Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Dr. Jasmine Tiisekwa Bunga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Vyuo Vikuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuipa kipaumbele sekta ya afya na kuendelea kuboreshwa kila wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi sana kwa mafanikio ambayo yanasaidia wananchi wa Tanzania kupunguza gharama za matibabu hasa nchi za nje. Mafanikio haya ni kama vile huduma za kupandikiza figo Muhimbili na Benjamin Mkapa Hospital; chanjo muhimu kwa watoto, chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana; upatikanaji wa dawa kwa kiwango kikubwa; dawa mpya ya kifua kikuu kwa watoto na ununuzi wa vifaatiba, mashine na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi hizi zinalenga kuendelea kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma za afya kwa wakati na ubora zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi pia kwa Mheshimiwa Waziri wa Afya pamoja na Naibu Waziri wake na timu yote ya wataalamu kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kusimamia na kutekeleza majukumu yao na kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda kutoa ushauri kwa Wizara hii ili kuweza kuendelea kutoa huduma bora; kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili wawe na tabia ya kupima afya zao na kugundua matatizo kabla hayajawa sugu na kuwasababishia vifo, gharama kubwa za matibabu na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu zaidi itolewe kupima tezi dume, saratani, ugonjwa wa ini, magonjwa yasiyoambukizwa (non-communicable diseases).

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza juhudi za Serikali kuwa na Bima ya Afya kwa kila mwanachi. Hivyo ili kuondoa changamoto ya msongamano wa wagonjwa kumuona daktari na kufanya vipimo ni vema sasa Serikali ikaendelea kuajiri madaktari na wasaidizi wengi wa afya ili kuondoa adha hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kitengo cha Tiba Asili ni cha muda mrefu, lakini bado hatujaona ripoti inayoonesha mafanikio ya upatikanaji wa dawa zilizothibitishwa na kitengo hiki ili zisambazwe kwenye maduka ya dawa. Hii itasaidia kupunguza matumizi ya dawa zenye kemikali ambazo si nzuri sana kiafya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuendelea kuboresha Hospitali za Rufaa za Mikoa kwa kuweka mashine za kisasa kama vile MRI, X-ray (Digital); CT-SCAN na kadhalika, lakini pia kuajiri Madaktari Bingwa ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Muhimbili na kupunguza gharama za usafiri na malazi kwa mgonjwa na ndugu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa kuna wanawake wengi wanaojifungua watoto zaidi ya mmoja. Wapo hadi wanaojifungua watoto watano. Wote tunafahamu ugumu wa kulea mapacha au idadi kubwa hiyo ya watoto watatu, wanne, watano na kadhalika. Ili kuokoa maisha ya watoto hawa pamoja na mzazi, kunahitajika matunzo ya hali ya juu ukizingatia familia hizi vipato vyao ni vidogo kukidhi kulea watoto wanne (kwa mfano) kwa wakati mmoja. Je, Wizara ina mpango mkakati gani katika kusaidia familia hizi kulea hawa watoto angalau katika kipindi cha mwaka mmoja wa kwanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wa mitaani na mimba za utotoni ni tatizo linaloendelea kukua katika nchi yetu. Sababu za watoto wa mitaani na mimba za utotoni zipo nyingi, lakini sababu mojawapo ni baba wa watoto hawa kukataa kutoa malezi na matunzo, hivyo kupelekea mama zao kushindwa kuwapa mahitaji ya msingi ikiwemo elimu, afya, chakula na kadhalika. Hali hii husababisha watoto hawa wajitafutie riziki kwa njia mbalimbali zikiwemo kuombaomba mtaani, kujiingiza katika mapenzi wakiwa na umri mdogo na kutumia ngono zembe na kadhalika.

Je, Serikali sasa, ina mpango mkakati gani wa kuhakikisha baba wa watoto hawa wanawajibika kulea watoto wao, maana hivi karibuni tumeshuhudia akina mama walivyofurika kwenda ofisini kwa Mheshimiwa RC wa Dar es Salaam kupeleka malalamiko yao. Hali hii imeonesha/
kudhihirisha kuwa kuna tatizo katika vyombo vya maamuzi ikiwemo Mahakama na Ustawi wa Jamii katika kuwawajibisha akina baba hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia na ninaomba kuwasilisha.