tuelewe na kwamba Zanzibar wakati huo ilikuwa tayari na sarafu yake ikitumia sham, rupia, noti zake zenyewe shaba, pesa ya Mnyasa, blue butter, shanga, mtama pamoja na cowrie. Kwa hiyo, Zanzibar ilikuwa ni eneo kubwa la kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize wakati huo Tanganyika ilikuwa wapi? Hata hilo jina Tanganyika lilikuwa halipo. Tanganyika imezaliwa tarehe 4 Mei, 1885 na baada ya Mjerumani kuchukua eneo la maili 600 la eneo la Mrima. Kwa hiyo, hapo ndiyo jina Tanganyika likapatikana wakati huo Tanganyika jina halipo hawana hata ngarawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitaka kuyaeleza haya ili kuiweka historia sahihi. Nakuja sasa kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwenye ukurasa wa 11 hapa alipozungumza kwamba katika kutatua kero za Muungano vikao vimefanyika baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuweza kutatua changamoto katika masuala hayo hususani masuala ya fedha, biashara, ajira katika taasisi za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile akaendelea kwamba, wamekutana na kuzungumza katika sekta zinazohusu fedha, biashara, viwanda, uwekezaji, ujenzi, uchukuzi, maliasili na utalii. Kama haya yamezungumzwa na kero za muungano zimeanza karne na karne ni lipi ambalo limepatiwa ufumbuzi katika haya? Hakuna hata moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni juzi tu, Mawaziri na kamatio zao za viwanda wa Zanzibar na wa Tanganyika hapa, wamekutana wameshindwa kutatua tatizo la sukari. Kuna tani 460,000 Zanzibar za sukari zinataka kuuzwa, Serikali ya Muungano imekataa, lakini wakati inakataa kununua sukari ya Zanzibar Serikali hii inaenda kuagiza sukari Brazil. Ndugu zetu wa damu, ndugu zetu ambao tumeungana hawawezi kununua sukari kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wanaenda kununua sukari Brazil. Kisingizio eti ukinunua sukari ya Zanzibar wataagiza sukari kutoka nje na badala yake watachanganya wauze Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi hata kama ni hivyo, iwe kweli ni hivyo, kwani kuna ubaya gani kununua hiyo wakati unaangalia wewe ile marker price tu. Kama bei ya Brazil na bei ya Zanzibar ni sawa kuna ubaya gani? Lengo la hili si kweli kama hapa hotuba ilivyoeleza kwamba, wana nia ya kutatua, lakini lengo lake ni kuikandamiza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar isiwe na mapato yake ya ndani, hili ndio lengo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, mwangalie market price, kwanini usinunue sukari? Mbona sukari inayotengenezwa Mtibwa mnanunua wakati kile ni kiwanda vilevile ambacho kinatokana na kiwanda cha sukari cha Zanzibar? Sasa hii kwa nini mnunue? Mtoto halali, lakini mama haramu, kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lengo hapa la hii hakuna lengo la kutatua kero ya Muungano na lengo lake ni kuhakikisha kwamba, Zanzibar haipati mapato. Matokeo yake ni nini…

T A A R I F A . . .

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, mie Mwongozo wake wala siusikilizi kwa sababu, hata masuala ya biashara hajui, wala hiyo Zanzibar haijui, wala hajui chochote huyu, huyu aljununi fununu humu ndani humu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama suala sukari ya Zanzibar haiwatoshi Wazanzibari wenyewe anajuaje yeye? Zanzibar inatumia sukari tani ngapi? Usinipotezee muda, huna unalojua, unataka sifa wala Uwaziri hupewi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mheshimiwa Naibu Waziri nakuheshimu sana, unajua fedha hujui biashara. Kwa nini mnaagizia mitumba wakati mnazalisha pamba hapa Tanzania na inawatosha kuzalisha nyie? Njoo kwenye biashara tukufundishe biashara, wewe ni mtu wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema hata kama sisi tunaagiza sukari kutoka nje, tunaiuzia Tanganyika muangalie market price. Ikiwa market price ni sawa kwa nini msinunue Zanzibar mkanunue sukari Brazil wakati Zanzibar ipo imejaa kwenye ma-godown? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndio hoja yangu. Kwa hiyo, lengo ni kuikandamiza Zanzibar isipate mapato yake kiuchumi. Kwa hiyo, ajenda hii iliyozungumzwa hapa kwamba, mnakaa SMZ na SMT kuzungumzia kero za Muungano, halina ukweli wowote na lengo lake hii ni kuikandamiza Zanzibar isipate maendeleo kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake ni nini? Serikali ya Zanzibar sasa hivi ime-stuck na wanailazimisha ZRB kukusanya mapato ya milioni 200 kila mwezi kutoka kwenye vyombo vya moto tu, hivi Zanzibar kuna magari mangapi, vespa ngapi, pikipiki ngapi ambazo watatozwa faini wapate milioni 200? Matokeo yake kuwa na chombo cha moto Zanzibar sasa hivi ni laana. Ndugu zetu wa damu hawa kuinunua sukari ya Zanzibar hawataki ma-godown yamejaa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, amezungumzia hapa, katika ukurasa wa 17 na ukurasa wa 18 kwamba, Msajili wa Vyama anasimamia vizuri suala la demokrasia ya vyama vingi, ili iimarike. Siamini katika hili na ninaamini kama Msajili wa Vyama ndiye anayeuwa Vyama vya Siasa hapa Tanzania na hususan Vyama vya Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Msajili wa Vyama anaiandikia CHADEMA kwamba, wajieleze kwa nini asikifute kwa sababu wameandamana. Kwani kuandamana haramu kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa yeye badala ya kusimamia vyama vikaenda mbele yeye ndio anavikandamiza vyama, CHADEMA amewafanya hivyo, CUF amepandikiza mgogoro yeye mwenyewe, CUF haina mgogoro, yeye ndiye anayesababisha mgogoro huu. Yeye msajili alivyo mnafiki kamwandikia Katibu Mkuu kwamba, hatatoa ruzuku kwa sababu, ana mgogoro. Akamwandikia Ibrahim Lipumba kwamba, hatatoa ruzuku kwa sababu chama kina mgogoro.

M W O N G O Z O . . .

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, neno mnafiki, namuomba Mheshimiwa Waziri kama hajui arudi katika Biblia, arudi katika Qur-an, arudi katika tafsiri, neno unafiki maana yake ni nini. Arudi huko ataona, kama hajui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unafahamu vizuri maana ya unafiki, nitafsirie; mmoja kati ya alama za mnafiki ni anapoahidi asitekeleze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye hoja kwamba, Msajili huyu kamwandikia barua lipumba kwamba, hatatoa ruzuku kwa sababu chama kina mgogoro. Akamwandikia barua hiyohiyo Seif Sharrif Hamad kwamba, hatatoa ruzuku kwa sababu, chama kina mgogoro. Kwa nini leo msajili huyu anarudi anampa Ibrahim Lipumba zaidi ya bilioni 1.3 pesa za ruzuku wakati alishaandika kwa maandishi kama hatoi? Kama sio unafiki ni nini? Kaandika yeye mwenyewe, sasa hiyo ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hajengi siasa za vyama na badala yake anaua vyama na lazima tumwambie…

T A A R I F A . . .

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo siipokei kwa sababu, huyu yakuuluna maala yafaaluuna. Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa haipokelewi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokisema mimi ni kuandika barua yeye mwenyewe halafu akarudi akatoa pesa. Kama aliandikiwa barua kwa nini, asirudishe barua zake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye mwenyewe ndiye alisema; mimi nazungumzia hoja yake mwenyewe, maandishi yake mwenyewe.