Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu kwa hotuba yake nzuri na yenye kuleta matumaini. Tatizo la x-ray na Hospitali ya Wilaya ya Mafia limeingia katika hatua nzuri kuelekea kumalizika baada ya Serikali kutupatia mtaalamu wa mionzi (Radiology) na kufuatia mazungumzo yangu na Naibu Waziri Mheshimiwa Faustine Ndugulile tumekubaliana kuuwa tarehe 23 Aprili ataleta mtaalam sambamba na mtaalam wa kampuni iliyoleta x-ray hiyo ambao mimi Mbunge nawajibika kuwalipia gharama za safari zao kutoka India mpaka Mafia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nalisema hili kwa sababu mara ya kwanza mwaka 2016 niliingia gharama ya kuwaleta wataalam hao kwa gharama kubwa kuwafikisha Mafia na Wizara yako Mheshimiwa Waziri iliweka katazo la kufanya x- ray ya zamani iliyotolewa na kampuni ya Philips ambayo ndio yenye mkataba na Wizara kutengeneza mashine za x-ray. Mheshimiwa Waziri wataalam wale walikaa Mafia kwa wiki tatu huku mimi binafsi nikishughulikia vibali vya kufunga mashine bila ya mafanikio.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo furaha kukufahamisha kuwa baada ya mjadala mrefu uliopelekea kujengwa kwa chumba kipya cha x-ray sasa Wizara imeridhia kufungwa kwa x-ray Mafia na Naibu Waziri amenihakikishia atatuma mtaalam wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, angalizo ninalotaka kulitoa hapa ni mnaingia gharama kwa mara ya pili kuwaleta wataalam kutoka India kuja kufunga x-ray ile. Ninaomba Wizara itekeleze ahadi yao hii ya kutoa ushirikiano ili x-ray ile ifungwe Mafia. Ni ukweli usio na shaka ikishindikana kufungwa mara hii sitapata na sitakuwa na uwezo wa kugharamia gharama hizi ambazo kwa kweli ni kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Hospitali ya Wilaya ya Mafia gari la wagonjwa (ambulance)ni kuukuu na hufanya kazi kwa taabu sana na linaharibika mara kwa mara. Hivyo tunaiomba Wizara itufikirie kupata ambulance mpya. Sambamba na hilo Kisiwa cha Mafia kimezungukwa na visiwa vidogo vidogo vinne yaani Jibondo, Bwejuu, Chile na Juani. Kwa namna ya kipekee tunaiomba Wizara itusaidie kupata ambulance boats ili kusaidia dharura zinapotokea iwe rahisi kuwa wagonjwa kukimbizwa Hospitali ya Wilaya.

Mwisho tunaishukuru Serikali kwa ahadi ya shilingi milioni 500 za kujenga Kituo cha Afya Kirongwe. Tunaomba tuharakishiwe kupata fedha hizo ili ujenzi uanze mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naunga mkono hoja.