Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi jioni ya leo niweze kuchangia hotuba hizi mbili za Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia nitakuwa mnyimi wa fadhila kama sitamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. Kabla sijawa Mbunge katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nilikuwa nafuatilia sana midahalo humu ndani, moja ya changamoto kubwa ilikuwa ni malalamiko kwamba Tanzania hii hatuna ndege, Tanzania hii hatuna rail way za kisasa, lakini Mheshimiwa Rais amethubuti kuhakikisha kwamba tunakuwa na rail way ya kisasa, amethubutu kuonesha kwamba tumenunua ndege kwa kweli lazima tumpongeze. Itakuwa ni jambo la kusikitisha sana kama hatasisima Mbunge katika Bunge hili bila kumsifia Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo machache sasa nianze mchango wangu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita zaidi kwa kuanza na TARURA (Mfuko wa Barabara Vijijini). Mimi nipongeze maamuzi ya Serikali kuwa na TARURA, ni kweli kabisa kwamba TARURA imesaidia utengenezaji wa barabara zetu vijijini, lakini zipo changamoto mbalimbali ambazo mimi kama Mbunge sina budi kuzungumzia, wamezungumza wenzangu hapa kwamba TARURA inachangamoto ya fedha na mimi niseme kwamba tuone namna ambavyo tunaweza tukakaribisha mfumo wa TARURA, tuweke chombo ambacho kinaweza kuwa kinasimamia utekelezaji wa majukumu ya TARURA ili kile chombo kinaweza kufanya tathmini ya majukumu ya TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi tuone namna ambavyo TARURA wanaweza kuongezewa watumishi, natoa mfano katika Jimbo la Kilindi ambalo lina kilometa za mraba takribani 845.2, eneo hili ni kubwa sana, lakini tunalo gari moja, tu utaona kwa kiasi gani kwamba dhamira ya kuwa na TARURA inaweza isifanikiwe katika Jimbo langu la Kilindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto hii naiona ipo katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo tuangalie namna ambavyo tunaweza kuwaongezea TARURA vitendea kazi tuwaongezee staff.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitofautiane kidogo na wazungumzaji wengine kwamba tuone chombo hiki kiende kwa Waheshimiwa Madiwani hili sikubaliani nalo, kwa sababu TARURA iko katika maeneo yetu ya Majimbo. Mheshimiwa Diwani anaweza kumwona Meneja wa TARURA akamweleza barabara yake, hata Mheshimiwa Mbunge anaweza akazungumza jambo hili. Kwa hiyo, sioni umuhimu wa kuipeleka chombo hichi katika chombo cha Madiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni zahanati. Ninamshukuru Ndugu yangu Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo kwamba tumepata shilingi milioni 500 kwa ajili ya kituo chetu cha afya Songe, niseme wazi kabisa nilikuwa miongoni mwa watu ambao niliomba kuwa na Hospitali ya Wilaya, lakini kwa sababu nimepata shilingi milioni 500 na zimeweza kwa kiasi kikubwa tumejenga majengo naomba tuongezewe shilingi milioni 500 nyingine ili ikiwezekana tuweze kupandisha hadhi Kituo cha Songe iwe ni Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linakwenda sambamba na suala la watumishi. Watumishi imekuwa changamoto sana, tumeona juzi tu watumishi wengi wameondolewa. Ushauri wangu kwa Waziri wa TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utumishi tuone namna ambavyo tunaweza tukawaajiri watumishi wa kada ya chini, huko ndiko kwenye watendaji wengi sana tuone namna gani zoezi hili ambalo limepita na lile la nyuma tuweze kuhakikisha kwamba mapengo haya ambayo yapo maeneo mengi yanafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, katika Jimbo langu la Wilaya ya Kilindi tunaupungu wa walimu 589, sekondari walimu 135, kada ya afya 320. Kwa hiyo, utaona uhitaji huu uko kila sehemu. Ninakuomba Mzee wangu Waziri wa Ofisi ya Rais, Utumishi waangalie namna gani wanaweza kupitia mahitaji haya katika Halmashauri zetu ili tuone kwamba huduma zile za wananchi zinakwenda vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo mchango wangu mwingine utaenda kwenye suala la utawala bora. Imejitokeza changamoto katika maeneo mbalimbali watumishi wengi wanakaimu, hili limekuwa ni tatizo kubwa sana. Mimi nina uzoefu kwa sababu nimefanya kazi Serikalini, zamani ilikuwa kwamba Katibu Mkuu akistaafu unajua kabisa ni nani anayefuata kuwa Katibu Mkuu, Mkurugenzi akistaafu unajua ni nani anafuata kuwa Mkurugenzi. Hii succession plan sasa hivi katika Serikali haipo na hii ndiyo inasababisha kwamba unamteua mtu anakaimu unamfanyia upekuzi kwa muda mrefu kwa sababu humfahamu. (Makofi)

Ninakuomba Katibu Mkuu Dkt. Ndumbaro wakae chini walitafakari hili, utaratibu wa succession plan urudi ili tuwe na uhakika kwamba Katibu Mkuu leo akistaafu tunajua nani anayefuata, badala ya kwenda kuchukua hapa na hapa ma-gap haya yanakuwa ni ya muda mrefu sana. Haya kwa kiasi fulani yana zorotesha utendaji wa Serikali kuanzia Serikali Kuu mpaka Halmashauri. Jambo hili ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nirudi kwenye suala la huduma hizi za afya. Katika Jimbo langu la Wilaya ya Kilindi pamoja kwamba nimemsifia Mheshimiwa Waziri hapa kwamba amenipa shilingi milioni 500 kwa ajili ya Kituo cha Afya Songe, lakini vipo vituo mbalimbali katika Jimbo langu la Kilindi ambalo jiografia yake ni ngumu sana, nimuombe Mheshimiwa Selemani Jafo ikiwezekana zikipatikana fedha unitengee fedha kwenye vituo vifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Jaila ambacho kina takribani watu 20,000, Kituo cha Afya Kwediboma kina takribani watu 50,000 na Kituo cha Afya cha Negero, wananchi wangu pamoja na Mbunge wao tumeshaweka majengo yameshakuwa ni makubwa sana, tunahitaji fedha za kumalizia, nitashukuru sana Mheshimiwa Waziri kama utapata fursa ya kuja kwenye Jimbo langu na kutembelea maeneo haya kwa sababu wananchi wa Wilaya ya Kilindi bado wana changamoto ya afya. Najua dhamira ya Serikali ni nzuri ya kuwasogezea huduma ya afya lakini katika eneo langu la Wilaya ya Kilindi tulikuwa tunaomba sana sasa maeneo niliyoyataja yaweze kujengewa vituo vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nipongeze japo kuwa halijaja suala hili dhamira ya Serikali ya kuwa na mamlaka kama chombo kama cha TARURA cha maji vijijini, hii itasaidia kwa kiasi kikubwa sana. Ni juzi tu nimeuliza swali juu ya miradi ya maji katika Jimbo langu la Wilaya ya Kilindi, kuna mapungufu hapa ya usimamizi wa miradi ya maji. Naomba watu wa TAMISEMI na Wizara ya Maji wawe na Tume maalum wale na Kamati maalum ya kufuatilia miradi hii wasisubiri mpaka Wabunge tuje tuzungumze Bungeni hapa au CAG aandike ripoti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa inapopelekwa katika maeneo yetu tuhakikishe kwamba inafuatiliwa, kwa sababu unapokuwa umeleta mradi halafu mradi ule haujakidhi viwango, mradi ule haojatoa matokeo yanayotarajiwa maana yake wanaoathirika ni wananchi wa maeneo husika na Serikali hairudishi tena pesa inachukua muda mrefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa Waziri wa TAMISEMI na Naibu Mawaziri wake wote wanafanya kazi kubwa sana, kwa sababu wanafanya ziara za mara kwa mara, jambo hili ni jema sana kwa sababu linasaidia Waheshimiwa Mawaziri kujua changamoto katika maeneo yetu na hii linafanywa na Mawaziri wengine pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kusema kwamba naonga mkono hoja na ahsante sana.