Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kusimama hapa, nianze kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia hoja yangu ya kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka 2018/2019. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya kipekee nimshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo na Huduma ya Jamii, Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba ambaye amewasilisha Maoni na Ushauri wa Kamati kuhusu utekekelezaji wa kazi za Wizara kwa mwaka 2017/2018 pamoja na bajeti ambayo tunaipendekeza Bunge lako Tukufu kuipitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawashukuru Kamati kwa kututia moyo, kwa kupongeza Wizara yangu na kwa niaba ya wafanyakazi wote wa sekta ya afya katika ngazi zote nchini Tanzania na maendeeo ya jamii kwa niaba yao napenda kupokea pongezi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kutoa majibu ya hoja mbalimbali ambazo zimewasilishwa na Waheshimiwa Wabunge niwatambue Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa kuzungumza na kwa maandishi; na kwa sababu kanuni zinanibana kuwataja niseme tu kwamba hoja yangu imechangiwa na Wabunge 117, kati ya hao Wabunge 73 wamechangia kwa kuzungumza na Wabunge 44 wamechangia kwa maandishi. Aidha, Waheshimiwa Wabunge nane wamechangia kuhusu sekta ya afya wakati wa mjadala wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kutoa ufafanuzi, niseme kwamba tumepokea maoni, ushauri na mapendekeo ya Kamati na Waheshimiwa Wabunge kuhusu kuboresha huduma za afya. Vilevile tumepokea pongezi zenu na mimi ninasema pongezi hizo zirudi kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye kwa dhamira yake ya dhati ameamua kuwekeza kwenye afya ya Watanzania; na hii ni kutokana na kuamini kwamba hatuwezi kujenga Tanzania ya viwanda bila kuwa na Watanzania wenye afya bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ametoa kipaumbele katika sekta ya afya. Kabla hajaingia madarakani tunaona kwamba bajeti ya sekta ya afya imeongezeka. Wakati hajaingia madarakani ilikuwa shilingi trilioni 1.8, mwaka wa kwanza wa Mheshimiwa Magufuli imepanda mpaka shilingi trilioni 1.9 na mwaka wa pili wa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli bajeti ya Sekta ya Afya imepanda mpaka shilingi trilioni 2.2.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kwamba Wizara ya Fedha wanaendelea kufanya tathmini na uchambuzi wa bajeti ya mwaka 2018/2019. Sina shaka hata kidogo kwamba sekta ya afya itaendelea kuwa kipaumbele kati ya vipaumbele vitatu vya Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu changamoto za sekta ya afya katika nchi yetu ni nyingi, hasa katika mazingira ambayo tuna idadi kubwa ya wanawake ambao wanazaa watoto wengi. Kiwango cha uzazi ni asilimia 5.1. Vilevile tuna mzigo wa magonjwa, zamani tulikuwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kipindupindu, TB, HIV lakini sasa hivi tunabeba mzigo wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo kisukari, magonjwa ya moyo na saratani.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na changamoto hizi, sekta ya afya katika kipindi cha miaka miwili na nusu ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli imepata mafanikio makubwa sana. Tumeona leo katika historia ya nchi yetu Tanzania tumeanza kupandikiza figo katika Hospitali yetu ya Muhimbili na hospitali yetu ya Benjamin Mkapa. Lakini tumeona watoto wanaozaliwa na matatizo ya kusikia wakiweza kupandikiziwa vifaa vya kuongeza usikivu katika Hospitali yetu ya Muhimbili wakati zamani miaka miwili na nusu iliyopita huduma hizi zilikuwa hazipatikani katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kaka yangu James Mbatia aliongelea kuhusu Medical Tourism in Tanzania. Nataka kusimama mbele ya Bunge lako tukufu kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge ndani ya Magufuli Medical Tourism Tanzania itawezekana na itawezekana kwa kipindi kifupi tu. Tunamaliza kufunga mitambo ya LINAC katika Hospitali yetu ya Ocean Road ambayo ni mionzi ya kisasa kwa ajili ya tiba ya saratani. Tunakaribia kununua kifaa cha Pet Scan, hakipo Kenya, hakipo Uganda, hakipo Zambia, hakipo Malawi. Kwa hiyo, watu wa kutoka nchi za Afrika watakuja Tanzania kwa sababu ya uwekezaji mkubwa ambao anaufanya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo ya Mheshimiwa Rais ni mengi, lakini nimalize tu kwa kusema tumeona uwekezaji mkubwa katika afya ya mtoto, asilimia 97 ya watoto wote Tanzania wanapata