Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuwa mchangiaji wa mwanzo jioni yetu ya leo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai wake nikaweza kusimama hapa na mimi kutoa mawazo yangu haya ambayo nitayatoa. Kabla ya yote nielezee tu kuridhika kwangu kwa jinsi unavyolisimamia vizuri Bunge hili. Kwa kweli shukrani sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza kabisa mimi leo nataka nianze na jambo moja ambalo ni kuhusu maswali tunayoleta Wabunge hapa Bungeni. Leo nataka nitumie fursa yangu hii ili kupitia Waziri husika anijibu maswali ambayo kuanzia Bunge la Kumi nikiwa Mbunge niliyapeleka kwenye Ofisi ya Maswali Bungeni sikupata majibu na katika Bunge hili tumekuwa na miaka miwili na nusu maswali hayo pia hayajajibiwa na mpaka sasa tamaa inakuwa ni ndogo. Hivyo naona ni bora nitumie fursa ya muda wangu huu wa kuchangia ili ikimpendeza na nimuombe Mheshimiwa Waziri wakati wa winding up ili anipe majibu ya mambo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewahi kuuliza swali hili na najua liko katika meza ya maswali, Serikali yetu inatumia vigezo gani kuitambua BAKWATA kuwa ndiyo chombo kikuu cha kuwasemea na chenye mamlaka ya uislamu wa Tanzania. Niliuliza hili swali, Serikali inatumia sheria ipi ili kuitambua BAKWATA kwamba ndiyo Baraza Kuu la Waislamu Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliuliza hili kwa kutambua kwamba Tanzania haina dini na waasisi wa Taifa letu waliweka hilo wazi ili kuepuka mambo makubwa yanayohusu kuingiliana mambo ya dini na kiutendaji wa Serikali. Niliuliza hili kwa sababu waislamu tuna taasisi nyingi kama zilivyo dini zingine. Kuna taasisi nyingi ambazo kwa mujibu wa sheria yetu ya kiislamu ambayo Serikali si juu yake kuingilia utendaji wetu waislamu, kila muislamu ana maamuzi kwa taasisi na Jumuiya anayoiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kusikitisha sana, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuitambua BAKWATA na kuipa mamlaka makubwa ikiwemo kusimamia hija za waislamu jambo ambalo si haki! Ikiendelea kusimamia mashtaka ya waislamu jambo ambalo pia si haki! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu madhehebu haya yanatofautiana na ni jukumu la Waislamu kujiamulia madhehebu wanayoyataka niliuliza hili ili Serikali ituweke wazi, kwanini mmetambua BAKWATA pekee kama ndiyo chombo kikuu cha waislamu Tanzania jambo ambalo haliko kwenye kitabu chetu kitukufu cha Qurani, Qurani haitambui BAKWATA, Qurani haitambui uamsho, Qurani inatambua waislamu na imani yao ya kiislamu. Haya maamuzi tumeyafanya wenyewe waislamu. Kama ambavyo wakristo wana taasisi zao wanazozitambua, haifai kwa Serikali kujiingiza kuitambua BAKWATA. BAKWATA iwaachie waislamu wafanye maamuzi kwa jumuiya. Kwa hivyo natoa wito kwa Serikali kuanzia sasa iache kuitambua BAKWATA kama ndiyo Baraza Kuu la Waislamu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema hilo sikujua kama siku moja hata Bunge letu litaingia kwenye mtego. Leo Bunge limewakaribisha BAKWATA kuweka mkutano wa mambo ya kiislamu ndani ya ukumbi wa Bunge hili, jambo ambalo leo hii kila taasisi ikitaka kupewa nafasi hiyo kwa sababu mmeanza kwa BAKWATA itakuwa tatizo, wengine hamtawapa. Kuna Wapentekoste watataka waje mle, Walokole, Walutheri, ndiyo kwa sababu mmeanza njia mbaya! Kuna Uamsho, ni jumuiya halali na mpaka leo nadhani ina usajili watataka kuja humu, kuna mabaniani wanaabudu ng’ombe wataingia na ng’ombe humu ndani waabudi baa baa! Mko tayari? Haya ni mambo ya kuyaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili niliuliza, Serikali wakati walipomtaka Komandoo Salmin Amour ajitoe katika uhusiano wa Jumuiya ya Kiislamu (OIC) ilitoa ahadi kwa Watanzania Serikali ya Jamhuri itaangalia namna bora ya kujiunga ili jambo hili liwe la Kimuungano, Jumuiya ya Kiislamu OIC. Ahadi hiyo watu wanaitambua na wawakilishi wao wanatukumbusha tuijulishe Serikali. Kama limewashinda bado Zanzibar kwa maslahi ya kiuchumi, sio ya kidini tunaomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano iachie Zanzibar ijiunge na Jumuiya hii kwa maslahi ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la tatu nililouliza ambalo sikupatiwa jibu. Niliuliza hivi; kulikuwa na utaratibu ambao sio wa kisheria lakini ulikuwa ni utamaduni mzuri. Viongozi wa Mataifa ya nje wanapokuja Tanzania wanapewa nafasi ya kuzuru Zanzibar na sisi Zanzibar tulikuwa tunapata nafasi ya viongozi wetu kuwaambia baadhi ya mambo yetu. Utamaduni huu umeondoka, mtuambie ni kwa nini. Hayo matatu ni maswali ambayo sikupata majibu 2010, naomba leo Mheshimiwa Waziri unijibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia suala la vikao vya Makamu wa Rais vinavyohusu kero ya Muungano. Nasikitika sana, kama kuna mambo ambayo nadhani kwa maoni yangu ni mambo ya aibu ni Wanamuungano wa Tanganyika na Zanzibar kukaa Makamu wa Rais na baadhi ya Mawaziri kujadili kero ambazo siku zote hazipatiwi muafaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hapa tumeshuhudia, Mheshimiwa Yussuf akizungumzia kuhusu sukari ya Zanzibar kuzuiwa kuingia Tanzania Bara. Suala hili limezungumzwa kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili wamekuja Mawaziri wamekaa na Mawaziri wenzao wa Bara na suala hili wawakilishi wa wananchi tumepewa tulisemee humu. Kwa hivyo, inapoonekana tunaposemea mambo ya Zanzibar wenzetu inawauma inabidi mvumilie sana kwa sababu kila kitu kina gharama zake. Leo nisingejibu hili lakini nimesikitishwa sana na Naibu Waziri wa Muungano kusimama na akajibu kwamba sukari ya Zanzibar haiwatoshi wenyewe Wanzanzibari, ni kidogo, iweje iletwe huku, jamani! Ni vingi vidogo Zanzibar lakini wananchi wa Bara mwavitumia! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viko vingi vidogo, hata humu Bungeni vimo vidogo vingi, lakini tunavitumia na wala hakuna ubaya ndugu zetu wa damu, wajomba kuvitumia vya Zanzibar kama sisi ambavyo hakuna ubaya kuvitumia vya Bara. Leo ajabu kubwa eti sukari ya Zanzibar inakuwa ni aibu kuingia Bara. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, leo hii Mheshimiwa Yussuf amesema pamba ya Tanzania haitoshi kutengeneza nguo lakini wazalishaji wa pamba wanaruhusiwa kuuza nje wakati tunaaagizia mitumba kuingia Tanzania, aibu iko wapi? Hapa linaloangaliwa na Mheshimiwa Yussuf amemuambia Naibu Waziri, tunazungumza biashara! Leo kiwanda kile kwa udogo wake na idadi ndogo inayozalisha mkikipa fursa ya kufaidi soko la Tanzania Bara kitajipanua na kuongeza ajira kwa Zanzibar. Ninyi kosa lenu mkiiona Zanzibar inaendelea, tatizo lenu nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali jana kupitia Waziri Mahiga alisema Zanzibar inafaidika na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kufaidika kuuza mazao yao katika Soko la Afrika Mashariki. Afrika Mashariki ipi tutaifikia ikiwa daraja la mwanzo ni Tanganyika hamtaki tuguse? Hebu niambieni, tutafika vipi Afrika Mashariki wakati ndugu