Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia.

Nilikuwa namwomba Mheshimiwa Waziri wa Sheria afikirie upya na kuendelea kufanya ziara hasa kwenye Majimbo yetu yaliyoko kule vijijini. Tuna shida kubwa sana ya Mahakama, namaanisha majengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ni sehemu ambayo kila mtu anategemea akatendewe haki, lakini kweli Mahakama nyingine hata huyo hakimu kwenye kutenda haki inamuwia vigumu kutokana na mazingira yenyewe ya kufanyia kazi. Huwezi ukafanya kazi ya kuhukumu watu halafu umekaa kwenye jengo limejaa popo, unakwepana na mavi ya popo, halafu ukatenda haki sawa sawa. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri ajaribu kufanya ziara, aangalie hasa kule vijijini, tuna hali mbaya sana kuhusiana na majengo ya Mahakama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili, Mheshimiwa Waziri, Mahakama nyingi zimejaa mahabusu ambao kimsingi wengine wako mle tu kwa makosa ambayo yanastahili hata ungeleta amendment tukabadilisha sheria wakapigwa hata makofi tu wakarudi nyumbani. Kwa mfano, Gereza letu la Geita, capacity yake ni watu 141, lakini mpaka jana watu 750 wako ndani. Hii ni hali mbaya sana. Ukiangalia watu wengi walioko humo, wana kesi ndogo ndogo kuingia kwa jinai. Mtu ameingia tu labda eneo la mgodi, amekutwa karibu na ziwa kwenye maeneo ya hifadhi huko Rubondo; wamerundikwa wako mle.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, hebu jaribu kuangalia uwezekano, ikiwezekana hata kupanua Magereza, lakini ikiwezekana kujaribu kuleta tubadilishe hizo sheria makosa ambayo hayastahili mtu kuingia ndani, basi aachwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda nchi za wenzetu zilizoendelea, nakumbuka siku moja nilikuwa China, nilifanya kosa Hong Kong, nilivyokamatwa, nilikuwa na kosa tu, tumebishana tukataka kupigana ngumi na mwenzangu, lakini nilivyoitiwa oolisi, walikuja wakaniomba kitambulisho changu peke yake. Nilivyowapa kitambulisho, wakaniachia na mwenzangu wakamwachia. Siku ambayo tunataka kutoka, tulitozwa faini ya dola 5,000 pale pale immigration wakati wa kugongewa passport. Lakini Tanzania unakuta mtu anamwambia tu huyu amenitukana, huyu amenidhulumu, hata hawajahakikisha, mtu amerundikwa Magereza. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Mheshimiwa ukaze buti, lakini nikuhakikishie Mheshimiwa Kabudi unaenda sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilikuwa najaribu kuangalia michango, hata rafiki yangu Mheshimiwa Lema mwenye uzoefu kule Magerezani, anakushauri tu, ni mambo madogo madogo, ujaribu kuyarekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba sisi kama Waheshimiwa Wabunge ambao tunatunga hizi sheria, tuviache vyombo vifanye kazi. Haya mambo ya kuwa watu wanakuja humu wanasema nani kapotea, Beni Saanane, hata watu wa CCM wamechinjwa wengi tu. Kibiti wamechinjwa, hatujapiga kelele, tumevikabidhi vyombo vifanye kazi. Kwa hiyo, hata wale ambao mnasema wamepotea, polisi wanafanya kazi. Ukitaka kujua vizuri, acha kupiga kelele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona watu wanapiga kelele, tunaelekea kuzuri, kwa sababu kila siku tunaambiwa tufuate sheria bila shuruti, lakini watu wanajitokeza na viburi vyao.

Mhshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa kwenye kampeni ile ya Kinondoni. Tumepiga kampeni na hawa wenzangu, nani hajui kama mlikuwa mnasema watu waandamane mbebe majeneza 200? Ungekuwa wewe ni Serikali ungewaacha watu wanahamasisha watu wafe? Mimi nilikuwa nadhani tuviache vyombo vifanye kazi, nina hakika polisi na watu wengine wasitishwe na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi niliwekwa ndani, si nilikuwa na kosa, kuna shida gani? Ni vizuri hata Waheshimiwa Wabunge hawa wakorofi korofi wanapowekwa Magereza kule wanapewa fundisho.

Unamwona hata rafiki yangu Mheshimiwa Lema sasa hivi kidogo amekuwa binadamu! Tena nashukuru hata leo amenisalimia vizuri. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nimekuwa nikisikia mara nyingi sana wanapiga kelele kuhusiana na matamko ya Rais kwamba anavunja Katiba, lakini humu ndani kuna wasomi Wabunge, wanasahau kwamba Waheshimiwa Wabunge mnatunga sheria, lakini na tamko la Rais nalo ni sheria. Kwenye Katiba Ibara ya 37 inampa mamlaka Rais kusikia au kutokusikia ushauri. Sasa kama mnaona ni tatizo, leteni hoja humu ndani tubadilishe sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.