chanjo, na sisi tumejidhatiti tutamfikia kila mtoto popote alipo ili kuhakikisha anapata chanjo ili kuweza kumkinga na magonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo sasa nijibu hoja za Waheshimiwa Wabunge na nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ufafanuzi ambao ameutoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na hoja kubwa za Kamati. Kamati imezungumzia kuhusu makubaliano ya Abuja ambayo yalifanyika mwa 2001 ambapo nchi za Afrika zilikubaliana kutenga asilimia 15 ya bajeti zao za nchi katika ajili ya kutatua changamoto za sekta ya afya. Suala la Abuja Declaration ni dhamira si kwamba ni kitu kina-bind, kinabana nchi wanachama, ni dhamira ya nchi za Afrika kuwekeza kwenye sekta ya afya. Hata hivyo kama nilivyosema tumeona uwekezaji ambao Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ukifanya katika sekta ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, tumefanya utafiti, ni nchi moja tu ya Afrika ambayo bajeti yake ni asilimia 15 ya bajeti ya nchi. Kwa sababu kama nilivyosema changamoto za nchi za Afrika ni nyingi, kuna masuala ya maji, barabara, kilimo,na maji. Kwa hiyo muhimu kile kidogo ambacho tunakipata muhimu kwetu sisi sekta ya afya ni kuhakikisha kwamba kinatumika kikamilifu bila kupotea katika mambo ambayo hayana tija kwa Watanzania hasa Watanzania wanyonge. Kwa hiyo, nashukuru maoni ya Kamati kwamba haijafika lakini ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba tunafikia asilimia 15 ya bajeti nzima ya Serikali katika sekta ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati imeongea suala la kwamba bajeti ya Wizaya ya Afya kwa mwaka 2018/2019 imepungua ukilinganisha na ya mwaka 2018/2019.

Waheshimiwa Wabunge, mwaka jana wakati nawasilisha bajeti hapa mlini-challenge kwamba Mheshimiwa Waziri bajeti yako kwa kiasi fulani inategemea wafadhli wa nje, je, wafadhili wa nje wakijitoa mtatatua vipi changamoto za sekta ya afya?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kilichotokea bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka huu kwa fedha za ndani imeongezeka kutoka bilioni 628 mwaka jana hadi bilioni 681. Punguzo tunaloliona ni fedha za nje na hii ni kuonesha dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ya kutaka kupunguza utegemezi kwa wadau wa maendeleo katika kutatua changamoto za watanzania ambao wao ndio wamempa ridhaa ya kumchagua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ukiangalia domestic allocation zimepanda, lakini kwenye forex zimeshuka, na ni kwa sababu tunataka kuanza kujipima wenyewe leo donor akijitoa tutaweza kutatua changamoto zetu kwa kiasi gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo limeongelewa na Kamati ni suala la kwamba inashauri Serikali kutoa fedha zote zilizotengwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kama ambavyo Bunge lako tukufu liliidhinisha. Serikali hii ni sikivu na kwa sababu bado hatujamaliza mwaka wa fedha wa 2017/2018 tunaamini kwamba tutaweza kupata fedha kutoka Wizara ya fedha na mipango kwa ajili ya kutekeleza miradi ambayo tumejiwekea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala ambalo Kamati ya Bunge imelizungumzia, suala la lishe, kwamba lishe sio suala la wizara ya afya pekee bali ni suala mtambuka na Serikali ichukue hatua za makusudi za kupunguza janga la lishe. Tunapokea ushauri na maoni ya Kamati kuhusu suala hili, na mimi nikiwa Waziri mwenye dhamana nimefarijika sana kuona Kamati ya Bunge na Wabunge wote wanatoa kipaumbele katika suala la lishe. Kwa kweli suala la lishe na mimi nakubaliana nanyi si suala la mchezo kwa sababu kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015/2016 kiwango cha udumavu kwa watoto wetu ni asilimia 34. Of course tumepiga hatua ukiangalia kutoka mwaka 2010 ilikuwa ni asilimia 42.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini maana ya watoto kuwa na udumavu ni nini, tunawekeza katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda, tunakosa watoto ambao wanaweza wakawa na ubunifu, udadisi lakini ambao wanaweza wakawa na afya bora kwa ajili ya kutatua changamoto za kujenga Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama Serikali tumechukua mikakati na hatua mbalimbali chini ya uratibu wa Mheshimiwa Waziri Mkuu na yeye mwenyewe alisimamia kikao cha kwanza cha wadau wa masuala ya lishe kutoka wizara zote ambapo sasa tunatekeleza mpango jumuishi wa kitaifa wa utekelezaji wa masuala ya lishe kwa kipindi cha 2016/2017 mpaka 2020/2021. Mpango huu umeweka vipaumbele mbalimbali ambavyo Mikoa pamoja na Halmashauri zitatekeleza katika kuinua hali ya kiwango cha lishe nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimshukuru sana Waziri wa Fedha Dkt. Mpango, hayupo hapa, lakini baada ya kuona tatizo la lishe aliahidi na ameyatekeleza. Katika Wizara ya Fedha sasa hivi kuna Afisa mahususi ambaye anahusika na masuala ya lishe, yeye kazi yake ni kuangalia bajeti zote hizi ni kiasi gani masuala ya lishe yamepewa kipaumbele. Pia tumepeleka maafisa lishe sasa hivi wako katika mikoa, wako katika halamashauri pia wako katika ngazi mbalimbali za wizara mtambuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumezindua pia mpango wa kuhamasisha mabadilko ya tabia miongoni mwa jamii ijulikanayo kama Mkoba wa siku 1000 za mwanzo, kwa sababu kwa mujibu wa wataalam wa afya siku 1000 za mwanzo za mtoto ndizo siku muhimu katika maisha yake. Pia tumeongeza idadi ya viwanda vinavyoongeza virutubishi, tunasema food fortification kutoka viwanda 13 hadi viwanda 21. Sasa hivi viwanda ambavyo vinazalisha ngano, mafuta ya kula, unga wa mahindi na chumvi lazima viwe na virutubisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ambayo tunaipata na mimi nikiri, kwa sababu wanakoboa unga katika lower level kwenye vijiji na mitaa, kwa hiyo, kidogo kuwabana kwamba ule unga ambao wanazalisha uwe na virutubisho inakuwa ngumu. Lakini kubwa ambalo tumeliona ni kutoa elimu ya lishe katika jamii kwa sababu hata ukiangalia mikoa ambayo ina viwango vikubwa vya udumavu unakuta ni mikoa ambayo ina uzalishaji mkubwa wa chakula. Kwa mfano, tukiangalia Rukwa wana udumavu asilimia 56 wakati ndio wazalishaji wakubwa wa chakula. Tukiangalia Njombe, Ruvuma, Iringa, Katavi na Mbeya. Kwa hiyo, sisi tumeona ni suala la elimu kwa jamii hasa kwa siku zile ambazo mama anajiandaa kubeba ujauzito.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa ambalo tutaendelea nalo pia ni kuhimiza uzalishaji na matumizi ya mazao lishe katika mahindi, viazi vitamu, maharage na mihogo; lakini ambalo sasa nataka kulifanya baada ya kuwasikiliza Waheshimiwa Wabunge ni kufanya tafiti ya kitaalam ili kubaini sababu au chanzo cha hali ya lishe nchini. Kwa sababu nimesema Rukwa, Katavi, Iringa, Njombe wanazalisha chakula kwa nini tuna udumavu. Kwa hiyo nataka kupata majibu ya kisayansi kuhusu hali ya viwango vya utapiamlo katika baadhi ya mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala kubwa ambalo limeongelewa na Wabunge wote, Wabunge wanawake na wanaume ni suala la huduma za mama na mtoto. Tunawashukuru sana Kamati kwa kupongeza jitihada ambazo Serikali inafanya katika kuhakikisha kwamba tunaboresha huduma za afya ya mama na mtoto ikiwemo huduma za upasuaji wa dharura.

Waheshimiwa Wabunge wameniuliza Mheshimiwa Waziri kwamba vifo vitokanavyo na uzazi vinaongezeka tumetoka kwenye 432 mwaka 2015/2016 vimefika mpaka vifo 556.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunatoa majibu haya Disemba, 2016 tulitaka kubishana, tulibishana kidogo tukasema tumekosea wapi, pamoja na jitihada zote ambazo Serikali imefanya kwa nini vifo vya akina mama wajawazito vimeongezeka? Baada ya kutafakari tukaamua hakuna maana ya kubishana, awe amekufa mwanamke mmoja bado kwetu sisi ana umuhimu mkubwa sana. Kwa hiyo, tukajikita katika kuchukua hatua za kuboresha huduma ya mama na mtoto na ndiyo maana sasa hivi tukaandika andiko na tukapata fedha kwa ajili ya kuboresha vituo vya afya ili viweze kutoa huduma za uzazi za dharura ikiwemo upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Watanzania wanataka kumuhukumu Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli mumuhukumu kwa jitihada ambazo amezifanya katika kuboresha huduma za upasuaji za dharura. Mwaka jana ni asilimia 21 tu ya vituo vya afya vya Serikali vinavyoweza kufanya upasuaji, lakini tutakapofika Disemba tutakuwa na asilimia 53 ya vituo vya afya vya Serikali vitakavyoweza kufanya upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ambayo iko mbele yangu sasa kama sekta ni kuhakikisha tunakuwa na wataalam, watumishi wenye ujuzi ambao wataweza kuwahudumia akina mama wajawazito ambao watapata matatizo ya uzazi wa dharura. Tumeshaanza kuwafundisha wauguzi katika masuala ya utaalamu wa usingizi ambao tutawasambaza katika vituo hivi ambavyo vinajengwa theatre. Tumesambaza ambulance 50 katika mikoa mbalimbali pamoja na kuimarisha huduma za damu salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hatua inayokuja sasa hivi kama nilivyosema ni kuimarisha huduma za uzazi wa mpango. Kwa sababu wataalam wamenifundisha Wizara ya Afya kwamba endapo tutakuwa na idadi kubwa ya wanawake wanaotumia uzazi wa mpango tutaweza kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 30.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge tuhimize matumizi ya uzazi wa mpango kwa wanawake kwa sababu sasa hivi ni asilimia 32 tu ya wanawake nchini Tanzania ambao wanatumia huduma za kisasa za uzazi wa mpango. Pia tutaendelea na jitihada za kuimarisha huduma wakati wa ujauzito na hapa tunahitaji lengo letu wanawake wajawazito angalau wahudhurie kliniki mara nne kama wataalam wanavyoshauri. Sasa hivi wanawake wanahudhuria kliniki mara nne ni asilimia 51.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo eneo ambalo tutaliboresha pia pale ambapo mama mjamzito anaenda kliniki tunataka apate huduma bora badala tu ya kupoteza muda wake. Tunawaambia wenzetu mama mjamzito anatoka kilometa 20, 30 hata 40 anafika kwenye kituo hapimwi wingi wa damu, hapimwi maambukizi aliyokuwa nayo, hapewi huduma mtoto amekaa vizuri, kwa hiyo, tunatoka kwenye miundombinu tunaenda kwenye ubora wa huduma. Tunataka kuona huduma bora kwa akina mama wajawazito. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa mama na mimi nimeingia labour mara mbili, nataka kuwaahidi Waheshimiwa Wabunge na Watanzania tutahakikisha huduma kwa mama mjamzito zinaendelea kuboreka.

Mheshimiwa Naibu Spika, limejitokeza suala la delivery pack kwamba zinauzwa, na pia tutoe ufafanuzi kwamba matibabu kwa wajawazito je, ni bure au si bure?

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Afya na mimi nimeuwa nikilisisitiza hivi si hili kwamba matibabu kwa wajawazito, huduma kwa wajawazito ni bure kuanzia wakati anapohudhuria kliniki mara tu baada ya kujigundua ni mjamzito, lakini pia wakati wa uzazi na wiki sita baada ya kujifungua. Kwa hiyo suala la kwamba akina mama wajawazito wanatozwa fedha za kumwona daktari nalikemea mara moja, na niwatake watoa huduma za afya zote Waganga Wakuu wa Mikoa kusimamia agizo hili, kusimamia sera hii. Ni marufuku kum-charge mama mjamzito fedha pale ambapo amekwenda katika kituo cha kutoa huduma za afya kwa ajili ya kupata fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la delivery pack, Waheshimiwa Wabunge mama mjamzito hatoi fedha ya kumwona daktari, hatoi fedha ya dawa, hatoi fedha anapojifungua wala hatoi fedha ya kufanyiwa upasuaji. Kwa hiyo delivery packs zitaendelea kuwepo kaatika vituo vya kutoa huduma za afya kwa kuzingati rasilimali fedha ambayo Serikali au kituo kinacho. Nimeongea hapa, kwa mwaka tunakuwa na wajawazito milioni mbili delivery pack 21,000. Waheshimiwa Wabunge, naomba mnisaidie shilingi bilioni 40 ambazo kila mwaka tutazitenga kwa ajili ya kutoa delivery pack. Sisi tulichokifanya pale ambapo kuna fedha za Serikali na mama mjamzito ataenda atakuta vifaa hivi atapewa bure. Sasa suala la delivery pack ni suala la mama mjamzito kujiandaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, uzazi si dharura ni miezi tisa, uzazi ni miezi tisa, kwa hiyo, ni sawa sawa na mama anavyojiandaa kununua nguo ya mtoto, kununua kanga, akiikuta delivery park kwenye kituo atasema Alhamdulillah, asipoikuta inakuwa ni sehemu ya maandalizi. Hata hivyo nataka kuendelea kuwaahidi, tunaelekea kwenye Bima ya Afya kwa kila mtu (Universal Health Coverage). Kundi ambalo tutaanza nalo pale ambalo tutatoa Bima ya Afya, kwa sababu tumesema akina mama wajawazito huduma ni bure tutawapatia huko mbeleni, kwa hiyo, ndio kundi ambalo tutalipa kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ina maana tunaweza tukaangalia utaratibu wa kupata kadi za bima ya afya ili waweze kupata huduma bila vikwazo vya fedha. Tumeanza kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani, huduma hii tunaiita Tumaini la Mama, inafanyika katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga na Mbeya. Msije mkasema Tanga nimeikuta hata kabla sijawa Waziri, kwa hiyo, ni eneo ambalo tumeanza nalo, lakini tunaamini kwamba tutaweza kuboresha huduma hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine lililohusu masuala ya afya ya mama na mtoto ni suala la chanjo ya kuwakinga wasichana na saratani ya mlango wa kizazi. Nafurahi kuona kwamba Waheshimiwa Wabunge mmelipokea vizuri na wengi mmetusisitiza kwamba tukatoe elimu kwa jamii na sisi tutaenda kutoa elimu kwa jamii.

Tunaomba Wabunge, hasa Wabunge wenzangu wanawake, kumuuguza mgonjwa mmoja wa saratani ya mlango wa kizazi tunatumia shilingi milioni tano, hatujahesabu gharama familia ambayo inaingia katika kumuuguza mgonjwa yule. Nadhani tutakuja kufanya semina muone, endapo tutawachanja wasichana na chanjo hii ya saratani ya mlango wa kizazi ndani ya miaka 10 saratani ya mlango wa kizazi itakuwa historia katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai tena kwa wazazi na walezi wenzangu, tuwapeleke binti zetu kupata chanjo hii. Mimi mwenyewe binti yangu ana miaka 13. Tumeanza na miaka 14 kwa sababu chanjo hizi mahitaji ni makubwa sana. Waziri wa Afya wa Nigeria kwa mwaka anahitaji dozi milioni 20, mimi nikiwachanja mabinti wote wa miaka tisa mpaka 14 nahitaji dozi kama milioni 3.9. Kwa hiyo, mzalishaji amesema nitaweza kuwapa dozi za wasichana 600,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tumeona badala ya kusubiri mpaka mwakani na Mheshimiwa Kiteto Koshuma umeongea vizuri, watoto wetu wanaanza utundu mapema. Tunaweza tukasema tusubiri mwakani tuwachanje wote miaka tisa mpaka 14 hawa 14 kuna asilimia fulani tutawapoteza. Kwa hiyo, tumesema tuanze na miaka hii 14 halafu sasa mwakani tutawatoa wasichana wote na Mheshimiwa Angellah Kairuki ameniahidi na yeye watoto wake amewachanja tena amewachanja dozi tatu.

Kwa hiyo, akina mama Wabunge nitaomba tutoke mbele, tuwashawishi wanawake wenzetu kwamba chanjo hii ni salama. Chanjo hii itapigwa dozi mara moja kwenye sindano halafu baada ya miezi sita itarudia. Sambamba na hayo tutaongeza jitihada pia za kuwapima na kutoa huduma za matibabu ya awali kwa wanawake wajawazito.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati pia iliongelea suala la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na ambao wameshauri kwamba tuufanyie marekebisho pamoja na kuja na vifurushi vya bima. Ushauri huu tunaupokea na mimi mwenyewe nimekuwa nikiwa-challenge Bima ya Afya, kwamba kwa nini msifanye kama kampuni za simu, jipimie, unajipimia. kwamba unataka huduma za afya mpaka Muhimbili, unataka huduma za afya mpaka Hospitali ya Bombo Tanga au unataka huduma za afya mpaka ufike KCMC.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimefurahi kwamba ndani ya siku chache tutazindua vifurushi mbalimbali ili wananchi wajipimie katika kupata huduma za matibabu. Pia tumeona kuna bima ya afya, total afya kadi 50,400 kwa mtoto matibabu mwaka mzima mpaka Muhimbili, mpaka MOI mpaka JKCI. Kwa hiyo, tumekubaliana badala ya kusubiri mzazi alipe shilingi 50,400 kwa mara moja nimewaelekeza NHIF waweke utaratibu, mzazi leo ana shilingi 5000 anachangia, ana shilingi 10,000 anachangia, baada ya miezi fulani tumeweka utaratibu wa miezi mitatu kadi itakuwa imekamilika mnampa bima ya afya mtoto anakuwa na uhakika wa matibabu kwa mwaka mzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa Nzega kwa Mheshimiwa Bashe, tukawauliza boda boda kuna bima ya afya ya kikundi tunaita kikoa, kwa nini hamkati? Wakaniambia Waziri shilingi 78,600 hatuwezi, lakini ukiniambia nitoe shilingi 2,000 kila siku nitaweza kuchangia shilingi 2,000. Kwa hiyo tumeona kwamba inawezekana kuongeza idadi ya Watanzania watakaokuwa na bima ya afya lakini lazima pia na sisi tuwe wabunifu. Kwa hiyo, tunaupokea ushauri wako Mheshimiwa Peter Serukamba pamoja na Wabunge wote ambao mmeutoa katika kuongeza idadi ya Watanzania ambao wana Bima ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumejiongeza, tunafanya mazungumzo na vyama vya ushirika, Wabunge wa Mikoa ya Kusini mmezungumzia suala la korosho. Kwa hiyo, tayari tunasema wakati mkulima anauza korosho basi pale pale aweze pia kukatwa na Bima ya Afya.

Kwa hiyo tumechukua hili zao la korosho, pamba pamoja na kahawa, na vyama vya ushirika vimeshakubali, kwamba pale ambapo wananchi wanapewa fedha zao watakatwa pia ili kupata Bima ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge matibabu ni gharama na matibabu ni gharama narudia tena tukisema kila mzigo ubebe Serikali hatuwezi kufika, tutakuwa tunajidanganya. Kama wapiga kura wetu wanaweza kununua vocha ya simu shilingi 500 kila siku siamini kwamba wanashindwa kuchangia shilingi 500 hiyo hiyo ili waweze kupata Bima ya Afya.

Kwa hiyo, tutaendelea pia kuhamasisha ili wananchi waone kwamba kuwa na Bima ya Afya unakuwa na ukahika wa kupata matibabu kabla ya kuugua. Mtu maskini akiumwa leo atauza baskeli yake, atauza shamba, atauza vitu alivyokuwa navyo, lakini mwenye Bima ya Afya ataweza kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya Kamati pia ilikuwa ni mapambano dhidi ya UKIMWI, kwamba upatikanaji wa fedha za Serikali kwa ajili ya ununuzi wa dawa za kufubaza UKIMWI tunategemea wenzetu kutoka nje. Tumepokea changamoto hii na nitumie fursa hii kuwatoa hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Jenista tumeanzisha extra fund ambayo itaweza sasa kugharamia huduma mbalimbali zinazolenga UKIMWI.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Jenista nakushukuru sana uliweza kunipa cheque ya milioni 260 ili tuweze kununua dawa kwa ajili ya magonjwa nyemelezi kwa wenye matatizo ya UKIMWI. Kwa hiyo, suala hili ninamini kabisa kwamba ndani ya muda mchache; na sasa hivi pia, kama nilivyosema tunakamilisha mkakati wa kugharamia huduma za afya (financing for health sector). Kwa hiyo katika mkakati huu pia tumebainisha maeneo ambayo tunaweza tukapata vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kugharamia huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa naongea na Waziri mwenzangu wa South Africa, wao katika kila asilimia fulani ya fedha ambayo ni kwa ajili ya sukari inaenda kwa ajili ya kugharamia pia changamoto za sekta ya afya. Juzi tulikuwa pia na watu wa Ghana na wenyewe wametupa nao uzoefu wao kwamba asilimia mbili ya VAT pia inaenda kugharamia huduma za afya. Kwa hiyo, tutaendelea kufanya mashauriano na wenzetu Hazina ili kuona ni kiasi gani basi; Mheshimiwa Bashe amezungumza wale watu maskini ambao kwa mujibu wa takwimu za World Bank ni asilimia kama 28 ya Watanzania ndio maskini sana. Kwa hiyo, tutaangalia ni kiasi gani sasa tutaweza kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kugharamia changamoto za afya ikiwemo masuala ya UKIMWI na HIV. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala ambalo pia limeongelewa na Waheshimiwa Wabunge hasa Mheshimiwa Lubeleje ni suala la afya ya mazingira. Nimpongeze sana Mheshimiwa Lubeleje kwamba hawa Mabwana Afya wamewekwa katika maeneo ambayo si sahihi. Mheshimiwa Lubeleje nimepokea hoja yako na ndiyo maana ukiangalia hotuba yangu ya bajeti ya mwaka jana na mwaka huu. Mwaka huu baada ya chanjo eneo la pili ambalo nimeliweka ni suala la afya na usafi wa mazingira. Kwa sababu tunapoteza fedha nyingi sana katika kutibu magonjwa ya kuhara kipindupindu na minyoo na magonjwa mengine ilhali tungeweza kuyaepuka pale ambapo Watanzania watazingatia kanuni za usafi wa mazingira pamoja na usafi wa afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni kweli kaka yangu Shangazi tutaendelea pia na kampeni yetu ya usichukulie poa nyumba ni choo na lengo la kampeni hii ni kutaka kubadilisha mtazamo na mwamko wa Watanzania kuhusu usafi wa mazingira ikiwemo vyoo bora. Watanzania wana nyumba nzuri, utamwona ana tv screen inchi sijui hamsini na ngapi, nenda kaangalie choo chake, nenda kaangalie vyoo katika stand zetu, nenda kaangalie vyoo katika vituo vyetu vya kutoa huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwangu mimi baada ya suala la chanjo kwa watoto suala la afya na usafi wa mazingira ndicho kipaumbele cha pili. Kwa hiyo, natuma salamu kwa Mabwana Afya wote katika Halmashauri na mikoa, haitakuwa business as usual maana Mabwana Afya wetu muda mwingi wanapoteza kwenda kukagua butcheries na mahoteli kwa sababu wanapata fedha. Kwa hiyo tumeambizana tutakaa chini na tutatoa miongozo, tunataka waende kwenye kaya na kuhamasisha masuala ya afya na usafi wa mazingira badala ya kujikita kwenda kukagua butcheries na hoteli kwa sababu pia kuna ka- asilimia fulani wanaweza kupata.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Lubeleje pia tumeangalia suala la kada ile ya kama ulivyosema environment health officers na assistant, kwa hiyo tutalijadili Wizarani, na tumeamua kwamba baada ya kulijadili tutakuja na mapendekezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala ambalo pia linahusu kuhusu afya ya mazingira na hili nimpongeze sana mdogo wangu Mheshimiwa Maria Kangoye amezungumzia suala la hedhi salama. Tunakubaliana, ndiyo kipaumbele pia kama kweli tunataka kuimarisha usafi na afya ya mazingira. Kwa hiyo, suala hili la hedhi salama hasa kwa wasichana na wanawake wa vijijini tunalipa kipaumbele. Sisi kubwa ambalo tutalifanya ni kuongea na wenzetu wa Wizara ya Fedha kama ulivyosema kuweza kuwaomba tutoe kodi katika taulo za wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini hili litawezekana, kwa sababu tusidanganyane tutatoa taulo za kike kwa sasa hivi kwa watoto wangapi, kila mwaka tunaongeza Watanzania wapya milioni mbili, na ninyi mnafahamu asilimia 51 ya wananchi ni wanawake. Kwa hiyo hili suala tunalichukua, lakini tutaendelea kuimarisha tu mazingira kwenye shule zetu pamoja na vituo vya kutoa huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, limeongelewa pia suala la ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambalo Waheshimiwa wameongea, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete pia dada yangu Mheshimiwa Dkt. Jasmine Tisekwa. Pamoja na utoaji elimu ya afya kwa jamii pamoja na kupima magonjwa tutaendelea, na ndiyo maana tunaimarisha pia kitengo chetu cha elimu ya afya kwa umma. Mheshimiwa Rita Kabati alizungumzia mpango wa kutoa chanjo ya HPV kwa watoto wa kiume pia kwa watoto ambao wana umri zaidi ya miaka 15.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeipokea hoja hii, lakini kwetu sisi tumeangalia kundi au rika ambalo ndilo liko kwenye hatari. Kwa hiyo, nchi zenye uwezo zinatoa chanjo hii kwa wavulana, zinatoa chanjo hii kwa wasichana wa zaidi ya miaka 15, sisi tunajikuna pale ambapo tunaweza. Kwa hiyo, tumeona tuanze na umri huu wa miaka tisa hadi miaka 18.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maendeleo ya jamii, kuna hoja imetolewa kuhusu mimba za utotoni ikiwemo mikakati gania ambayo tunafanya, tunaendelea kutoa elimu kwa wasichana, wazazi na walezi kutoa elimu ya sexual and reproductive health education (elimu ya uzazi na afya ya uzazi kwa wasichana) na nimeongea na Mheshimiwa Profesa Ndalichako tunaangalia pia, curriculum (mitaala yetu) ili sasa katika shule zetu tuwe na walimu, lakini pia tuwe na somo ambalo hawatafanya mitihani, lakini watoto watajua A, B, C, my right my protection, angalao wajue my body my pritection. Kwa hiyo, ni eneo ambalo tunaona linaweza kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Mwenyekiti Najma, amezungumza kuwahasi watu ambao wanabaka na kulawiti watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimelitafakari suala hili, nikaangalia Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ambayo imeingizwa katika Sheria ya Kanuni za Adhabu, tumeweka adhabu kali miaka 30, kuanzia miaka 30 mpaka kifungo cha maisha kwa mtu ambaye atakutwa amebaka. Mimi naona adhabu hii ni kali kwa kiasi fulani. Kwa hiyo, sisi tujikite katika kuelimisha jamii ikiwemo wasichana na wazazi kutimiza wajibu wao kwa malezi, lakini na watoto wa kike pia kujitambua na kujilinda na kuwajengea uwezo watoto kutoa taarifa pale ambapo wanafanyiwa vietndo vya ukatili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dalaly Kafumu amezungumzia masuala ya vituo vya afya na Wabunge