zetu wa damu mnakataza bidhaa ya Zanzibar kuingia ndani ya Tanganyika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zetu wa damu ikitokea Tanzania ina vita, juzi tumepokea majeneza ya askari waliokufa kuiteteta heshima ya Taifa letu. Kati yao ilikuwa nusu kwa nusu tumepokea Zanzibar. Mimi binafsi akiwemo mmoja ndugu yangu wa damu. Tumepokea kwa kutetea maslahi ya Tanganyika na Zanzibar. Tanzania tunakuwa pamoja katika maumivu lakini katika kula mnatutupa, huu ni Muungano wa aina gani? Leo tukienda kutetea maslahi na heshima ya Taifa hili Wanzanzibari tunakufa pamoja na ninyi, lakini tukirudi hapa Mzanzibari kuchukua packet za sukari kuleta hapa mnasema tunatafuta njia ya kuleta magendo. Mnaidhalilisha Serikali ya Zanzibar kwamba Serikali nzima ya Zanzibar ni Serikali haramu inayofanya magendo. Hili jambo hatuwezi kukubali, binafsi kwa imani yangu simtambui Rais wa Zanzibar kama ni Rais halali, lakini natambua maslahi yanayokwenda Zanzibar kwa sababu yanasaidia wananchi wote wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani maziwa ya Zanzibar mmeyawekea vikwazo, maji ya Drop kutoka Zanzibar mmeyawekea vikwazo, kila kitu. Tulikuwa na Kiwanda cha Sigara Zanzibar mmekiua kwa vikwazo, leo mnaitakia nini Zanzibar? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyezi Mungu katika Qurani tukufu kuna sura inaitwa Suratul-Falaq amezungumzia namna ya uhasidi. Husda mbaya, kisiwa cha Zanzibar mnakiangalia kwa husda, haifai sisi ni ndugu wa damu. Leo hii hasidi huhusudi hata yule maiti kwa sanda aliyozikwa nayo. Hukaa akamwangalia; “hee, sanda yote nyeupe anazikwa nayo huyu” hasidi itamfaa nini sanda maiti na anazikwa? Inamfidia nini ndugu yangu? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu rekebisheni, tafadhalini, Muungano huu ni tunu ya Taifa letu, lakini niwaambieni tena kwamba kile kidogo cha Zanzibar mkiruhusu kifaidi soko la Afrika Mashariki, kifaidi soko la Tanzania Bara, vilindeni mna vyombo vya dola mna Polisi, mna TRA zote zilizoko Zanzibar ni za Muungano, msituambie sababu kwamba italetwa kwa magendo wakati mnajua mna vyombo vyote vinavyosimamia ni vyombo vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama Kiwanda cha Zanzibar kinazalisha packet 10,000 waacheni wafaidi soko la huku hata wanywaji wa Zanzibar hawafiki 1,000 lakini bia ya Tanganyika inawalewesha Wazanzibari. Wazanzibari hawana Kiwanda cha Bia, wakianguka kwa ulevi ni bia mliyotengeneza ninyi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo soko la nyanya limekuwa kubwa. Mwaka jana nyanya zilikuwa zinaliwa na ng’ombe. Mwaka huu sasa hivi kilo ya nyanya Zanzibar inafika shilingi 4,000. Mkulima wa Dumila hamuwezi kumzuia asipeleke Zanzibar kwa sababu hapa kwetu hazijatosha. Kwa nini iwe Zanzibar? Tunasema haya yanayofanyika siyo halali na sisi Wapinzani ndiyo tunaimarisha Muungano na ninyi wa Chama cha Mapinduzi kwa matendo yenu haya, uhasidi huu, hamuusaidii Muungano wetu. Tafadhalini sana msimchore Makamu wa Rais.

Mheshimiwa Naibu Waziri wewe unafaa kuadhibiwa leo, kwa sababu kumbe ulijua haliwezekani kwanini unamuacha Makamu wa Rais anakaa vikao kujadili jambo ambalo wewe jibu unalo? Why? It’s a shame for you Mheshimiwa Naibu Waziri, ungemuambia Makamu wa Rais kwenye vikao vyenu vya cabinet kwamba hili unalotaka kulisimamia Makamu wa Rais ni jambo lisilowezekana, akaacha kuhangaika Mama wa watu tunamheshimu sana Mheshimiwa Samia, kwa nini? It’s a shame for all CCM. Kwaherini.