Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuungana na wenzangu kuweza kuchangia katika hoja hizi mbili Ofisi ya TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote aliyenipa fursa ya kuweza kusisimama na kuweza kuchangia katika Bunge lako Tukufu. Nitoe pole sana kwa wananchi wenzetu Afrika Kusini kwa kuondokewa na muasisi wetu mama Winnie Mandela. Naomba niungane nao sisi Chama cha Mapinduzi tumepeleka mwakilishi na UWT tumepeleka mwakilishi, tunaomba tuungane nao na Mwenyezi Mungu ampoke na amlaze mahala pema peponi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na timu yake yote ya Serikali yake kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ya kutekeleza Ilani ya CCM kiasi kwamba hata tukifanya uchaguzi hata hizi ndogo zilizopita Chama cha Mapinduzi kinaibuka na ushindi mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni dalili tosha kwamba hata kura zingepigwa leo za Mheshimiwa Rais na hata kura zingepigwa leo za Wheshimiwa Wabunge na hata kura zingepigwa leo za Serikali za Mitaa na hata Madiwani Chama cha Mapinduzi kingepata ushindi wa asilimia 100 kwa sababu wananchi wana imani nacho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kumtia moyo Mheshimiwa Rais kuwatia moyo Waheshimiwa Mawaziri wote na hasa TAMISEMI na Utumishi waendelee kuchapa kazi na sisi wanawake wa Tanzania tuko nyuma yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada ya utangulizi huo, naomba sasa nijielekeze katika mambo machache niliyoyachagua kuyatilia mkazo. Hapa nitaanza na kwa kweli kuipongeza Ofisi ya TAMISEMI chini ya kijana wetu shupavu Mheshimiwa Jafo kwa kazi nzuri sana waliofanya ya kudhibiti matumizi ya fedha na mapato yake. Kwa mujibu wa taarifa ya mkaguzi wa hesabu za Serikali inaonesha kwamba kwa halmashauri zilizokaguliwa 166 halmashauri zimepata hati safi zaidi asilimia 90. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mkombozi mkubwa sana kwa sababu nilikuwa mjumbe wa Kamati ya LAAC tulikuwa tukiona madudu mengi katika halmashauri, matumizi ya fedha yalikuwa ni ya ovyo, watu walikuwa hawafuati kanuni za fedha, fedha zilikuwa zinaibiwa, lakini kwa usimamizi wa Mheshimiwa Waziri na wenzake kuwa makini naona sasa matokeo mazuri yanakuja. Ni matumaini yangu sasa hata fedha zitakazokaguliwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018 tutapata asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze mpango wa kukusanya mapato ni ukweli usiopingika kiwango kimeongezeka, lakini niseme ukweli bado hakijawa cha kuridhisha. Ni asilimia 50 tu ya mapato yote yaliyokusanywa katika halmashauri, lakini unasikiliza huku Wakurugenzi kilio kingi wanazungumzia sijui mazao, mara tulikosa mvua, mara tulikosa nini, nataka niishauri Serikali hebu Ofisi ya TAMISEMI waweke mkakati na waelekezwe Wakurugenzi waje na mawazo mapya ya kukusanya mapato, wasiendelee kutumia vyanzo vya zamani vya kutegemea kilimo peke yake, wajaribu kuwa wabunifu watafute vyanzo vipya vya mapato na Serikali kuu iwasaidie kuwekeza katika miradi ya kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwenye uvuvi tuwekeze katika suala zima la uvuvi, kwenye kilimo tuhakikishe mazao yetu yanapata masoko, mazao yetu yananunuliwa , pembejeo zinawahi ili mapato ya nchi yetu yaweze kuimarika na tuachane na tatizo la Serikali za Mitaa kuwa ni tegemezi kwa Serikali Kuu. Najua Wakurugenzi wakipewa maelekezo kwa Madiwani tulionao na wenyeviti wetu wa halmashauli wakithubutu najua inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Mfuko wa Wanawake na Vijana. Naomba nichukue nafasi hii kupongeza Serikali kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Wakurugenzi, Madiwani na Wenyeviti wa Halmashauri kwa kweli wameonesha kabisa tulikadiria kutenga bilioni 60, fedha zilizotolewa ni bilioni 15. Hali siyo nzuri, nazungumza kwa sababu nina uhakika nilikuwa kwenye Kamati ya LAAC kila halmashauri wanaokuja wakuja na maneno matupu, fedha haipelekwi, unaona zimepelekwa bilioni 15 peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukienda kwenye uhalisia, hawaji na vikundi ambavyo vinathibitisha kweli wamepata hizi fedha. Kila siku tukiuliza hapa maswali, Serikali iko kwenye mkakati, tumejipanga, tutahakikisha tunaelekeza, leo nataka nimwone Mheshimiwa Waziri Jafo, atakapokuja kuhitimisha hotuba yake atuambie sheria hii inaletwa lini katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu jambo hili, sio la leo, taarifa ya Mwenyekiti Mheshimiwa Ngombale kwa awamu zote tangu tumeingia kwenye Kamati ya LAAC amekuwa akizungumza na hii taarifa ambayo Mheshimiwa Waziri ametuletea imesema kwamba Serikali ije na sheria, hansard zote nimezitafuta tangu 2010, vitabu vyote hivi leo nimevibeba ninavyo, Kamati ya Bunge ya mzee Zungu na wengine na mpaka ameingia Mheshimiwa Rweikiza na hata jana wameendelea kushauri namna ya kuleta hii sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumechoka na kusikia kwamba tuko kwenye mkakati, kutengeneza mipango, tunataka kusika sasa sheria inaletwa lini hapa Bungeni. Leo nitangaze rasmi kabisa hapa, Mheshimiwa Waziri namheshimu sana, ni mwanangu, nimemlea mwenyewe, nimemtengeneza mwenyewe mpaka hapo alipofika na namjua uwezo wake wa kazi. Nataka nimtangazie rasmi kabisa kwamba kama haji na hii sheria hoja yake sikubaliani nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu Mfuko wa asilimia kumi ya wanawake na vijana ndiyo Mfuko pekee uliowekwa kwa ajili ya kuwakomboa wanawake wanyonge, hawa wanawake walio vijijini hawana fursa ya kufikia mabenki ambayo yana riba kubwa, mashirika mengine hawayawezi kabisa wanawafanyia wao kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Mfuko uliwekwa kwa ajili ya kuwakomboa wanyonge. Nimemsikia amekuja na mkakati wa kuwasamehe riba, lakini tunataka kusikia hii sheria inaletwa lini. Kwa kweli nitawaomba na nitawashawishi Waheshimiwa Wabunge, atakapokuja wakati wa kupitisha vifungu kama haji na majibu kwa kweli mwanangu leo ajiandae kwamba mama yake sasa leo namkwamisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niiombe Serikali kuu huu Mfuko wa wanawake na vijana tukitegemea halmashauri peke yake hazitafika popote. Kulikuwa na mfuko ambao Serikali Kuu ilikuwa inatenga, kila mwaka zinapelekwa kwenye halmashauri kuongezea nguvu, lakini miaka mitatu hii mfululizo hakuna kinachotengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunataka leo pia tusikie Serikali ina mkakati gani wa kupeleka hizi fedha kwenye halmashauri kuongezea katika mfuko. Kwa sababu tukitegemea halmashauri zetu na halmashauri zingine ziko hoi kabisa na zingine mapato yake hayatoshi, lakini matumizi yake wakati mwingine yanakuja ya dharura, naomba leo Serikali ituambie huu Mfuko wetu uliokuwepo miaka nenda rudi ukaja ukaondoka katika miaka hii miwili, unarudi lini ili fedha ziende kusaidia wanawake na vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie sekta ya afya na hapa nichukue nafasi hii kwa kweli kumpongeza Mheshimiwa Waziri Jafo na timu yake yote, Waziri mwenyewe na Naibu Waziri, Katibu Mkuu Iyombe na Naibu Katibu Mkuu mama Chaula, naomba nimtaje kabisa kwa jina huyu mama kwa kweli amenishangaza. Sekta ya afya wanafanya kazi vizuri sana katika kitengo hicho, wamepeleka fedha kwa ajili ya kujenga vituo 48 nchi nzima, wamepeleka fedha za kutosha na nimeshavitembelea hivyo vituo, nimeviona, juzi nilikuwa Makete, nikaenda Nyasa nimekwenda kuangalia mwenyewe kushuhudia kama kweli kazi imepelekwa. (Makofi)

Mhshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza sana kwa hii kazi na wananchi wamenituma wanasema ahsanteni sana kwa sababu sekta ya afya ni ukombozi. Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya Waziri tunaona kabisa tuna kata zaidi ya 4000 lakini vituo vilivyopo havifiki hapa 600, lakini nimekwenda mbali zaidi nimekwenda kufanya research katika Ofisi ya TAMISEMI wamenipa kitabu hiki chenye mpango mkakati wa mipango yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaona kabisa sekta ya afya ni eneo muhimu sana, vituo vilivyopo havitoshi kuhudumia wananchi. Kwenye Ilani ya CCM tumejielekeza kupeleka kituo cha afya kila kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kuomba sana na nimeona mipango ya TAMISEMI wamenipa, hapo wanachohitaji TAMISEMI ni fedha, wanahitaji fedha kwa ajili ya kwenda kujenga vituo vya afya, wanahitaji fedha kwa ajili ya kujenga zahanati, wanahitaji fedha kwa ajili ya kujenga hospitali za Wilaya, lakini wanahitaji fedha kwa ajili ya kumalizia maboma, ambayo yalijengwa na wananchi yako zaidi ya 1800. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nguvu za wananchi zimeishia hapa. Nilimsikia juzi Mheshimiwa Ntimizi anasema yeye amejenga karibu vituo kumi na kitu kwenye kata yake. Nimekwenda juzi Wilaya ya Njombe nimeona. Naomba sasa Serikali na bahati nzuri Ofisi ya TAMISEMI wameshatengeneza mchanganuo kwa kila eneo wanakohitaji fedha wametengeneza wanahitaji fedha katika sekta ya afya kiasi gani, wanahitaji fedha katika hospitali ya Wilaya kiasi gani na katika halmashauri. Tunaomba fedha hizi ziende ili wananchi waweze kupatiwa vituo vya afya na hospitali kwa ajili ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie upande wa Utumishi, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana mzee wetu mzee Mkuchika kwa kazi mzuri wanayoifanya ya kuhakikisha sekta ya uchumi inaleta maendeleo katika Taifa letu. Kwa kweli ni ukweli usiopingika wafanyakazi sasa hivi wanafanya kazi tofauti na zamani, watu walikuwa wakiingia Ofisini kuangalia mitandao, kupiga simu, kwenda kunywa chai, lakini sasa hivi kumekuwepo na nidhamu ya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwapongeza, lakini ni ukweli usiopingika wafanyakazi wa nchi hii na wenyewe wanafanya kazi katika mazingira magumu. Kuna posho zao za kujikimu katika masaa ya ziada ya kazi, manesi wetu wanafanya kazi usiku na mchana Madaktari, wafanyakazi wetu katika Taasisi mbalimbali, Walimu wana madai yao huko, lakini wanafanya kazi kwa weledi, wanafanya kwa moyo na wanafanya kazi kwa uzalendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba katika bajeti inayokuja hii hebu tuwatengee fedha katika kulipa madeni tulipe na madeni ya wafanyakazi wetu ili waendelee kuwa na hali na kuendelea kuiamini Serikali yao na waendelee kuchapa kazi. Kwa kweli hapa naomba tuangalie sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la upungufu wa wafanyakzi, sekta ya afya peke yake wafanyakazi kwa upande wa TAMISEMI 66,000, upungufu huo kwenye zahanati kwenye vituo vya afya kila mahali na sijakwenda sekta zingine upungufu wa Walimu hasa wa sayansi na wa hesabu, pia Walimu wa shule za awali hawapo. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa hebu atuambie katika hawa wafanyakazi milioni hamsini mnaosema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)