Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Eng. Joel Makanyaga Mwaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chilonwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hotuba mbili za Mawaziri wa Wizara ya TAMISEMI pamoja na Utawala Bora ambazo zimewasilishwa hapa jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninampongeza Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, kwa utendaji wake mzuri. Tunashuhudia sasa tuna miaka miwili na nusu tangu ameingia madarakani na tuliona mwanzo kabisa alipoanza watu tulifika mahali tukafikiri kwamba hii ni nguvu ya soda, lakini tunadhihirisha muda unavyokwenda nguvu hii inazidi kuwa kubwa zaidi. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili nichukue fursa hii kuwapongeza Mawaziri husika wa Wizara ya TAMISEMI pamoja na Utawala Bora, Mheshimiwa Jafo pamoja na Naibu Mawaziri wako, pia kwa Mheshimiwa Kepteni Mkuchika, mmedhihirisha kwamba ninyi ni hodari na kwamba Mheshimiwa Rais hakukosea kuwateua katika nafasi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia kwanza kabisa suala la utawala bora, wachangiaji walio wengi wamejaribu kuchangia, nami nataka niguse sehemu ambayo naona kama haijapewa uzito unaostahili. Katika suala la utawala bora vipo vigezo vingi vinavyotumika kusema hapa kuna utawala bora wengi wamevizungumza hivyo, lakini mimi nizungumzie suala la kuwa msikivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuwa kiongozi bora kama wewe siyo msikivu, lazima uwasikilize wenzako, lazima uwasikilize walio chini yako wanasema nini ili utoke hapo ujue namna gani ya kuifanya kazi yako iende vizuri. Katika hili niwe wa kushuhudia katika hili pamoja na Wabunge mliomo ndani humu, kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano ni sikivu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nipo kwenye Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, tulikuwa watu wa kwanza wakati tumeanza kujadili hizi bajeti kwenye Kamati zetu, tarehe 19 Machi ndipo tulianza kujadili hizi bajeti na siku hiyo tulikuwa tunajadili bajeti ya Utawala Bora. Wajumbe wa Kamati walilizungumzia kwa kina sana na kwa uchungu sana suala la watumishi walioachishwa kazi kutokana na kigezo cha kutokuwa na elimu ya kidato cha nne na tunashukuru Mheshimiwa Waziri alilichukua na akasema atalifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama vile haitoshi, tarehe 4 Aprili tulianza vikao vya Bajeti hapa ndani na Wabunge humu ndani wamechangia kwa nguvu sana, kwa uchungu sana, suala hili la watumishi walioachishwa kazi kwa kutokuwa na elimu ya kidato cha nne. Tarehe 9 Aprili nataka muone jinsi gani Serikali yetu ni sikivu Mheshimiwa Waziri, Kepteni Mkuchika, amesimama hapo mbele na kutoa tamko ambalo tunalijua sisi sote. Tuseme nini sasa kama siyo usikivu wa Serikali. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa msemaji anayeendelea kuongea sasa hivi kwamba hata hao watu ambao walifukuzwa kwenye kazi walifukuzwa na Serikali ile ile ambayo imewarudisha. Kwa hiyo, hakuna usikivu wowote kwa sababu wangetaka kusikia wasingewafukuza toka mwanzo, siyo wanasubiri waondoke halafu wawarudishe tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Sina haja ya kusikiliza ushauri huo kwa sababu unaposema mtu msikivu ni baada ya kupewa ushauri. Bunge tunafanya kazi gani humu ndani, kazi yetu ni kuishauri Serikali. Baada ya kuwa yametendeka mambo ambayo hayako vizuri tumefanya kazi yetu ya kuishauri Serikali na Serikali imesikia, imetekeleza, tuseme nini sasa? (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa yake lakini kwa angalizo, naipokea. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee upande wa TAMISEMI, katika kuzichambua bajeti za Wizara hizi mbili, jambo lililojitokeza la wazi ni kwamba upelekaji wa fedha za maendeleo kwenye Halmashauri zetu ni mdogo sana unasuasua, jambo hili linafanya miradi yetu ya maendeleo kwenye Halmashauri haiendi katika kasi tunayoitarajia. Sambamba na hilo, ilijidhihirisha pia suala zima la ukusanyaji wa mapato ya ndani kwenye Halmashauri zetu pia linasuasua, haya mambo yote yanachangia kufanya miradi yetu ya maendeleo kusuasua katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naomba nizungumze suala moja, ninaiomba sana TAMISEMI, pale Halmashauri zinapokuja zinahitaji ushauri basi maamuzi yawe yanatoka mapema ili kama kunahitajika kuchukua plan B Halmashauri ziweze kuchukua na kusonga mbele na masuala ya maendeleo. Katika hili nitoe mfano mmoja kwa Mheshimiwa Jafo, Waziri wa TAMISEMI, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino imekuwa na matatizo ya ulipaji fidia kwa viwanja vilivyopimwa katika maeneo ya Buigiri na maeneo ya Aneti, pesa imekosekana ya kulipa fidia, Halmashauri imekuwa ikijaribu kupata hela kutoka sehemu mbalimbali bila mafanikio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya mwisho tumeandika barua kama Halmashauri, imekuja ofisini TAMISEMI kwa maana ya kwamba watusaidie tupate mkopo ili tuweze kulipa fidia kwa wananchi na viwanja vile viweze kugaiwa. Viwanja hivi vikigaiwa ni chanzo cha kuleta maendeleo, watu watajenga na kodi zitakusanywa, mapato ya ndani yataongezeka na miradi ya maendeleo itatekelezeka. Ninaomba sana katika hili Mheshimiwa Waziri uliangalie kwa karibu kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ninapenda nizungumizie ni suala zima la elimu. Tunalia sana na masuala ya elimu na hasa tunalia ukosefu wa walimu, sehemu kubwa tunalia walimu wa sayansi mashuleni. Jambo hili pia liko mezani kwako Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI. Kuna walimu wa sayansi ambao walikuwa form six, lakini wamesoma wamemaliza wamepata degrees zao mpaka sasa wana miaka mitatu wanafanya kazi hawajarekebishiwa mishahara yao, wanateseka sana lakini pia wanavunjwa mioyo katika utekelezaji wao wa kazi. Tunaomba haya mambo yafanyike kwa haraka ile watu waweze kufanya kazi kwa moyo mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuishukuru sana TAMISEMI, walitupatia kama Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino shilingi milioni 500 kwa ajili ya kukarabati kituo cha afya pale Chamwino, pia walitupatia shilingi milioni 400 zilienda kwa Ndugu yangu Mheshimiwa Livingstone Joseph Lusinde kule Jimbo la Mtera kukarabati zahanati. Kama vile hiyo haitoshi pia wametupatia shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Chamwino, tunasema ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache, naomba kuunga mkono hoja.