Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Prof. Norman Adamson Sigalla King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kuwapongeza Mawaziri wenye dhamana, dada yangu Mheshimiwa Ummy pamoja na rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kwenye Wizara hii. Katika kufasili kwa usahihi matamshi na matarajio ya Rais wetu waliweza kuandaa kongamano au mkutano kwa ajili ya kupata wawekezaji tarehe 4 Aprili ambapo na mimi nilihudhuria, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka, jambo la kwanza, pamoja na jitihada nzuri za Serikali za kununua vifaa na hasa Hospitali zetu za Muhimbili pamoja na Mloganzila, naomba sana Serikali ijikite kusomesha madaktari hawa nje ya nchi, nasisitiza Madaktari Bingwa wasome nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi ya India kwa mfano na Hospitali zake za Apollo, idadi kubwa ya madaktari wake, actually asilimia 94 ya madaktari ambao tunawaona kwenye Hospitali za Apollo India, hawajasoma India. Kwa hiyo, ni muhimu sana na sisi tujenge uwezo kwa kufanya hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, ninaomba sana, pamoja na kwamba Serikali inaweza ikapata shida kwenye taulo za kike, lakini utafiti uliofanywa kwenye Wilaya ya Makete wanafunzi wa Wilaya ya Makete hasa darasa la sita na la saba na sekondari wengi wao ni yatima kwa sababu orphanage rate kwa maana ya Tanzania hii Makete tunaongoza. Wanahitaji kuangaliwa kipekee ili taulo za kike waweze kupewa watoto hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vituo vya afya; ninaipongeza Serikali kwa kazi nzuri ya vituo vya afya, lakini naomba sana Wilaya zile ikiwemo Makete, ambazo zina mtandao wa barabara au wa eneo kubwa zipewe upendeleo wa vituo vya afya. Kwa mfano, Tarafa ya Ukwama inahitaji kituo cha afya na gari la wagonjwa, Tarafa ya Bulongwa, vivyo hivyo Tarafa ya Ikuo, kitu cha afya na ambulance, kwa sababu inachukua karibu kilometa 105 kutoka kwenye kata hizi kwenda Makao Makuu ya Wilaya. Jambo hili likifanyika mtakuwa mmefasili kwa usahihi matatizo wanayoyapata wananchi wa Wilaya ya Makete na Watanzania wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, itoshe kusema tu kwamba kazi nzuri inayoendelea kufanywa sasa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi ya kuendelea kuongeza bajeti Wizara ya Afya ni kazi kubwa na nzuri ambayo wananchi wa Makete tutaendelea kuiunga mkono kwa nguvu zote. Na kwa hili, kipekee kabisa nimpongeze sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na timu ya wasaidizi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba niongelee kidogo Hospitali ya Misheni ya Ikonda. Makete tunayo Hospitali ya Ikonda, hospitali hii inahudumia mikoa takribani nane lakini Serikali inapaswa kutia jicho la kipekee na kuwapa ahueni na hasa malipo ya Madaktari Maalum ambao wanatoka Ujerumani na Italia kwa ajili ya kwenda kuhudumia wananchi wa Wilaya ya Makete na Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili, tumeandika barua mara nyingi kwa maana ya Hospitali ya Ikonda na mimi kama mwakilishi wao kwa Waziri kuomba favour na hasa ya madaktari hao, wasiwe wanatozwa fedha kwa sababu wanakuja kuhudumia Watanzania hawa na kwa kweli hata malipo yanayotozwa Watanzania kwenye hospitali hii ni malipo madogo sana. Niombe sana Waziri aweze kuiangalia Hospitali ya Ikonda ya Misheni kwa jicho la kipekee ili kuendelea kuwasaidia Watanzania zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia umealikwa Mheshimiwa Waziri ili utembelee Hospitali ya Ikonda ukajionee mwenyewe. Pale tuna kituo kikubwa cha viungo bandia ambavyo huwezi kupata eneo lingine lolote Tanzania hii, tunaomba sana utenge muda utembelee ili uone shida za wananchi wa Makete.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja, Mungu ibariki Serikali ya CCM.