Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa nami kuchangia katika bajeti hii. Naomba nichukue fursa hii pia kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo naomba nichukue fursa hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na Watendaji wote kwa kuandaa hotuba hii. Naomba nichukue fursa hii pia kuipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Rais kwa kutoa kipaumbele kwa afya katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa 21 wa hotuba hii Serikali imebainisha ongezeko la maboresho ya vituo vya afya ili kuweza kutoa huduma za dharura. Pia naipongeza sana Serikali Ila napenda kufahamu, pamoja na kutoa huduma za dharura; je, Serikali imejipangaje kwa ajili ya kupata vifaa mbalimbali ikiwemo vifaa vya Ultra Sound, X-Ray sambamba na hilo pamoja na wataalam? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuipongeza Serikali kwa kujitahidi kuongeza uwezo kwa baadhi ya Watendaji wa Idara ya Afya. Naomba niishauri Serikali pia iweke mkakati wa muda mrefu wa kuweza kupata wataalam wa afya zaidi. Kwa sababu wenzangu wengi wamelizungumzia, tuna upungufu mkubwa sana wa wataalam wa afya.

Kwa hiyo, nilikuwa naomba niishauri Serikali, iandae mkakati wa muda mrefu wa kuhakikisha kwamba wanapatikana watendaji wa afya wengi zaidi kwa kupewa elimu na kutoa kipaumbele ili kusudi waweze kupatikana hawa Watendaji katika Idara ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Dodoma, pia na sisi tuna upungufu mkubwa sana wa rasilimali watu na tuna karibu 60%. Kwa hiyo, naomba nitoe shime kwa sababu Mkoa wa Dodoma ni Makao Makuu, hebu Serikali ione iiangalie Mkoa wa Dodoma kwa jicho la kipekee kwa kuwapatia watendaji. Naishukuru tena Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya katika baadhi ya Wilaya za Mkoa wa Dodoma ikiwemo Wilaya ya Chemba, Wilaya ya Chamwino, pamoja na Wilaya ya Bahi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Dodoma imeonekana kwamba kuna ongezeko sasa hivi la maambukizi ya VVU kutoka asilimia 2.9 mwaka 2014/2015 imekwenda kwenye ongezeko la 5% mwaka 2016/2017 wakati kiwango cha Kitaifa kimepungua kutoka asilimia 5.1 kwenda asilimia 4.7. Hii it is alarming kwamba kwa kuwa Dodoma ni Makao Makuu na watu wengi sasa wameanza kuja hapa, hebu Serikali ione umuhimu wa kuwa na mkakati kabambe wa kuhakikisha kwamba maambukizi haya hayaendelei tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda ni mfupi, naomba pia nizungumze kuhusu suala la ukatili ambalo linaendelea kwa kasi sana katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa 97 wa hotuba hii imebainisha kwamba matukio ya ukatili katika mwaka 2016 yalikuwa ni 31,996 wakati mwaka 2017 yamekuwa 41,416. Maana yake ni kwamba matukio ya ukatili yameongezeka kwa matukio 9,420. Hii kwa kweli siyo hali nzuri, ipo sababu sasa jamii pamoja na familia waone jinsi gani ya kulea watoto wetu katika malezi mazuri ili kusudi wasiwe na tabia ya ukatili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, nawaomba viongozi wa dini wajaribu kuendelea kuwahubiria wananchi wetu ili kusudi waweze kuwa na mioyo ya uwoga na kumwogopa Mungu ili kusudi kuweza kupunguza huu ukatili. Sambamba na hilo, nilikuwa naomba pia, Serikali ione jinsi gani itafanya kuzuia ukatili badala ya kutoa takwimu nyingi ambazo zinaendelea kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie pia Sera ya Wazee ya mwaka 2003, kwa kweli bado haijatungiwa sheria. Kwa hiyo, nilikuwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Naunga mkono hoja, ahsante.