Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nitoe pongezi kwa dada yangu Mheshimiwa Ummy kwa kazi kubwa anayoifanya, kazi inaonekana, chapa mwendo tuko pamoja na wewe. Lakini shukrani za pekee nizitoe mimi kama Mbunge wa Jimbo la Mlalo kwa msaada mkubwa wa mabati ulichotupatia katika kituo chetu Mwangoi, tunashukuru sana. Nitoe pia pongezi kwa Mheshimiwa Naibu Spika kama Balozi wa Afya katika Jimbo la Mlalo, umefanya mambo makubwa sana, Mwenyezi Mungu aendelee kukubariki na ile wodi ambayo tumeipa jina lako sasa tuko katika hatua za usafi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa haraka sana nichangie katika hoja iliyopo mbele ya Bunge lako Tukufu, nikianza katika ukurasa wa 112, vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2018/2019, kipengele namba mbili, kuimarisha huduma ya kinga dhidi ya magonjwa yanayotokana na kutokuzingatia kanuni za usafi na usafi wa mazingira kama magonjwa ya kuhara, kuhara damu, kipindipindu na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ipo kampeni inayoendelea sasa hivi ya “usichukulie poa nyumba ni choo” hapa kuna jambo la msingi saa ambalo Wizara inatakiwa ilifanyie kazi. Nimefanya utafiti mdogo katika Jimbo langu nimegundua kwamba watoto wengi wa shule ndio ambao wanaugua ugonjwa wa UTI na sababu kubwa inayosababisha tatizo hili ni ukosefu wa vyoo bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninaitaka sasa Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI watengeneze mkakati mahsusi wa kuhakikisha kwamba shule zetu za msingi na sekondari zinakuwa na vyoo bora kabisa. Inawezekana kabisa kila mwaka tunasema bajeti ya Wizara ni kubwa, haiongezeki lakini inawezekana tukawa tunahitaji bajeti kubwa kwa kuwaaminisha kwamba Watanzania ni wagonjwa sana kumbe tatizo siyo ugonjwa labda tukipata elimu inawezekana bajeti hii ikapungua kabisa wala hatuhitaji kuwa na mabilioni mengi katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba sana hii kampeni ya “usichukulie poa maisha ni choo” tuiendeleze na hata kule kwa wenzetu Wasukuma kule Mwanza tunaona nyumba ziko milimani kule na hatujui hata vyoo wanachimbia maeneo gani, naamini katika hili tutapunguza fedha nyingi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye report ya CAG amezungumzia deni la Wizara ya Afya katika hospitali zile za nje hasa kule India. Niiombe Wizara ilifanyie kazi eneo hili. Wapo Watanzania wengi sana ambao wanahitaji rufaa za kwenda kupata matibabu nje, lakini wanashindwa kwenda kwa sababu tunadaiwa fedha kule.

Kwa hiyo, nikuombe dada yangu Ummy, wewe ni shahidi kuna mgonjwa mmoja nilikuomba angalau umsaidie alikuwa ameshapata kibali na alikuwa ameshapata kibali na alikuwa yuko tayari hata kujilipia nauli tatizo lilikuwa fedha za matibabu na natumia nafasi hii kukwambia kwamba Mwenyezi Mungu yule mgonjwa amempenda zaidi. Kwa hiyo, huoni kwamba ni Watanzania wengi wanapoteza uhai kwa kukosa fursa hii? Kwa hiyo, nawaomba sana Wizara isimamie hili ili liweze kupata ufumbuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la Kituo cha Saratani cha Ocean Road; wanafanyakazi nzuri sana lakini kwa kweli kuna msongmanao mkubwa. Nitoe rai kwa Wizara hii; hebu tutengeneze mkakati wa kuwa na hospitali kwa kanda, tunaweza tukaanzia Kanda ya Ziwa pale Bungando, tukaenda Mbeya angalau pale hospitali ya Rufaa ya Mbeya tukatengeneza vituo vya saratani ili tupunguze ule msongamano pale Dar es Salaam. Wananchi wengi wanapata shida sana kwa kwenda mpaka Dar es Salaam kupata hii huduma ambayo sasa hivi sasa saratani imekuwa ni ugonjwa wa kawaida sana kwa ndugu zetu hawa.

Mheshimiwa naibu Spika, lingine nizungumzie huduma za hospitali katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa Bombo pale Tanga, najua Mheshimiwa Waziri wewe ni mwenyeji vizuri pale, lakini siyo wakati wote unapata muda wa kuembelea pale. Huduma zetu bado zinahitaji kuboreshwa sana . Tunaye Daktari Bingwa nadhani ni mmoja tu, kwa hiyo bado tunahitaji tupate Madaktari Bingwa wa kutosha. Kama unavyojua jiografia ya Mkoa wetu wananchi ni wengi sana wanaohitahi huduma katika hospitali hii, kwa hiyo, nikuombe sana na hili nalo ulizingatie.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, ahsante sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja.