Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Mwantum Dau Haji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia siku hii leo, Ijumaa ndiyo siku yangu adhimu aliyoniwekea kipindi hiki ili niweze kuchangia Wizara hii ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake.

Mheshimiwa Waziri, Mama Ummy, mwanangu nakushukuru sana na nakushukuru kwa jitihada zako unazozitendea Wizara hii ya Afya na ninakushukuru kwa jitahada zako kwamba umefika pia nami kunisaidia kufika Ocean Road kumpeleka ndugu na akapata uzima kuhusu cancer. Nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dakika zangu tano, kwanza niingie suala la ukatili dhidi ya watoto na wanawake nchini. Ukatili wa watoto na akina mama umezidi hapa nchini kwetu. Umezidi mno, umekithiri, maana yake sijui mtu afanye nini hasa! Nataka kuishauri Serikali, hili suala wasilitizame kwa jicho tu hivi, waangalie kwa kina ili hili suala la udhalilishaji wa watoto na akina mama lifanyiwe kazi ili liondoke katika nchi hii. Inawezekana kwa nchi yetu hii ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mama na mtoto katika kuimarisha huduma ya afya, lazima aimarishe kwa jitihada zake na uwezo wake ambao anao. Mama anakwenda hospitali hana mbele wala nyuma, ana mtoto wake anaumwa, pengine naye pia anaumwa, anakwenda pale, hana hata shilingi. Bima ya afya pia hana, anafika pale anaandikiwa madawa anakwenda akahangaike nje ili apate pesa zimsaidie mtoto. Kuimarisha huko ndiyo kunaendelea? Hakuna. Kwa hiyo, jitihada ya Serikali itazame vilevile kwa jicho la huruma mama na mtoto waweze kusaidiwa waweze kuimarisha afya zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee na uboreshaji wa huduma ya vituo vya afya; vituo vya huduma ya afya hapa nchini niseme Wizara imejitahidi sana, lakini kwa kuingilia ndani ukaitazama katika huduma zetu za afya ndani ya madaktari wengine wanakuwa madaktari, maana yake ni kama wanawanyanyasa wale wanaohitaji huduma, wanaokwenda pale kutibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu ashakwenda pale anaumwa, lakini daktari anajifanya kama yeye ni daktari, amesoma na uwezo wake, basi kumhudumia yule mtu aliyekwenda pale, mnyonge, maskini, anamnyanyapaa.

Anaona kama hakwenda mgonjwa pale. Anapiga simu au kama ana kikaratasi chake, anaendelea kusoma. Wengine utakuta wanachukua simu wanachapa zile karata katika ile simu, mna zile karata wanacheza. Mtu hajui huku kama kaja mgonjwa anaumwa amhudumie. Hilo limo katika vituo vyetu, nakuomba uliangalie kwa kina katika vituo vyako hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapokwenda kutembelea uangalie vizuri madaktari wetu. Sisemi kama hawafanyi vizuri, wanafanya vizuri, tumewapongeza humu sana, lakini suala hilo madaktari wengine wanafanya. Jitahidi katika kutembelea vituo vyako.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia, kuna ukurasa wa 14 aya 22 - afya na usafi wa mazingira. Kuna mazingira mengine katika vituo vyetu ambavyo tunakwenda kuingilia kama vituo vya mabasi, huduma za vyoo sio nzuri. Huduma ni mbaya, hazina usafi, utoke huku uende ukachukue maji uingize ndani ndipo uende ukafanye huduma yako.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Wizara izingatie suala hili na hivi vyoo vitembee hasa ili kwenda kutizama juu ya huduma zilizokuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja Wizara ya Afya. Ahsante sana.