Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naunga mkono hoja, pili nataka kueleza kwamba hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Kamati inayosimamia Wizara hiyo pamoja na wachangiaji wengi wameelezea umuhimu wa kupatikana haraka iwezekanavyo watumishi wa Idara ya Afya. Wameeleza kuwepo kwa upungufu katika maeneo mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kutoa taarifa na kuwaondoa mashaka Waheshimiwa Wabunge kwamba kama mnavyokumbuka mwezi Oktoba, 2016 Serikali ilifanya zoezi la uhakiki, katika uhakiki ule walipatikana jumla watu 14,000 wa kada mbalimbali ambao waligundulika kujipatia kazi kwa vyeti vya kughushi. Kati yao walikuwemo watumishi 3,310 kutoka katika sekta ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa uhakiki huo Serikali ilisitisha ajira kwa maana ya kujiridhisha tuna watumishi wangapi. Napenda niliarifu Bunge lako tukufu kwamba zoezi lile limekamilika na kazi ya kwanza iliyofanywa na Wizara yangu ilikuwa ni kuziba pengo la wale watu ambao walionekana wameondolewa katika utumishi wa umma. Kwa hiyo, ilitoa kibali kuajiri watumishi mbadala 2,500 ili kufidia upungufu uliotokana na watumishi wa kada ya afya kuondolewa; kwa hiyo hao zoezi hilo linaendelea. Pamoja na hayo katika mwaka wa fedha 2017/2018 kama mtakumbuka Bunge hili lilipitisha ajira ya watumishi 52,436 zikiwemo nafasi za ajira za watumishi wa kada ya afya 14,104 sawa na aslimia 26.9 ya nafasi zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili zoezi la watu 52,000 tutakapokuwa tunaajiri asilimia 26 sawasawa na watu 14,000 watakuwa wametoka sekta ya afya. Pia katika bajeti mlionipitishia juzi, na ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge Serikali imetenga nafasi zingine za ajira 49,536. Ukichanganya wale 49,000 na 52,000 tutaajiri watumishi inafika karibu laki. Sasa ajira ya watumishi wa kada ya afya katika hao laki moja ni 16,205 sawa na asilimia 32.7 watakuwa ni watumishi wa sekta ya afya. Kwa hiyo utaona kwamba Serikali tumejipanga. Hata hivyo msisitizo wa Serikali kwa sasa ni kuhakikisha huduma za afya hazikwami kwa namna yoyote ile na hivyo ninawataka waajiri wote katika Serikali za mitaa kufanya uwahishaji wa matumizi kada za afya pamoja na kada nyingine kwa kuwatoa watumishi wa kada hizi sehemu mbalimbali ambapo wapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nataka kusisitiza watu wengi, Waheshimiwa Wabunge wengi walipokuwa wanachangia hapa ndani walikuwa wanaeleza kwamba ziko zahanati zimefungwa, kuna vituo vya afya vimefungwa kwa kukosa watumishi. Mimi nataka kuliambia Bunge lako tukufu, nilishatoa maagizo na leo narudia tena, Serikali ya CCM haitoruhusu kituo cha afya kifungwe kwa sababu ya kukosa watumishi. Nilishasema ikitokezea mahala pengine amefariki maana si lazima iwe kwa sababu ya kufukuzwa, iwe kwa sababu yoyote ile Serikali ya CCM haitaruhusu kituo cha afya kifungwe kwa sababu ya kukosa mtumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikipata taarifa katika Wizara yangu haraka haraka pale walipo wengi nitahamisha mtu nitapeleka wakati zoezi la kuajiri linaendelea naomba nilieleze Bunge lako Tukufu kuanzia leo yoyote ambaye aliongea humu ndani ambaye ana uhakika kuna zahanati haina mtumishi imefungwa; kuna kituo cha afya kimefungwa huduma zinakosekana niletewe taarifa hiyo wakati Bunge hili linaendelea nitapeleka watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.