Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Martha Jachi Umbulla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja hii. Kwanza kabisa na mimi nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwa na afya njema na kuwa mahali hapa leo hii, na kwa moyo wa dhati nichukue fursa hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa hotuba nzuri na zaidi kwa mengi ambayo anawatayarishia Watanzania kupitia hotuba yake.
Mheshimwia Naibu Spika, wananchi wa Tanzania wamemuunga mkono sana Mheshimwia Rais kupitia hotuba yake na kwa hakika Tanzania nzima inampongeza, Afrika inampongeza na dunia inampongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais ameainisha maeneo mengi muhimu kwa maendeleo ya haraka ya nchi yetu. Vilevile ameainisha kero na malalamiko mengi sana ya Watanzania na baada ya kuainisha kupitia hotuba yake akatuletea sisi Wabunge wasaidizi wake ambao anatutarajia tuweze kumsaida katika kutatua kero hizo na malalamiko ya wananchi, alijua mahali pa kupeleka akijua kwamba Wabunge bila kujali kwamba ni wa chama gani wote ndiyo wananchi wanawategemea. Sasa kilichonishangaza mimi na kunisikitisha ni kujiuliza kwamba hivi wananchi wameiopokea na kuipongeza hotuba ya Rais na bila kujali itikadi. Amekwenda kila Jimbo akaainisha kero na malalamiko ya wananchi, sasa hawa wenzetu ambao hawakutaka kusikiliza hizi kero na malalamiko ya wananchi wanamwakilisha nani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningewaona mashujaa kama siku ile wangemsikiliza Mheshimiwa Rais, wakaona hotuba ile inasema nini na basi leo ama jana tulivyoanza kuchangia kwa kuona kwamba haiwafai basi wakatoka. Lakni tukashangaa wanaendelea kunga‟nga‟nia kujaribu kuchangia jambo ambalo hawakuweza kukubaliana naye. Lakini ya Mungu mengi niachie hapo.
Mheshimwia Naibu Spika, naomba nichangie kidogo sekta ya ardhi. Ardhi yetu imekuwa na thamani kubwa sana na inaendelea kuwa na thamani, tena kwa kasi kubwa sana, na hivyo kadri watu tunavyoongezeka na mifugo na mahitaji ya ardhi, kunakuwa na mahitaji makubwa ambayo ardhi inaendelea kuwa finyu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa mfano, kule kwetu Manyara kuna migogoro kila Wilaya na hasa kufuatia uhaba wa ardhi. Ukienda Wilaya ya Kiteto kuna migogoro, ukienda Wilaya ya Mbulu, ukienda Wilaya ya Hanang, ukienda Wilaya ya Babati, Simanjiro kote kuna migogoro kutokana na uhaba wa ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mapendekezo mazuri ya Mheshimwia Rais na maainisho yote ya kwenye framework ya mpango wa miaka mitano mimi naomba kutoa mawazo ya ziada. Nchi yetu tumejaliwa kuwa na mapori makubwa sana ambayo mengineyo yana-potential kubwa ya kuweza kuzalisha mazao na hasa kutumika kwa ufungaji. Sasa ninaomba kwa sababu wananchi wenyewe hawawezi kuyawezesha hayo mapori ili yaweze kutumika kwa kilimo na ufugaji, naiomba Serikali itenge bajeti ya maksudi kabisa, ili iweze kusaidia kuwezesha haya mapori makubwa ambayo ni potential yaweze kutumika kwa ajili ya kilimo na kwa ajili ya ufugaji na zaidi sana kwa ajili ya uwekezaji vilevile kwa sababu tunakwenda kwenye Tanzania ya viwanda.
Mheshimwia Naibu Spika, katika Mkoa wetu wa Manyara pia sasa hivi, kuna wimbi kubwa la wizi wa mifugo, wafugaji wanawaibia wakulima mifugo yao ikiwa ni njia mojawapo ya kuwafukuza wale wakulima ili waweze kuwaachia maeneo hayo waweze kuingiza mifugo yao. Sasa hii ni tabia inayopelekea mauaji, naiomba Serikali iweze kubuni ni namna gani wanaweza wakaikomesha hii tabia ya wizi wa mifugo ambayo pia inapelekea mauaji. Itakapotoa tamko ya kuhakisha kwamba Serikali imetoa tamko kuhakikisha kwamba inatoa adhabu kali kama fundisho wimbi hilo la wizi wa mifugo linaweza likapungua na wananchi watafanya shughuli zao kwa amani na utulivu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ya viwanda tunaiona na kwa hakika mimi nakubaliana nayo, viwanda vitajenga uchumi wetu kwa haraka na kuongeza Pato letu la Taifa. Ninakubaliana na mapendekezo yote yaliyopo kwenye Hotuba ya Rais wetu, lakini vilevile niombe kwamba Mkoa wetu sisi wa Manyara ni maarufu sana kwa kilimo cha mazao hasa vitunguu swaumu. Najua vitunguu swaumu siyo zao lililozoeleka, niwahakikishie lina soko hata nje ya nchi. Ninaiomba Serikali wakati ukifika tuweze kufikiria kuweka kiwanda katika Mkoa wetu wa Manyara hususani Wilaya ya Mbulu ambapo tunalima kwa wingi sana zao hili ambalo kwa sasa hivi soko lake halina uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo kuhusu matumizi ya shilingi milioni 50 alizoahidi Rais wetu. Tuna mifano mingi sana ya fedha za aina hiyo ikiwepo mabilioni ya Kikwete ambayo tuliyasikia kipindi kilichopita, lakini vilevile asilimia 10 ya fedha zinazotengwa na Halmashauri kwa ajili ya vikundi vya wanawake na vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi kwa bahati mbaya hazikuwekewa mfumo mzuri ambao ungeweza kuwafikia walengwa. Ninaiomba Serikali itakapofikia wakati huo wa kutupa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji na hasa kwa kuwawezesha wanawake na vijana na makundi mengine. Tuangalie isije ikaenda kwenye mfumo huo huo wa upotevu bali tuiwekee utaratibu mahsusi, bila haraka yoyote kuhakikisha kwamba kunakuwa na taaluma ya kutosha ili fedha hizi ziweze kuwafikia walengwa waweze kufanya kazi iliyokusudiwa na hivyo kufikisha dhamira ya Rais iliyo njema ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo waweze kufanya kazi yao kwa urahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa na haya machache naunga mkono hoja na naendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa juhudi kubwa anayoiweka katika kuliongoza Taifa letu, ahsante sana. (Makofi)