Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Sabreena Hamza Sungura

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuweza kuchangia katika Bunge lako hili Tukufu. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kutupa afya na uhai na leo hii kuweza kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijielekeze kwenye mchango wangu kwenye mambo mbalimbali ambayo yameainishwa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu na ningeomba nianze na suala la kwanza kuanzia kwenye suala la Mahakama, lakini pia, mambo ya ndani, magereza na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa masikitiko yangu kwa kile ambacho nilikiona kimetokea Ijumaa iliyopita tukiwa Mahakamani Kisutu. Tulishuhudia kwamba, ile tunayoita miongoni mwa cardinal principle za Criminal Law kwamba, alignment to the Court kwa accused ama suspect inavunjwa waziwazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatarajia kabisa kwamba, mtuhumiwa ana haki ya kufikishwa Mahakamani kwa wakati, lakini kulikuwa kuna sababu mbalimbali ambazo tunaambiwa kwamba, magari yameharibika hivyo, wale watuhumiwa hawawezi kuletwa mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunakuwa tunavunja ile misingi ambayo tumejiwekea kwenye sheria. Kwamba tunategemea Jeshi la Magereza liweze kujipanga vizuri na liwe linafanya kazi kwa wakati na tusiwe na visingizio vidogovidogo, itakuwa inatuharibia sura ya Wizara, lakini na pia sura ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwenda moja kwa moja sasa kwenye Mahakama ya Mafisadi, ile ambayo inaitwa The Corruption Economic and Organised Crime, High Court Division. Tulisema mafisadi papa na wale ambao ni mafisadi size ya kati kwa makosa yatakayoanzia bilioni moja wanatakiwa wapelekwe pale, lakini kumekuwa kuna upungufu wa watu wanaopelekwa kwenye Mahakama ile kwa sababu, kuna watu ambao hawafikii kile kigezo cha bilioni moja kwa hiyo, wanakuwa hawana sifa ya kwenda Mahakamani pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, kama Mahakama ambayo tumeianzisha, tumeweka watendaji, tumeweka Majaji, tumeweka Maafisa wa Mahakama na maofisa wengine, inakuwa Mahakama ile tunaona kama haijiendeshi kwa makusudio ambayo yaliwekwa kwa sababu, watuhumiwa wanakuwa ni wachache sana. Hivyo, tungependa kuiomba Serikali iweze kupunguza kile kiwango kilichowekwa, ili watu wengi waweze kwenda kuchajiwa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna changamoto. Changamoto ya kupata report za Mkemia Mkuu wa Serikali, zimekuwa zinacheleweshwa sana, kitu ambacho kinasababisha watuhumiwa wengi kuweza kucheleweshwa kesi zao. Hata ukiangalia katika hotuba ya Kitabu chetu cha Waziri Mkuu, ukurasa wa 62, ukiangalia idadi ya kesi ambazo zilipelekwa Mahakamani na idadi ya kesi ambazo ziliamuliwa kwa kweli, zinaonekana ni chache sana, hivyo, kunakuwa kuna shida hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la pili ambalo ningependa kuchangia ni suala la kufungiwa kwa mabenki yetu. Nilikuwa Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji Mitaji ya Umma, tulishuhudia benki mbalimbali zikiwa zimefungiwa kwa kukosa mitaji. Hata hivyo, tunaangalia initial capital ya benki hizi ambazo wakati wanaanza ku-operate walianzisha kwa milioni 250, lakini wakapewa limit ndani ya miaka mitano waweze kufikia bilioni mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kilichotokea hapa ni kwamba, waendeshaji wa taasisi hizi za kibenki wameshindwa kufikia mitaji ile na kusababisha benki hizi kufungwa. Kwa hiyo, kwa akili ya harakaharaka hapa sisi tuko watu 360 humu ndani, hivi ni nani ambaye anaweza akapewa milioni 250 halafu akaambiwa azalishe mpaka bilioni mbili ndani ya miaka mitano?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaweza tukaona hapa kwamba, kuna changamoto kubwa sana na waathirika wa suala hili wanakuwa ni Watanzania ambao ni wafanyabiashara wa kawaida kabisa ambao wanaambiwa walipwe 1,500,000/= halafu wasubiri process ya insolvence mpaka itakapokamilika. Ukiangalia hata katika sheria process hii ndefu na inachukua muda mrefu sana. Kwa hiyo, tungejaribu kuyafikiria mabenki haya, ili pale tunapowawekea conditions za kujiendesha basi wawe na viwango ambavyo watafanya kazi na vitakuwa ni viwango stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kwenda kugusia suala la maji. Pale Kigoma Ujiji Manispaa kuna mradi mkubwa sana wa maji, lakini pia tuna changamoto ya umeme. Tuna pampu takribani 13, lakini mpaka sasa pampu zinazo-operate ni nne, pampu tisa zimekaa pembeni, changamoto kubwa ni umeme. Wakisema wa-operate pampu zote maana yake ni kwamba, shirika lile la maji litakuwa linajiendesha kihasara kwa sababu, utahitajika umeme ambao utakuwa ni 2.5 megawatt kwa mwezi, kiasi ambacho ni kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, the only solution ambayo tunaitegemea ni whether tuunganishwe na gridi ya taifa, ili ule mradi uweze ku-run ama Serikali iweze kutenga pesa kwa ajili ya kununua solar system, ili tuweze kupata maji safi na salama na watu waweze kupata maji kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, basi tungeomba Serikali ilifanyie mkazo suala hili kwa sababu, wananchi wetu wanaathirika sana, hususan wale wanaofanya ibada za asubuhi, mchana na usiku wanakuwa muda mwingi sana wanahitaji maji. Kwa hiyo, tukikosa maji kwa kweli, inakuwa ni kikwazo kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna changamoto ya maji katika Mji wetu wa Uvinza, kuna kituo cha afya kiko pale, mama mjamzito anapoenda kujifungua anatakiwa aende pale na dumu tano za maji, bila hivyo pale hupokelewi wala huzalishwi. Sasa kwenye mazingira kama haya tungeweza kuiomba Serikali, kwenye bajeti ya mwaka huu waweze kututengea kiasi kidogo cha pesa, ili angalau katika eneo lile la kituo cha afya kichimbwe kisima ambacho kitaondoa kero ya akinamama kuweza kwenda na madumu ya maji, ili waweze kupata huduma za kuzalishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, ningependa kujikita kwenye dawa za kulevya. Kwa kiasi fulani ningependa kuipongeza Serikali kwamba, suala hili kwa kiasi fulani linapungua, lakini bado tuna changamoto, vijana wakati unga unazuiliwa vijana wengi wame-diverge, wanatoka kwenye unga wanaingia kwenye ugoro kwa maana ya tumbaku, lakini pia na mirungi. Kwa hiyo, Serikali sasa na yenyewe ijaribu kuangalia kwamba, huu ugoro ambao vijana wengi wanatumia una madhara gani na kuweza kutoa elimu kwa umma ili kuweza kuzuwia hujuma kama hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, ningependa kuchangia kuhusiana na masuala mazima ya ardhi. Katika mradi unaoendelea wa upanuzi wa Airport ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ama ya Mkoa wa Kigoma kwa ujumla, kumekuwa kuna wakazi ambao wanakaa maeneo yale karibu na airport ambao kuna ambao walipata upungufu wa fidia, lakini pia, kuna wale ambao hawakulipwa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilikuja ikaahidi kwamba, itafanya malipo ya mwisho kwa wale ambao walipata fidia pungufu na wale ambao hawakulipwa kabisa wangekuwa included. Hata hivyo, mara baada ya malipo kubandikwa ilionekana waliopata fidia zile ni wale ambao walisahaulika na wale ambao walipata pungufu hawajaweza kupatiwa fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia kwenye Sheria zetu za Ardhi, yaani Sheria ya Land Acquisition Act, inataka pale Serikali ambapo inachukua ardhi ya wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali kwa manufaa ya umma, basi fidia stahiki na ya haki iweze kutolewa kwa wakati, ili wananchi wale waweze kujipanga na maisha mengine yaendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiomba Serikali wakati tunaenda kwenye Bunge hili la bajeti, tunaenda kupitisha bajeti mbalimbali za Wizara; ningeomba waweze kuwaangalia wale wananchi wote ambao walipata fidia pungufu kutokana na ujenzi wa airport unaoendelea waweze kulipwa fedha zile na shughuli mbalimbali ziweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala la ajira kwa vijana, kumekuwa kuna shida kubwa sana kwawenzetu wa bodaboda, lakini pia na Askari Polisi. Wiki tatu zilizopita nilishuhudia tukio ambalo ni la kusikitisha sana Dar-es-Salaam, maeneo ya Buguruni. Vijana wa bodaboda wakati wanaendesha bodaboda kwa jinsi ambavyo traffic wetu wamekuwa wakilenga kuwakamata na pale ambapo wanashindwa kufanikiwa kufikia vijana wale basi inafikia hata hatua traffic wanashika usukani ule wa mbele na kutaka kama kuugeuza hivi ili waweze kusimama wale vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea ni yule kijana alirushwa kutoka kwenye bodaboda kwenda mpaka barabarani na gari nyingine ikapita ikapitia kichwa moja kwa moja akapasuka na akafariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo yanasikitisha sana na vijana wengi nchi nzima wanalalamika, lazima tuwe na njia za staha ambazo zitatufanya tuweze kuwakamata hawa vijana hata pale wanapokosea lakini sio njia ambazo zinapelekea mpaka kwenye mauaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni changamoto na tungeomba wenzetu wa Mambo ya Ndani waweze kuona ni kwa jinsi gani wanaweza wakaongea na askari wetu polisi na kuwapa mafunzo kwamba lazima tufanye kazi kwenye njia ambayo itakuwa ni ya kibinadamu, lakini na njia ya staha ambayo haiwezi kupelekea vifo wala majeruhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye viwanda, nimeangalia mpango wa Serikali, nimeona kuna viwanda ambavyo vimeanzishwa na mashirika ya umma na taasisi nyingine takriban viwanda 110, lakini katika viwanda vyote hivyo vilivyoanzishwa kwenye mkoa wangu wa Kigoma sijaona kiwanda hata kimoja. Kwa hiyo ningependa kuishauri tena Serikali zipo sababu mbalimbali zinazopelekea mikoa ya pembezoni isiweze kupata viwanda uki-compare na Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani na Tanga. Sisi kwa sababu ya umbali tunapata…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.