Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa rejea ya muda niseme tu kwamba pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na Waziri, Profesa Mbarawa na Mawaziri wake wote naomba Serikali itambue kwamba siasa za Rufiji ni ngumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siasa za Rufiji ni ngumu sana kwa sababu wananchi wetu wengi wanaamini kwamba serikali imewaacha mkono. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri ukisimama hapa utambue kwamba boma la Rufiji lilijengwa mwaka 1800. Hii inamaanisha kwamba Rufiji ilikuwepo nyakati za mkoloni, ni Wilaya ya sita nyakati za mkoloni na ni Wilaya ya 21 nyakati za uhuru (tulivyopata uhuru). Historia yetu inamuweka Bibi Titi Mohamed kuwa ni Mbunge wa kwanza Rufiji aliyepigania barabara ya kutoka Dar es Salaam kuja Kibiti na barabara hii ilijengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Warufiji hawaamini ahadi aliyoiweka Mheshimiwa Rais ya tarehe 2 Machi, 2017 kwamba barabara ya Nyamwage - Utete sasa inakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami. Nimuombe Waziri ukisimama hapa waambie Warufiji kwamba sasa barabara hii inakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami. Kwa bahati mbaya nimekagua kwenye kitabu chako sijaona ukurasa wowote unaozungumzia barabara ya Nyamwage - Utete.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana, ukisoma ukurasa wa 228 imetengwa kiasi cha shilingi milioni 200 kwa ajili ya upembuzi yakinifu barabara ya Nyamwage - Utete. Nikuombe Mheshimiwa Waziri ukisimama hapa waeleze wananchi wa Rufiji namna ambavyo Serikali sasa inakwenda kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itambue kuwa akina mama wengi wanafariki wakiwa wanalekea Utete kupata huduma za hospitali. Barabara hii ina kilometa 32 tu lakini inatumia masaa manne mpaka masaa matano kutembea kwenda Halmashauri ya Wilaya. Tangu mkoloni na baada ya uhuru, Rufiji ndiyo Wilaya pekee ambayo haiunganishwi na lami katika Halmashauri zote za awali, tangu nyakati za mkoloni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri, Warufiji sasa wamechoka, miaka 57 wamechoka, wamenituma niseme kwamba wamechoka. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri utakaposimama hapa uwaambie ahadi ya Dkt. John Pombe Magufuli ya tarehe 2 Machi, 2017; alisema mwenyewe pale Ikwiriri kwamba ataijenga barabara hii kwa kiwango cha lami kabla ya mwaka 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, siasa za Rufiji ni ngumu sana, Warufiji wanabadilisha Wabunge kila baada ya miaka mitano. Nataka niiambie Serikali kwmaba iwapo barabara hii haitajengwa basi wajue na mimi watanikosa mwaka 2020. Niiombe Serikali, lazima niseme, niiombe Serikali hiki ni kilio cha muda mrefu Mheshimiwa Waziri, nikuombe sana utuambie. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ukurasa wa 212 Mheshimiwa Waziri umezungumzia ukaratabati mdogo, nikuombe tupe ufafanuzi wa ukarabati mdogo wa barabara Nyamwage - Utete. Kama barabara hii tayari Mheshimiwa Rais aliashaahidi na ameeridhia ujengwe, sasa je, ni kwa nini ni kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya ukarabati? Ni kwa nini fedha hizi zisiende kwenye mambo mengine na barabara hii ikajengwa kwa kiwango cha lami? Tumechoka Mheshimiwa Waziri. Nikuombe sana ukisimama hapa utueleze. Tumebakiza miaka miwili tu kwenda kwenye uchanguzi, sina sababu ya kukaa kimya, dhamira yangu ni kuizungumzia barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti. lakini pia tunaomba Mheshimiwa Waziri tumeridhia ukurasa wa 196, ujenzi wa barabara ya kutoka Kibiti kuelekea Mwaseni - Mloka ambako inajegwa kwa kiwango cha lami, nikuombe Mheshimiwa Waziri ukisimama hapa sasa utuelezee kuhusu Daraja la Utete kwa sababu halimo kwenye orodha ya mipango ya Serikali, na kwamba kwa kuwa Mheshimiwa Waziri wa nishati yeye alikwambia kwamba daraja hili litajengwa ili kuweza kuwaunganisha wananchi wa Rufiji na wananchi wa Kusini, tukuombe sasa utuelezee daraja hiliā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)