wengi, kwamba, kuboresha vituo vya afya. Mheshimiwa Naibu Waziri amelijibu suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba, ujenzi wa miundombinu ya afya, zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya upo chini ya Serikali za Mitaa, TAMISEMI. Sisi kazi yetu ni kusimamia sera kuhakikisha kwamba kuna miundombinu ya kutoa huduma za afya. Hata hivyo pale ambapo tunaona kuna changamoto. Kama nilivyosema tumekuja na hoja ya uzazi salama, kwa hiyo, sisi tukaamua tutafute fedha za kuboresha vituo vya afya, ili viweze kutoa huduma za uzazi za dharura. Kwa hiyo, ni eneo ambalo..., kwa mfano, tunataka kuja na mpango wa kuboresha huduma ili tuweze kuwahudumia wagonjwa wa kifua kikuu, wagonjwa wa UKIMWI, lakini pia na ugonjwa wa malaria.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mama Mheshimiwa Riziki Lulida sijakusahau, balozi wa malaria katika Bunge hili. Malaria ni changamoto na ninafurahi kuwataarifu Waheshimiwa Wabunge tarehe 25 Aprili tunaenda Kasulu na moja ya shughuli ambayo tutaifanya ni kuzindua hali ya malaria nchini Tanzania. Habari njema ni kwamba kiwango cha malaria kimepungua na tutatoa takwimu. Tutaendelea pia kujikita katika afua za kuzuwia badala ya kusubiri kutibu. Ni kweli tunatumia fedha nyingi sana kwa ajili ya kuwatibu watu malaria wakati tungeweza kutumia viuadudu vile ambavyo vinazalishwa Kibaha kwa ajili ya kuuwa mazalia ya mbu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge kwa hiyo nimemua katika fedha za dawa ambazo tunazipeleka kwenye Halmashauri tutakata baadhi ya fedha kwa ajili ya kununua viuadudu vya kuuwa mazalia ya mbu. Kwa sababu badala ya kusubiri wanunue wenyewe hawanunui, kwa hiyo, tutawakata kwenye fedha za dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize kuhusu mapambano ya VVU na UKIMWI, Mheshimiwa Mama Salma Kikwete kwamba suala la dawa za kufubaza VVU hazipatikani kwa wakati, Mheshimiwa Mama Salma tutafuatilia, lakini kati ya eneo ambalo kwa kweli tuna uhakika wa kupata dawa ni suala pia la dawa za ARV na tunawashukuru sana wadau wetu ambao wanatupa fedha katika kutoa ARV ambao ni Global Fund pamoja na PEFA wa Marekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala pia la ongezeko la UKIMWI Dodoma, Mheshimiwa Fatma Toufiq. Ni kweli, hata mimi Tanga maambukizi kwa mujibu wa takwimu za THIMS yameongezeka kutoka 2.4 percent mpaka asilimia tano. Kwa hiyo pia tutafanya tathmini kwenye hii mikoa ikiwemo Tanga na Dodoma, ni kwa nini maambukizi ya VVU na UKIMWI yameongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, sitaki kupigiwa kengele, lakini kwa kweli, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa maoni na ushauri, na tutajibu hoja zenu kwa maandishi. Kipekee nirudie tena kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri Dkt. Faustine Ndugulile, kwa sababu wote mnafahamu hata kabla hajawa Naibu Waziri alikuwa ni mmoja wa washauri wangu katika kutatua sekta ya afya. Kwa hiyo, ninamshukuru sana kwa ushirikiano mzuri ambao ananipatia, vile vile nawashukuru sana wataalam wote, madaktari, wauguzi wote wanaotoa huduma katika vituo vyenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuwa mkali sana ninapoona hatutoi consideration, tunafanya vitendo vya kuwaumiza watoa huduma za afya. Sisemi kwamba, wote ni wazuri, wapo wabaya, lakini ni wachache…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, wale wazuri lazima tuwape heshima yao, lazima tuwathamini. Kwa mfano wauguzi, kazi ya wauguzi wanne inafanywa na muuguzi mmoja na yeye ni binadamu anachoka. Kwa hiyo, nitaomba sana viongozi wenzangu wa Serikali tuwaheshimu na kuwathamini madaktari na wauguzi kwa sababu wanatoa huduma za afya na wanatibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Rais, Katibu Mkuu Mpoki na Mama Sihaba Nkinga na Mganga Mkuu wa Serikali na wote Profesa Janabi anatuletea heshima kubwa sana katika nchi yetu na Mwenyezi Mungu ninaamini Medical Tourism itaanza Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kutoa hoja.