Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Ummy kwa hotuba yake nzuri, nimpongeze Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara ya Afya. Nampongeza sana Mheshimiwa Ummy kwa sababu ni ukweli usiofichika kwa jinsi anavyofanya kazi kubwa ya kuhakikisha vifo vya akina mama na watoto vinamalizika, ninampongeza sana. Tumeendelea kuona anavyofanya kazi katika nchi yetu ya Tanzania, anavyofanya ziara katika maeneo mbalimbali, kwa kweli ziara zake anazozifanya zinazaa matunda, tunampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweza kushuhudia jinsi theatres zinavyojengwa, vituo vya afya, wodi za wazazi zinavyojengwa, sasa baada ya juhudi hizo kinachofuata sasa tunaomba ahakikishe wanapatikana wataalam wa kuweza kufanya shughuli hiyo ya kuwasaidia akina mama kwa sababu maeneo mengi hakuna madaktari, hakuna waganga wa upasuaji. Kwa hiyo, tunaomba wataalam hao baada ya kuwa theatres zimejengwa, baada ya kuwa wodi zimejengwa, waweze kupatikana wataalam wa upasuaji. Tusipofanya hivyo akina mama wengi watapoteza maisha kwa sababu maeneo hayo wasipopelekwa wataalam watakuwa wanafanya upasuaji watu wasiokuwa na ujuzi matokeo yake badala ya kunusuru maisha ya akina mama wataweza kufa kwa wingi.

Kwa hiyo, ninaiomba Serikali ihakikishe madaktari na wataalam wanapelekwa katika theatres hizo zinazojengwa pamoja na wodi hizo zinazojengwa.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nizungumzie Mkoa wa Kigoma; Mkoa wa Kigoma karibu asilimia 65 hatuna watumishi kabisa. Ninaomba basi kwa sababu muda mrefu Mkoa wa Kigoma kutokana na miundombinu haikuwa mizuri barabara tulikuwa hatuna, reli ilikuwa inasuasua, watumishi walikuwa wakipangiwa Kigoma hawaendi, lakini sasa baada ya Mkoa wa Kigoma kuanza kufunguka tunaomba wataalam waweze kupelekwa Kigoma ili tuweze kupata watumishi wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika Hospitali ya Kasulu tuna madaktari wanne na mahitaji ya madaktari ni 23, kwa hiyo tuna upungufu wa madaktari 19. Lakini wapo Madaktari Wasaidizi, mahitaji ni 35 lakini tunao wanne, pungufu 31 na ma-nurse pamoja na wauguzi kwa kweli hawatoshi, tunaomba mtusaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Kibondo kama nilivyoeleza wiki iliyopita wakati nauliza swali la nyongeza. Mkoa wetu wa Kigoma kuna wakimbizi, wakimbizi wanaotoka katika maeneo mbalimbali ya makambi ya wakimbizi wengine wanapelekwa katika Hospitali ya Kibondo, kwa hiyo, tunahitaji watumishi waweze kuongezwa katika Hospitali ya Kibondo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Kakonko ni Wilaya mpya hakuna Hospitali ya Wilaya na wagonjwa ni wengi kwa sababu Wilaya ile inapakana na Mkoa wa Kagera, wapo wagonjwa wengine wanaotoka mkoa wa jirani kuja kutibiwa katika kituo kile cha Kakonko, tunaomba Serikali ihakikishe Hospitali ya Wilaya ya Kakonko inamalizika haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hilo la hospitali lililopo Kibondo na Kakonko ni hivyohivyo. Katika Kituo cha Mtendeli cha Wakimbizi, wakimbizi wanatoka kuja kutibiwa katika Kituo cha Afya cha Kakonko, kwa hiyo, naiomba Serikali ihakikishe Hospitali ya Wilaya ya Kakonko inajengwa haraka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja.