Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Wizara kwa kugusia vitu vichache, lakini muhimu sana. Ni kweli kwamba Tanzania tumeingia Mkataba wa Abuja (Abuja Declaration) ya kutenga walau 15% ya bajeti yote kwenye afya, lakini miaka yote tumekuwa tukitenga fedha chini ya 10% na bado hatutekelezi hata hii asilimia ndogo tuliyotenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuizungumzia kwa takwimu sehemu mojawapo ya bajeti ya afya ambayo ni kuzuia vifo vya mama na mtoto, lakini katika bajeti ya mwaka 2017/2018 kwenye mradi wa kupunguza vifo vya akina mama zilitengwa jumla ya shilingi bilioni 12 ambazo zote ni fedha za ndani; kwenye ukurasa wa 179 kwenye jedwali la mchanganuo wa fedha za miradi ya maendeleo halijaonesha mchanganuo ni kiasi gani ambacho kilipokelewa katika kutekeleza mradi huu ikizingatiwa kwenda 2017/2018 fedha za ndani ambazo zilipaswa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa Wizara hii ilikuwa 42.8% ya fedha za ndani na zilizopelekewa zilikuwa 19% tu ya fedha iliyoidhinishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka unaokuja wa fedha 2018/2019 mradi wa kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi umeongezewa bajeti kwa 0.82% na hivyo kufikia shilingi bilioni 12.2 tu. Je, Wizara imezingatia masuala au vigezo gani katika ongezeko hilo ukilinganisha na ukubwa wa tatizo la vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi nchini?

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwa mwaka wa fedha 2018/2019 mradi wa kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi umetengewa shilingi bilioni 12.2 na katika malengo ya utekelezaji wake kwa mwaka 2018/2019 karibu 50% ya kiasi chote kilichotengwa imeelekezwa katika kukamilisha malipo ya mchango wa Serikali katika First Health Rehabilitation Project uliokuwa wa ukarabati mkubwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Kutokana na mradi huu kuchukua fedha nyingi ambazo ni takribani shilingi bilioni sita karibu 50% kutoka kwenye kiasi kilichotengwa kwa mradi wa kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kujua mradi huu wa First Health Rehabilitation umesaidia au utasaidia kwa kiwango gani kupunguza vifo vya akina mama ukilinganisha na kiasi kikubwa cha pesa zilizoelekezwa huko?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine kwa mwaka wa fedha 2018/2019 bajeti ya miradi ya maendeleo imeshuka kutoka kiasi cha shilingi bilioni 785.8 (785,805,952,000) kwa mwaka 2017/2018 mpaka shilingi 561,813,998,998 kwa mwaka 2018/2019 ambayo ni sawa na 28.50%. Nataka nijue Wizara ina maelezo gani kuhusu punguzo hili ukiangalia kwamba kutoka bajeti ya mwaka 2017/2018 ni 49% kati ya bajeti iliyopangwa ndio zilizopelekewa katika kutekeleza miradi ya maendeleo hii inamaanisha kuna miradi mingi bado haijateakelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kujua Serikali imejipangaje katika kutekeleza miradi iliyopangwa kwa mwaka uliopita na kuendeleza miradi iliyopangwa kwa mwaka huu kwa punguzo hili la bajeti ya miradi ya maendeleo?

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya maendeleo kwa mwaka 2018/2019 imepunguza utegemezi wa fedha za nje katika bajeti ya mradi wa maendeleo yenye kiasi cha shilingi 561,813,998,998 fedha toka vyanzo vya nje ni shilingi 184,959,998,998; je, Wizara imejipangaje katika ukusanyaji wa mapato ya fedha za ndani ili kukamilisha utekelezaji wa mradi wa maendeleo kwa kuzingatia mwaka 2017/2018 fedha za ndani zilizokusanywa kutoka bajeti ya maendeleo iliyopokelewa ni shilingi 385,771,297,343 zilikuwa ni shilingi 64,756,206 sawa na 19% na fedha za nje zilikuwa shilingi 34,015,208,137.12 sawa na 71% zilizoidhinishwa. Hii ina maana kwamba fedha maendeleo zinatoka nje.