Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Ally Seif Ungando

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nashukuru kwa kunipa nafasi hii nami nichangie. Kwanza awali ya yote nishukuru vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi hii kwa sababu sasa Kibiti tunalala usingizi. Hii ni kwa sababu Kibiti ilifikia muda hata mtu anayegonga mlango unamjua kipindi cha usiku unashindwa kwenda kufungua mlango, lakini nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimefanya kazi ipasavyo Kibiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuiomba Serikali yangu Tukufu kwamba iangalie sasa jinsi gani ya kuboresha maslahi ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Hii ni kwa sababu hawana nyumba za kuishi, vitendea kazi vyao magari machache kwa hiyo, naomba kila jitihada wapatiwe vyombo vyao ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kwa kuunga mkono hoja kwa sababu hotuba hii ya Waziri Mkuu kwa kweli imegusa maisha ya mtu wa hali ya chini kwa sababu ukiangalia katika sekta zote amezigusia kwa hiyo tuna kila sababu ya kumpongeza jinsi gani anavyofanya kazi na hii ndio kiu ya wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na afya, katika Wilaya ya Kibiti tunashukuru tumepata fedha ya kukarabati kituo kimoja cha afya Mbwela, lakini kila penye mafanikio hapakosi kuwa na changamoto bali tuna upungufu mkubwa wa watumishi katika sekta hii ya afya lakini tuna baadhi ya maboma wananchi walijitolea lakini bado hayajakamilika. Kwa hiyo, naomba mtuangalie kwa jicho la huruma wananchi wa Kibiti mtukamilishie maboma yetu ili yaweze kutoa huduma kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna upungufu mkubwa wa madawa katika vituo vyetu vya afya kwa sababu ule Mfuko wa CHF unachangia, lakini moja ya sera ya afya kama mama mjamzito, mtoto chini ya umri wa miaka mitano na mzee zaidi ya miaka sitini matibabu bure. Anapokwenda kwenye kituo kile cha afya inabidi apewe dawa kwa yule mwananchi ambaye anachangia. Kwa hiyo, tuombe Serikali nayo iongeze fungu katika kupeleka dawa katika Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo ndugu zetu na jamaa zetu ambao wanaishi na VVU. Tunafahamu kwamba unapoanza kutumia dawa za VVU lazima upate lishe bora, lakini familia nyingi ambazo hazina uwezo wa kupata lishe hii bora. Kwa hiyo, ningeomba Serikali iwaangalie kwa jicho la huruma watu hawa wenye makundi maalum, wapewe hata ruzuku ili waweze kupata lishe bora na wanapopata lishe bora wakati wa kutumia dawa hata ule uambukizi unapungua. Kwa hiyo, tusipofanya hivyo maana yake itakuwa maambukizi yanaendelea lakini tukiwapa lishe bora hata yale maambukizi yataweza kupungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wananchi wa Kibiti pato letu kubwa tunategemea kilimo na tuna kilimo cha aina mbili; tuna kilimo cha biashara na tuna kilimo cha mazao ya chakula. Mazao ya biashara tunategemea zao la korosho, sisi kule kwetu Kibiti korosho ndio dhahabu, ndio makinikia lakini zao hili la korosho linafanya vizuri lakini zipo baadhi ya changamoto ningeomba Wizara husika kwamba sasa watu wanasema kesi ya shamba inaishia shambani, tunaomba aje kule Kibiti yapo makandokando ili tumweleze makandokando hayo ili tuweze kuyamaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tushukuru kwamba sasa hivi tumepata miche ya korosho bure na kweli wananchi wa Kibiti tumepanda mikorosho mingi ambayo itafanya Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na kipenzi chetu Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo zao la ufuta, ningeomba Waziri mwenye dhamana kwamba sasa aangalie jinsi gani zao hili nalo liuzwe kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa sababu tumeona kwenye zao la korosho, stakabadhi ghalani kwamba mkulima anapata fedha nyingi zenye tija. Kwa hiyo, ningeomba basi na zao hili la ufuta nalo liuzwe kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo mwananchi mkulima anaweza akafaidika na zao lake hilo la ufuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna upungufu mkubwa wa Maafisa Ugani katika Wilaya yetu mpya ya Kibiti. Mbali na upungufu wa watumishi hao lakini tuna changamoto ya vifaa vya kutendea kazi vikiwemo pikipiki hata Ofisi zao hakuna ambapo sasa yule Afisa Ugani anashindwa kutimiza wajibu wake kwa kukosa vitendea kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu elimu, nashukuru Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwamba elimu bure, lakini kila penye mafanikio hapakosi kuwa na changamoto. Changamoto kubwa ambayo tuko nayo sisi wananchi wa Kibiti moja tuna upungufu wa Walimu, nyumba za Walimu, madawati na madarasa. Kwa hiyo, ningeomba sasa leo Serikali ituangalie kwa jicho la huruma sisi wananchi wa Kibiti basi ni kale kasungura kidogo na sio Kibiti mtupatie ili tuweze kufikisha lengo la wananchi wetu kupata elimu bure katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miundombinu, nafahamu kwamba tuna barabara yetu kubwa ambayo inatoka Bungu kwenda Nyamisati. Barabara hii inatumika na wananchi wa Wilaya mbili na ndugu/jirani yangu hapa Mheshimiwa Dau, Mbunge wa Mafia. Barabara hii kwa kweli ningeomba tuiangalie kwa jicho la huruma kwa sababu kipindi inaponyesha mvua inashindikana kupitika. Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kwamba barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, ningeomba sasa basi mtufikirie ili tuweze kupata barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami ili wananchi wa Mafia na Kibiti waweze kufaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ujenzi wa gati Nyamisati, nachelea kusema kwamba tatizo nini, kwa sababu tunaambiwa mkandarasi tayari ameshapatikana lakini mpaka leo ujenzi wa gati unashindwa kuendelezwa pale Nyamisati, wakati gati hii ya Nyamisati ikijengwa wananchi wa Mafia jirani zangu watafaidika, lakini na mie vilevile ambaye naishi katika Wilaya ya Kibiti (Nyamisati) nitafaidika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia gati lazima tupeleke kivuko cha kisasa kutoka Nyamisati kwenda Mafia kwamba usafiri unaotumika kwa kweli siku Mwenyezi Mungu anakileta mtihani wake nachelea kusema sijui kitatokea nini kwa sababu hali ya vivuko vyetu ambavyo wanavitumia sio salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo tuna matatizo ya maji katika Wilaya yetu ya Kibiti kwamba upatikanaji wa maji ni kama asilimia 38 tu na vijiji vingi havina maji lakini hata ile miradi ambayo tayari imekamilika bado inasua sua katika kutoa huduma yake kwa sababu tunafahamu maji sio biashara, maji ni huduma. Kwa hiyo niiombe Serikali itenge ruzuku kidogo ipeleke katika miradi ya maji ili iweze kukarabatiwa, ilipe gharama za bili za umeme na kuweza kulipa gharama za vibarua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo iko baadhi yake ni miradi mikongwe, ipo muda mrefu ambayo inatakiwa ifanyiwe ukarabati ili iweze kutoa huduma. Miradi hiyo ni kama wa Jaribu, Bungu, Nyamisati ambayo miradi hiyo yote ingefanyiwa ukarabati na miradi ya Lualuke, Mkenda na Muyuyu ingeweza kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanasema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Waziri wa Nishati namshukuru sana sasa hivi Kibiti suala lile la umeme kukatikakatika limekuwa historia maana Kibiti tulikuwa umeme kama indicator ya gari, unazima unawaka lakini sasa hivi Kibiti tuna umeme wa uhakika ambao tumeunganishwa na Gridi ya Taifa, kwa hiyo sisi kama wananchi wa Kibiti tuna kila sababu sasa ya kutumikia umeme huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ombi kwa Waziri mwenye dhamana kwamba sasa Kibiti tunaomba tupate na Ofisi ya TANESCO, kwa sababu kutoka Kibiti kwenda Ikwiriri kuna takribani kilometa 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.